Ripoti hiyo ambayo inatolewa kila mwaka tangu mwaka 2005 na shirika la afya duniani WHO inajumuisha takwimu mpya kutoka nchi 194 wanachama wa shirika hilo. Ripoti hiyo inaonesha kuwa mwaka 2015, wastani wa maisha duniani ni miaka 71.4, ambapo wanaume wanaishi miaka 69.1 na wanawaka 73.8.
Mkurugenzi wa idara ya takwimu ya WHO Dr. Ties Boerma anasema,
"Kwa jumla, maisha ya binadamu kote duniani yanaongezeka, na kufikia miaka 71. Lakini kuna pengo kubwa kati ya nchi tofauti. Katika nchi 12, watu wanaishi zaidi ya miaka 82, huku kukiwa nan chi 22, ambapo maisha ya watu ni chini ya miaka 60. Lakini kwa jumla, tumepata maendeleo makubwa tangu mwaka 2000."
Takwimu za ripoti hiyo zinaonesha kuwa watu wa Japan wanaishi maisha marefu zaidi duniani ya miaka 83.7 ikifuatiwa na Uswisi 83.4 na Singapore 83.1. Nchi zenye watu wanaoishi muda mfupi zaidi karibu zote ziko Afrika, ambapo watu wa Sierra Leon wanaishi miaka 50, huku watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Lesotho, Nigeria wanaishi maisha chini ya miaka 55.
Kinachotia moyo ni kwamba tofauti ya muda wa maisha kati ya wanauma na wanawake inapungua. Dr. Ties Boerma anasema,
"Tofauti ya maisha ya wanaume na wanawake inapungua, sababu muhimu ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwemo kuachana na tabia mbaya kama uvutaji wa sigara. "
Aidha, ripoti hiyo imetaja changamoto zinazopunguza maisha ya binadamu, zikiwemo ajali za barabarani, matumizi ya pombe, na kujiua. Nchi yenye kiwango cha juu zaidi cha vifo vitokanavyo ajali za barabarani ni Libya, ikifuatiwa na Liberia, Iran, Rwanda na Msumbiji.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |