• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Napenda kuiona China wala sio kuisikia tu"

    (GMT+08:00) 2017-03-01 16:30:47

    Theopista Nsanzugwanko kutoka gazeti la Habarileo mjini Dar es Salaam, Tanzania atatumia muda wa miezi kumi ijayo hapa China kujionea sura halisi ya nchi hii ambayo labda inasikika kila siku, lakini ni vigumu kupata nafasi ya kuitembelea kutokana na sababu mbalimbali.

    Hii ni mara ya kwanza kwa Bibi Nsanzugwanko kuja China, na amepata nafasi hii kutokana na mwaliko wa ofisi ya diplomasia ya umma ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China kupitia mpango wa "Kituo cha Mawasiliano ya Habari kati ya China na Afrika" ambao umetekelezwa kwa miaka mitatu mfululizo toka mwaka 2014. Mwaka huu, wanahabari 29 kutoka nchi za Afrika wamekuja China kushiriki kwenye mpango huo.

    Bibi Nsanzugwanko amesema kabla ya kuja China, wachina aliokutana nao nyumbani wanafanya kazi tofauti ambazo ni kazi ndogo ndogo, na alipoambiwa kuwa atakuja China, alisitasita haswa baada ya wenzake ofisini kumshawishi kuwa asije. Lakini baada ya kufika, anaona hali ni tofauti kabisa. Alisema, "Wengi ofisini waliniambia miezi kumi China? China ni nchi ngumu kuishi, utapata shida ya vyakula, kuna vyakula vingi huwezi kula, kweli wali-discouraged me. Nilirudi kwa bosi wangu bosi siwezi kwenda, lakini yeye ni mkali na aliniambia nimeshafika China, ni tofauti, utakuta vyakula tofauti unavyokula, na kujionea jinsi wachina wanavyokupokea. Kwa kweli wamenipokea vizuri sana, wao ni wakarimu sana, ni tofauti na nilivyofikirii kabla ya kuja."

    Bibi Nsanzugwanko alifika Beijing, tarehe 21, na katika siku chache zilizopita, alitembelea sehemu mbalimbali hapa mjini na alipozungumza mambo yanayomvutia zaidi, alisema, "Nilikuta ni mji tofauti, ni mji mkubwa na mzuri, wenye miundombinu tofauti tofauti ambayo sikutegemea kama naweza kuikuta hivyo. Kuna magari mengi sana, kwetu tunasumbuliwa sana na foleni, lakini huku wamejenga miundombinu ya kila aina, kurahisisha usafiri watu wanakwenda kazi na kurudi. Kitu kingine kimenifurahisha ni kuwa wachina wako makini sana katika kazi, yaani hawapotezi kwenye kazi. Tuna vitu vingi vya kujifunza hapa, cha muhimu ni jinsi wanavyothamini lugha yao, kila sehemu wanaongea lugha yao, wako very proud of na lugha yao. Kitu kingine ni jinsi China inavyolocalize vitu vyao, kwa mfano Tanzania na nchi nyingine za Afrika tunatumia Facebook au Google, lakini hapa ni tofauti, wana Facebook yao ambayo wameifanya kichina, naona China itafika mbali zaidi kimaendeleo kutokana na vitu vyao tofauti na vya nchi za magharibi."

    Kama Bibi Nsanzugwanko, Bw. Eric Biegon kutoka Shirika la Habari la Kenya KBC pia amealikwa kwenye mpango huu, na amesema mwandishi wa habari ana wajibu wa kuwaelezea watu dunia halisi, lakini hii inaamuliwa na kama anatumia macho na miguu au ni masikio tu. Alisema, "Kwa kweli mambo tunayosikia kuhusu China kwa muda mrefu yanatokana na watu wengine, mashirika ya utangazaji mbali na waafrika wenyewe. Naona ni muhimu sana sisi wanahabari kutoka Afrika tumealikwa humu humu tuje tujionee wenyewe. Programu ambyo ni ya miezi kumi nitakuwa nimejifahamisha au kujielimisha zaidi kuhusu China, kuhusu watu wa China, kuhusu uongozi wa China, kuhusu tamaduni za China, niweze nimeelewa bayana ni vipi nchi hii iliweza kufikia haya yote."

    Kama alivyosema Bw. Eric Biegon, mpango huo ndio unalenga kuwapa nafasi wanahabari wa nchi za Afrika kujionea China kwa macho, na katika miezi kumi ijayo, watafanya mahojiano, kupewa mafunzo, kuwasiliana na wachina na kutembelea sehemu mbalimbali za China.

    Akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango huo wa mwaka huu uliofanyika leo hapa Beijing, mwenyekiti wa Shirikisho la Diplomasia ya Umma la China CPDA ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa China Bw Li Zhaoxing amesema alipoombwa kutoa hotuba kwenye uzinduzi huo, alifurahi kiasi kwamba alishindwa kulala, kwani ana upendo mkubwa na Afrika na waafrika, na kwamba kati ya nchi 54 za Afrika, ametembelea 53. Ameutakia mafanikio mpango huo kwa mwaka huu, Bw. Li anasema,

    "Nawatakia wenzetu kutoka nchi za Afrika kutumia fursa hii, na chini ya usaidizi wa ubalozi wa nchi zenu hapa Beijing, juhudi za Shirikisho la CPDA na mwaandaji mwenza wa mpango huo, kutembelea na kujionea sehemu mbalimbali, na kuifahamu China ili kutoa mchango kwa ajili ya kuzidisha urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika."

    Miezi kumi haitoshi kwa mtu yeyote kuielewa nchi moja kwa undani, na pia watu husema uzuri ama ubaya upo kwenye macho ya mtu binafsi, kila mtu anaweza kuwa na tafsri yake kuhusu China, lakini kama ukitumia macho na sio masikio, inakaribia zaidi hali halisi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako