• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waziri Mkuu asisitiza kuwa China itaendelea kuwa wazi kwa biashara

    (GMT+08:00) 2017-03-06 15:09:41

    Mkutano wa tano wa Bunge la awamu ya 12 la umma la China unaendelea leo hapa Beijing, kwa wawakilishi kujadili ripoti ya mipango ya kazi za serikali kwa mwaka huu. Jana kwenye ufunguzi wa mkutano waziri Mkuu Bw Li Keqiang alianza kwa kuwasilisha ripoti hiyo mbele ya bunge ili ijadiliwe. Ripoti hiyo imekuwa na mambo mbalimbali yanayofuatiliwa, ili kujua mwelekeo wa uchumi wa China kwa mwaka huu utakuwaje, na utakuwa na athari gani kwa uchumi wa nchi nyingine duniani na hata uchumi wa dunia.

    Moja kati ya mambo yanayofuatiliwa zaidi na watu duniani kwenye ripoti ya waziri mkuu, ndani na nje ya China, ni uchumi. Sababu ni kuwa katika miaka michache iliyopita China imekuwa ni injini muhimu kwenye kufufua na kuchochea ukuaji wa uchumi wa dunia. Kwa hiyo anaposimama Waziri Mkuu wa China kuongea kuhusu uchumi wa China, anachoongea kinawahusu watu wa nchi mbalimbali na kinafuatiliwa na dunia nzima. Ndio maana sehemu kubwa ya ripoti yake ilihusu uchumi. Kwa nchi za Afrika ambazo uchumi wake unaendelea kufungamana na kuhimizwa na maendeleo ya uchumi wa China, ripoti hiyo pia ina umuhimu mkubwa.

    Kingine kinachofanya ripoti hii ifuatiliwe, ni kwamba imetolewa kwenye mazingira ambayo sauti zinazokosoa au hata kupinga mafungamano ya kibiashara kwenye baadhi ya nchi kubwa duniani zimeanza kusikika. Kutoka Marekani ambako serikali mpya imekuwa ikitishia kupandisha kodi dhidi ya bidhaa kutoka nje, hadi barani Ulaya ambako Uingereza imejitoa Umoja wa Ulaya, na makundi ya mrengo wa kulia yenye mwelekeo wa sera za kujilinda (Protectionism). Kwa hiyo kulikuwa na kila hamu ya kutaka kujua mwelekeo wa China ambayo kwa sasa ni moja ya mihimili ya uchumi wa dunia utakuwaje.

    Kwenye hotuba Waziri mkuu ameithibitishia dunia kuwa China haitakuwa na mwelekeo huo, na itaendelea kuwa wazi kwa biashara na uwekezaji kutoka nje. Zaidi ya hayo itaongeza kasi ya kujenga mfumo mpya ulio wazi wa uchumi, na kuimarisha ufunguaji mlango. Huu ni uhakikisho muhimu kwa nchi zinazofanya juhudi kujiendeleza kwa kufanya biashara na China.

    Pamoja na kuwa baadhi ya wanahabari wamefuatilia zaidi uamuzi wa serikali kupunguza lengo la ongezeko la uchumi kutoka asilimia 6.7 ya mwaka jana hadi asilimia 6.5, na kuona kama mwelekeo mbaya wa kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, waziri mkuu ameondoa hofu hiyo na kusema hali ya uchumi kwa mwaka huu itaendelea kuwa imara. Lakini pia ametoa takwimu nyingine ambazo zinaonyesha kuwa kupungua kwa kasi ya ongezeko la uchumi, haina maana kuwa kila kitu kinapungua. Kwa mfano ametaja kuwa serikali itaongeza nafasi milioni 11 za ajira, likiwa ni ongezeko la nafasi milioni moja kuliko mwaka jana. Nguvu kazi mpya inayoongezeka na mapato watakayopata, vitasaidia kuchochea maendeleo ya uchumi na hata kupanua matumizi ya ndani. Hii pia ni habari nzuri kwa nchi zinazouza bidhaa kwenye soko la China.

    Vilevile, hotuba ya waziri mkuu imeakisi mambo mengi yanayofuatiliwa na jamii ya China. Kwa muda mrefu ongezeko la uchumi lilikuwa likiangalia tarakimu za pato la taifa, lakini mambo kuhusu ubora wa maisha ya watu wa China, hali ya mazingira na hata umaskini hayakuwa na msukumo mkubwa. Waziri Mkuu Li amesema mambo hayo yatapewa msukumo mkubwa katika kazi za mwaka huu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako