• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni za China zinahamisha teknolojia Afrika

    (GMT+08:00) 2016-04-29 07:56:28

    Kampuni ya Huawei ya China, imeanzisha miradi mbalimbali kwa lengo la kuhamishia ujuzi kwa Waafrika na kutimiza wajibu kwa jamii za Afrika. Mipango ya kuhamisha ujuzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya wajibu huo, ambayo imeanzishwa kwa kushirikiana na serikali za nchi za Afrika, sio tu itaboresha hali ya maisha ya wakazi, bali pia itaongeza mahusiano kati ya China na bara la Afrika. Ronald Mutie anatuletea ripoti ifuatayo.

    Huawei hivi karibuni ilisaini makubaliano ya ushirikiano na serikali ya Nigeria kuhusu kuanzisha mpango wa maendeleo ya jamii ambao utawapa uwezo vijana 1,000 katika sekta ya habari na teknolojia ya mawasiliano ICT. Msaidizi maalum wa rais wa Nigeria anayehusika na maswala ya vijana na wanafunzi Nasir Adhama, alisema hatua hii ni sehemu ya juhudi za serikali kushughulikia suala la ukosefu wa ajira nchini humo. Alisema kati ya vijana hao 1,000 watakaopewa mafunzo na Huawei, 200 wataletwa nchini China kufundishwa zaidi ujuzi wa ICT.

    Mwezi Machi kampuni ya Huawei ilisaini mkataba wa kushirikiana na kampuni ya Kenya Techno Brain, ili kuzindua mpango wa utoaji mafunzo nchini Ethiopia, lengo kuu likiwa ni kuhamisha teknolojia katika sekta ya ICT.

    Akizungumza baada ya sherehe ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano, mkurungezi wa kampuni ya Techno Brain nchini Ethiopia Mekonnen Tesafye alisema ushirikiano huo utatoa mafunzo yanayohitajika sana ya ujuzi kwa wataalamu wa ICT nchini humo.

    Naibu afisa mtendaji mkuu wa Huawei nchini Ethiopia Cooper Qu, alibainisha kuwa kampuni yake imekuwa ikitoa miundombinu ya ICT kwa Ethiopia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa serikali, kama vile kwenye sekta za elimu, usafiri na fedha.

    Kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika ambazo zimeanzisha shughuli zake, tawi la Huawei nchini Zambia linasema lina mpango wa muda mrefu wa kutoa huduma za habari na mawasiliano kwa serikali na watu wa Zambia kwa gharama nafuu.

    Akizungumza hivi karibuni wakati wa maonyesho ya bidhaa za Huawei huko Lusaka, Zambia, mkurugenzi wa kampuni hiyo Emilion Ming alisema maoni ya serikali ya Zambia na Huawei katika siku za usoni yatawezesha kila mtu nchini humo kufurahia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya simu kwa usawa na kwa urahisi.

    Lakini sio tu sekta ya mawasiliano, China inafanya ushirikiano wa kuhamishia teknolojia barani Afrika. Makampuni ya ujenzi ya China pia yamejiunga na uzinduzi wa programu za kuwezesha uhamishaji huo huo.

    Moja ya kampuni hizo ni Kampuni ya Ujenzi wa Barabara na Madaraja CRBC ambayo inajenga reli ya kisasa nchini Kenya, na mwezi Machi mwaka huu ilizindua ripoti yake ya kwanza ya miradi ya wajibu wa jamii.

    Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa ripoti hiyo mjini Nairobi, katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi wa Kenya Bw Irungu Nyakera alisema CRBC imeleta manufaa mengi kwa jamii ambako reli inapitia.

    Ripoti hiyo inaonyesha shughuli za kampuni hiyo ya China za kuhimiza maendeleo endelevu nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na juhudi za kulinda mazingira, kuongeza ajira na mafunzo ya wafanyakazi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako