• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kaa nazi ana magando yenye nguvu kubwa ya kubana inayotisha

    (GMT+08:00) 2016-11-30 09:16:54

    Kaa nazi ni mnyama mkubwa zaidi mwenye miguu yenye viungo anayeishi kwenye nchi kavu. Kaa mkubwa zaidi ana mwili wenye urefu wa sentimita 40, miguu yenye urefu wa mita moja na uzito wa kilo 4.

    Kaa huyu na kaa walii (hermit crab) wana mababu wa pamoja katika miaka milioni 260 hadi milioni 530 iliyopita. Kaa nazi wadogo pia wanahitaji kujilinda kwa kubeba gamba la konokono nyuma yake kama kaa walii anavyofanya.

    Zamani watafiti walifikiri kaa nazi hana uwezo wa kuvunja nazi. Lakini mwaka 1986 mwanabiolojia Holger Rumpff alirekodi jinsi kaa huyu anavyovunja nazi. Kwanza anaondoa makumbi ya nazi mpaka moja kati ya matundu matatu ya nazi yaonekane, halafu anapiga tundu hili kwa magando yake mpaka nazi inavunjika. Kaa huyu pia anakula matunda mengine, mbegu na miili inayooza.

    Kaa nazi anaweza kunyanyua uzito wa kilo 28 kwa magando yake. Hivi karibuni Mtafiti kutoka Japan Bw. Oka Shin-Ichiro na wenzake wamepima nguvu ya kubana ya magando ya kaa 29 wanaoishi katika bustani ya bahari huko kisiwa cha Okinawa. Upana wa miili yao ni kati ya milimita 16.2 hadi 64.5 na uzito wao ni kati ya gramu 33 hadi 2120. Matokeo yanaonesha kuwa kaa mwenye nguvu kubwa zaidi anabana gando lake la kushoto kwa nguvu ya nyutoni 1765.2. Kwa mujibu wa data hiyo, inakadiriwa kuwa nguvu ya kubana ya gando la kaa mwenye uzito wa kilo 4 inaweza kufikia nyutoni 3,300. Uking'ata kitu kwa nguvu kubwa zaidi, nguvu ya meno yako ni nyutoni 760 tu. Fikiria kidole chako kikibanwa na magando ya kaa nazi, itakuwaje?

    Kaa nazi anakua polepole, anahitaji miaka mitano kukomaa, na miaka 40 hadi 60 kuwa mkubwa zaidi. Wale wakubwa kimsingi hawana maadui, isipokuwa binadamu, ambao wanawachukulia kama chakula kitamu. Hivi sasa makundi ya kaa nazi yametoweka huko Australia na Madagascar.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako