Mkutano wa 5 wa Bunge la 12 la Umma la China na Mkutano wa 5 wa Baraza la 12 la Mashauriano ya kisiasa la China inafanyika mjini Beijing, mojawapo ya masuala muhimu yatakayojadiliwa kwenye mikutano hiyo miwili ni mahusiano ya kibiashara kati ya China na dunia ikiwemo Afrika. Mwandishi wetu wa Nairobi Ronald Mutie amezungumza na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta anayefundisha masomo ya sayansi ya siasa Dkt Otiato Wafula.
Swala: Una matarajio gani katika mikutano hii miwili?
Natarajia kwamba hivyo vikao viwili vitajaribu kujenga mtazamo wa China wa sera ya njia moja ukanda mmoja ambayo ni ya kihistoria na ambayo ndio kama upeo wa China kutaka kutawala dunia kiuchumi na kisiasa na hata pia kitamaduni. Hivyo nafikiria kwenye hiyo mikutano watatathmini na watakuwa wanaangalia sana mambo hayo. Na matokeo yake yatakuwa kama vigezo vya kuonyesha ni umbali gani wanataka kwenda katika miaka mitano ijayo.
Swala: Unaweza kuzungumzia swala la uwekezaji na biashara kwa muktadha wa mikutano hiyo miwili.
Baraza la kitaifa la China ambalo ndilo lenye nguvu sana ya kisiasa nchini humo ni sauti moja, na unajua China ina mtaji mkubwa sana na pale baraza hilo linapopitisha pesa kama bilioni 10 ama zaidi inakuwa ni sera ya Afrika nzima. Kuna uwiano fulani.Lakini mataifa ya kimagharibi utapata ya kwamba wanapenda kufanya kazi na Afrika taifa kwa taifa na hivyo kunahitajika sahihi nyingi sana.
La pili ni kwamba nchi zenyewe kuna wafaransa, kuna waingereza, wajerumani na kila mtu ana mipango yake. Pesa zao zinaweza kuwa zinalingana na zile za China lakini uzuri wa China ni kwamba unafanya mkataba na mtu mmoja. Pia ukiangalia Mchina sasa anajaribu kutuweka pamoja kupitia makundi kama vile ECOWAS, EAC na unaona kama sasa Kenya inajenga reli lakini mchina anatuhimiza reli hiyo iende mpaka Uganda ili kufanya mshikamano wa kikanda na hicho ni kitu ambacho mataifa ya magharibi hayajawahi kufanya na hawapendi kuona mataifa ya kiafrika yakishikana lakini mchina anapofanya mambo kama hayo ya kutuunganisha, mwafrika anakuwa na kiu na kumuona kama ndugu wa karibu ambaye anatuelekeza kwenye njia zuri ya kiuchumi.
Swala: Kitu gani kinakupendeza katika mfumo wa kisiasa wa China?
Kuna maadili, na mimi binafsi naona kwamba matokeo na mafanikio makubwa ya serikali ya China yanatokana na maaadili, kwa jamii itakuwa vigumu ufikirie kuiba kule China. Wakati mwingine haya mambo ya haki za kibinadam tunayatumia vibaya. Kwa mfano mtu anafanya makosa kama kushikwa na pembe za ndovu lakini kwanza serikali inasema uchunguzi ufanywe, apelekwe kortini, lakini yeye ana pesa atamnnua wakili na mnaishia kupelekana katika mviringo. Lakini kama serikali ina nguvu kama serikali ya China hakuna wakati wa kupoteza kila mtu anajua umefanya makosa na serikali ina nguvu za kukuchukulia hatua na hiyo hatua itakuwa kali kiasi ya kwamba jirani yako mwingine ambaye alikuwa anafikiria hivyo hatajaribu. Nadhani hilo ndio somo kubwa ambalo tunafaa kusoma kutoka kwa serikali ama jamii ya kichina.
Swala: Una tathmini gani kuhusu uwekezaji wa China Barani Afrika?
Ni ukweli kwamba kila mtu ataona kuwa China imewekeza sana hasa kwenye miundo mbinu kama barabara, reli, maji safi. Ukienda kwenye bandari, na viwanja vya ndege utaona ni kweli kwamba mchina amesisimua na ni ukweli kuna msisimko mpya wa kiuchumi Afrika na ndio maana unaona sasa kila nchi kutoka Liberia hadi Ethiopia kutoka Somalia hadi Senegal kila mtu amechangamkia dhana hii ya China ya kujaribu kuchochea uchumi wa kiafrika kupitia miundo mbinu. Kufuatana na falsafa za tangu jadi tunaamini kwamba miundo mbinu ikiwekwa itawezesha mtu yeyote ambaye anataka kufanya biashara na kuchangia mwamko mpya kwa kila mtu kwamba kuna nyenzo hapa za kufanya biashara
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |