China imeweka lengo la ongezeko la pato la taifa GDP kuwa asilimia 6.5 kwa mwaka huu, kiasi ambacho ni cha chini zaidi katika miaka 25 iliyopita, na pia ni pungufu kuliko asilimia 6.7 ya mwaka jana.
Kwa mujibu wa ripoti ya kazi za serikali iliyotolewa leo na waziri mkuu wa China Li Keqiang kwenye mkutano wa mwaka wa Bunge la Umma la China, lengo hilo linalingana na kanuni za kiuchumi na halisi, na kwamba litasaidia kutuliza matarajio ya soko na kurahisisha mabadiliko ya kimuundo. Pia litasaidia kufanikisha lengo la kujenga jamii yenye maisha bora katika pande zote.
Ripoti hiyo pia imesema, sababu muhimu ya kusisitiza hitaji la kudumisha ukuaji tulivu ni kuhakikisha soko la ajira na kuinua kiwango cha maisha ya watu. Lengo la mwaka huu kwa utengenezaji wa nafasi za ajira mijini ni zaidi ya milioni 11, likiwa ni ongezeko la nafasi milioni 1 kuliko mwaka jana.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |