• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wachina wanavyosherehekea Siku ya mama duniani

    (GMT+08:00) 2016-05-11 21:13:24

    Wasikilizaji wapendwa, jumapili iliyopita ilikuwa ni siku ya mama. Ingawa sikukuu hiyo inatoka magharibi, katika miaka ya hivi karibuni, wachina wengi wameitumia fursa ya siku hiyo kumshukuru mama kwa upendo wake. Lakini kutokana na mchakato wa utandawazi wa miji kukua kwa kasi nchini China, upendo huo umekuwa si rahisi.

    Kabla ya sikukuu hiyo, kuna habari iliyosema kuwa mama mmoja mzee alisubiri kwenye foleni katika kituo cha basi kila asubuhi ili kumpatia kiti binti yake kwenye basi, jambo lililozusha mjadala mkubwa katika jamii. Binti huyo anaishi kwenye wilaya ya Yanjiao Mkoa wa Hebei unaopakana na jiji la Beijing, na anafanya kazi jijini Beijing. Mama yake anapanga foleni kila asubuhi kwa miaka minne mfululizo kwa ajili ya binti yake.

    Kwa kweli, katika miji ya China, mama kama huyo si wachache. Mama hao waliondoka maskani yao na kuhamia kwenye sehemu ambazo watoto wao wanaishi ili kuwahudumia watoto au kusaidia kuangalia wajukuu wao.

    Bibi Li Xiuying kutoka mji wa Suzhou, mkoani Anhui ana miaka miwili tangu ahamie mjini Beijing. Miaka miwili iliyopita, mjukuu wake alizaliwa, kwa hiyo alilazimika kubeba jukumu la kuangalia mjukuu huyo. Kabla ya kuja Beijing, ingawa hakupenda kuondoka maskani yake, alifanya uamuzi huo ili aweze kuishi na watoto wake.

    Kutokana na tofauti kati ya vijiji na miji, tabia tofauti za maisha na lahaja tofuati, pamoja na kusikia raha ya kuwa pamoja na watoto, pia aliona upweke na kukumbuka maskani yake. Bibi Li Xiuying anasema, mbali na kuangalia mjukuu pia anafanya kazi za nyumbani, lakini hawafahamu majirani, kwa hiyo baada ya watoto kwenda kazini, hana hata mtu wa kuongoa naye.

    Siku ya mama ya mwaka huu imepita, kila mwaka wakati kama huo, maua ya carnation yanayowekwa nje ya maduka na ujumbe wa salamu uliotumwa na marafiki na ndugu, zote zinazua hisia za jamii kuhusu maadili ya kutunza wazazi, na kuwakumbusha watu kuwa na moyo wa shukrani kwa wazazi.

    Kabla ya Siku ya Mama, Shirika la hisani la kimataifa Save the Children lilitoa ripoti kuhusu hali ya kina mama duniani inayohusisha nchi 178, na China inachukua nafasi ya 61 kati ya nchi hizo kwa faharisi ya kiwango cha maisha ya kina mama, ambayo ilipanda kwa nafasi 7 kuliko mwaka 2013. Ingawa hivyo, wachina wengi wanaona kuwa kina mama wa China wana majukumu makubwa kupita kiasi.

    Ushindani mkali, kuongezeka kwa gharama za kulea watoto na shinikizo la elimu ya watoto zote zinakubalika kuwa ni vyanzo vya ugumu kwa maisha ya kina mama wa China. Lakini katika mchakato wa utandawazi wa miji nchini China, kutengana kwa kina mama na watoto wao kama Bibi Li Xiuying kumekuwa mzigo mpya kwa kina mama hao.

    Hivi sasa idadi ya wachina wanaohamahama imefikia milioni 230, idadi ya wazee wanaoishi peke yake imefikia milioni 100, na idadi ya watoto wa vijijini ambao wazazi wamekwenda mijini kufanya kazi za vibarua imefikia milioni 60. Nyuma ya namba hizo, kina mama na watoto wao nchini China wanalipa gharama halisi za mageuzi ya kijamii katika zama hii ambayo utaratibu wa matunzo ya jamii bado haujakamilika.

    Kwa upande mwingine, siku hiyo ya mama pia imechukuliwa kuwa ni fursa kubwa ya kibiashara. Maduka yote yametoa matangazo ya kibiashara au kufanya shughuli mbalimbali kwa jina la siku hiyo, na vijana wengi ambao hawakuweza kurudi nyumbani kukutana na mama kwa sababu ya kazi walinunua zawadi kwa mama zao.

    Wataalamu wa mambo ya kijamii wanaona kuwa ni bora kuongea zaidi na mama kuliko kumpatia zawadi tu. Kauli hiyo ni sahihi kwa nusu tu kwa kuwa ni kweli kina mama wanatarajia zaidi kuongea na watoto wao kuliko kupewa zawadi peke yake, lakini kwa wachina ambao hawapendi kuonesha hisia zao moja kwa moja, wanatumia njia tofauti kuonesha upendo na shukrani kwa mama zao. Baadhi ya watu wanaweza kuwaambia mama moja kwa moja nakupenda mama au kumkumbatia, lakini wengi zaidi hawana mazoea ya kufanya hivyo, kwa hiyo zawadi imekuwa chombo kinachobeba upendo na shukrani hiyo bila maneno. Kwa upande huo, kuna kosa gani kuwapatia mama zawadi katika siku ya mama?

    Watoto wanaweza kuwapatia mama zawadi lakini kuwapatia faraja ya kiroho ni muhimu zaidi. Bila kujali ni wanafunzi wanaosoma nje au wafanyakazi wanaotafuta maisha mazuri, katika siku hiyo ya mama, njia bora ya kuonesha upendo kwa mama ni kuweza kurudi nyumbani kuwatembelea.

    Kutokana na sera ya mpango wa uzazi, asilimia kubwa ya vijana nchini China ni watoto wa pekee katika familia zao, na kutokana na utandawazi wa miji unaopiga hatua kwa kasi, wazee wengi zaidi wa vijijini wamebaki nyumbani huku watoto wao wakifanya kazi mijini. Hisia za wazazi kuwakumbuka watoto walioko mbali si kama tu ni vigumu kueleweka kwa watoto, na bali pia haziwezi kufajirika kwa zawadi moja au mbili. Mahitaji hayo ya kiroho ya kina mama nchini China yamekuwa undani maalumu wa siku ya mama ya kichina.

    Naam, msikilizaji, ningependa kukufahamisha kuwa, hiki ni kipindi cha mwisho cha Utamaduni Wetu. Katika kipindi cha leo tumezungumzia jinsi wachina wanavyosherehekea siku ya mama duniani. Nawatakia mama wote duniani afya njema na kila la heri! Mimi ni Guo Cong, Asante na Kwa heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako