• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ligi kuu ya Uingereza, Ibrahimovic aikomboa Manchester United, huku Everton ikiifunga Manchester City

    (GMT+08:00) 2017-01-16 09:04:29

    Mahasimu wa Jadi huko England, Manchester United na Liverpool wametoka Sare 1-1 katika Mechi ya EPL, Ligi Kuu England, iliyochezwa uwanja wa Old Trafford Mjini Manchester.

    Man United waliingia kwenye mtanange huo wakiwa hawajafungwa katika Mechi 15 zilizopita huku wakishinda Mechi 6 za EPL mfululizo wakati Liverpool, baada ya kuichapa Man City 1-0 Desemba 31, hawajashinda hata Mechi baada kufungwa 1 na Sare 2.

    Katika mechi ya jana, Liverpool walianza vyema kwa kufunga Bao la Penati ya Dakika ya 27 iliyopigwa na James Milner ambayo ilitolewa baada ya Kona ya Milner kudaiwa na Refa Michael Oliver ilishikwa kwa makusudi na Paul Pogba wakati Kiungo huyo wa Man United hakuwa akitazama Mpira na wala hakuinua Mkono juu akiwa kwenye harakati za kummaki Mchezaji wa Liverpool Dejan Lovren, kitu ambacho Wachambuzi wengi huko England walikiunga mkono.

    Dakika ya 84, Zlatan Ibrahimovic alisawazisha baada kutokea kizaazaa langoni mwa Liverpool kufuatia Kichwa cha Marouane Fellaini kugonga mwamba na kumrejea Ibrahimovic aliefunga.

    Katika mechi nyingine, huko Goodson Park Everton imechezesha mchakamchaka Manchester City kwa kuwatandika Bao 4-0 kipigo ambacho ni kibaya mno kwa Meneja wa City katika himaya yake kwenye Mechi za Ligi.

    City walikuwa nyuma 1-0 hadi mapumziko kwa Bao la Romelu Lukaku la Dakika ya 34.

    Kipindi cha Pili Everton wakatandika Bao nyingine 3 katika Dakika 47, 79 na 90 Wafungaji wakiwa Kevin Mirallas na Chipukizi Tom Davies na Ademola Lookman.

    Matokeo hayo yamewaacha City wakiwa Nafasi ya 5 na Everton wakiwa Nafasi ya 7.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako