• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wakimbizi wapya wa Somalia wafurika katika kambi ya Dadaab nchini Kenya kutoroka ukame

    (GMT+08:00) 2017-04-11 09:13:48

    Ukame unaoathiri sehemu mbalimbali Somalia umesababisha angalau wasomali 2,000 kuvuka mpaka na kuingia katika kambi ya Dadaab nchini Kenya katika miezi ya hivi karibuni.

    Haya ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa.

    Taarifa kutoka shirika la Umoja wa Mataifa zinasema kuwa wakimbizi wengine wengi wako njiani kuelekea katika kambi ya Dadaab,ili kutoroka ukame nchini Somalia.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inakadiriwa kuwa karibu wakimbizi 100 wapya waliowasili hivi karibuni ni miongoni mwa wakimbizi ambao walirudi Somalia kwa hiari kutoka kambi za Kenya katika sehemu ya mpango wa kurudisha wakimbizi wa Somalia nchini kwao kwa hiari.

    Shirika hilo limesema visa vya watu kutoroka makazi yao kutokana na ukame Somalia vinazidi kuongezeka maradufu.

    Zaidi ya wasomali 500,000 wamelazimika kutoroka makazi yao tangu mwezi Novemba mwaka jana,huku asilimia 52 ya jumla ya watu waliotoroka makazi yao ikitokea ndani ya mwezi mmoja uliopita.

    Huyu hapa ni Bi Aisha amewasili katika kambi ya Dadaab.Amemuacha mumewe na wazazi wake Somalia.

    "Tumekuja hapa kwa sababu hakuna chakula.Hatukuwa na pesa za kununua chochote njiani.Tulitembea kwa takriban siku thelathini,tulilala njiani na hatimaye tumefika hapa.Tulipovuka boda ndio tukaletwa hapa katika kambi ya Dadaab"

    Hawo Ali anasema mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu alifariki wakiwa njiani kuelekea katika kambi ya Dadaab.Anasema safari hiyo ilikuwa nzito na yenye dhiki.

    "Hatukusafiri hapa kwa gari,tulitembea kwa siku 30.Kuna mwanamke ambaye alijifungua njiani.Tulipata tabu sana"

    Mohamed Wadi ni miongoni mwa wakimbizi waliowasili katika eneo la Dhobley wakiwa katika safari ya kuelekea Dadaab kutoka sehemu mbalimbali za kusini mwa Somalia walikoathirika na ukame.

    "Ukame umetuathiri vibaya sana.Watu wamepoteza mifugo yao na ardhi imekauka.Hakuna maji,kuna ugonjwa kipindupindu na watu wanakufa.Joto limekuwa kali mno kwa watoto"

    Uhamiaji mkubwa wa walio na njaa na kiu katika kambi ya Dadaab utahatarisha au hata kuregesha nyuma hatua zilizopigwa miaka miwili nyuma za kuwarudisha kwa hiari wakimbizi nchini Somalia.

    Takriban raia wa Somalia 60,000 wamerudi nyumbani kutoka Dadaab tangu kuanzishwa kwa mpango wa kurudi nyumbani kwa hiari mwezi Desemba 2014.

    Umoja wa Mataifa unasema wakazi wa Dadaab 20,515 wamesaidiwa kurudi Somalia mwaka huu.

    Wengine 21,940 wamesajiliwa kwa ajili ya kurudi nyumbani kwa hiari.

    Shirika la Umoja wa Mataifa linaripoti kuwa kufikia tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu idadi ya jumla ya wakimbizi katika kambi ya Dadaab ilikuwa ni 256,192.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako