• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waziri wa mambo ya nje wa China asema China itaendelea kuzisaidia nchi za Afrika bila ya kujali mwenendo wa uchumi wa dunia

    (GMT+08:00) 2017-03-08 17:21:24

    Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi ameongea na waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali kando ya Mkutano wa bunge la umma la China unaoendelea hapa Beijing. Kwenye mkutano huo, Wang Yi alieleza sera za China na mambo yanayohusu China katika mazingira ya sasa ya dunia.

    Kuna mambo mengi aliyozungumzia Waziri Wang ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu hali ya kikanda kama vile maendeleo baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora, na Marekani kuweka mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora, maendeleo ya pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja", na hata maandalizi ya mkutano wa BRICS.

    Kwa eneo la Afrika, kilichofuatiliwa na kufurahisha zaidi kwenye mkutano huo, ni uhakikisho aliotoa waziri Wang kuhusu mwelekeo wa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika. Amesema bila kujali hali ya kimataifa na ya dunia itakavyokuwa, uungaji mkono wa China kwa Afrika hautapungua. Amesema kinachofanya ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika uwe wa kipekee, ni kwamba China huwa inatimiza ahadi. Ametolea mfano ahadi ya dola bilioni 60 iliyotoa China kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, ambazo amesema kuwa tayari China imetoka karibu nusu ya fedha hizo, na nusu nyingine iko katika mchakato wa kutolewa.

    Kwa nchi za Afrika Mashariki, tunaweza kusema kuna hali ya faraja kwa kuwa Waziri Wang ametaja kwa majina nchi za Tanzania, ambako amesema ujenzi wa mradi wa bandari unaendelea, na Kenya ambako ujenzi wa reli ya Standard Gauge unaendelea. Tanzania na Kenya kutajwa kwa majina kwenye mkutano mkubwa unaofuatiliwa na dunia nzima, sio tu kunaonyesha kuwa Afrika ni sehemu muhimu ya sera ya kidiplomasia ya China, bali pia inaonyesha nafasi muhimu ya nchi hizo kwa China. Sio siri kuwa kuna miradi mingi inayoendeshwa na China karibu katika nchi zote rafiki za Afrika, na karibu nusu ya dola bilioni 30 ambazo zimetumwa barani Afrika zimeenda kwa nchi mbalimbali, lakini Tanzania na Kenya ndio zimetajwa. Jambo hili ni ishara nzuri.

    Japo muhimu lingine ambalo lilisubiriwa na watu ni kuwa, tangu waziri mkuu wa China Bw Li Keqiang alipotangaza kupungua kwa makadirio ya ongezeko la uchumi kwa mwaka huu kutoka asilimia 6.7 hadi asilimia 6.5, kulikuwa na wasiwasi kuwa mwelekeo huu wa kupungua kwa kasi ya ongezeko la uchumi wa China, unaweza kumaanisha kupungua kwa uungaji mkono wa China kwa nchi za Afrika. Waziri Wang amekumbusha kuwa China iliwahi kutoa misaada zamani, na amesisitiza kuwa China itaendelea kutoa misaada. Amekumbusha kuwa kwa sasa kuna sifa tatu kwenye uhusiano wa China na nchi za Afrika. Kwanza unapiga hatua kutoka kuongozwa na serikali na kuendelea kuongozwa na soko, pili kutoka biashara ya bidhaa na kuwa ushirikiano wa kiviwanda, na tatu ni kutoka ukandarasi hadi uwekezaji. Mabadiliko haya yanayoonyesha kuwa uhusiano na ushirikiano una mwelekeo wa kivitendo (practical) na utakuwa na manufaa kwa serikali na watu wa pande zote mbili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako