• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Pendekezo la ukanda mmoja na njia moja litasaidia kukuza Kenya kiviwanda asema Rais Uhuru Kenyatta

    (GMT+08:00) 2017-05-10 20:27:47

    Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema pendekezo la "Ukanda mmoja, Njia moja" litasaidia nchi yake kuwa na uwezo mkubwa wa kiviwanda na kuongeza nafasi za ajira.

    Kenyatta ambaye anatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa kilele wa baraza la kimataifa la "Ukanda mmoja, Njia moja" baadaye mwezi Mei hapa mjini Beijing, amesema pia miradi ya miundo mbinu inayofadhiliwa na China nchini Kenya itasaidia sio tu nchi hiyo lakini pia na kanda ya Afrika Mashariki kiuchumi na kuongeza uwekezaji.

    Mbele ya mkutano huo wa kilele wa tarehe 14 na 15 mwezi huu rais Uhuru Kenyatta ameandaa mkutano na waandishi wa habari kuelezea agenda yake kwenye mkutano huo na pia kuhusu pendekezo la Ukanda mmoja na njia moja.

    Kenya ikiwa ni nchi ambayo tayari imeanza kuvuna matunda ya pendekezo hilo lililotolewa na rais Xi Jinping wa China mwaka 2013, Kenyatta anauona kama mwanzo mpya wa kunufaisha pande zote mbili.

    "Wazo kuu la pendekezo la ukanda mmoja na njia moja ni kufungua maeneo na kukuza ushirikiano wa kikanda, na China inaongoza agenda hii. Naamini kwamba ni agenda yenye lengo la kuwezesha watu na pia kuboresha biashara na uwekezaji kwa pande zote mbili. Hivyo sina shaka kwamba mwishowe kutakuwa na ongezeko la biashara kutoka China kuja Afrika na pia kutoka Afrika kwenda China"

    Kulingana na rais Uhuru Kenyatta pendekezo la "Ukanda mmoja, Njia moja" pia litawezesha kukua kwa viwanda barani Afrika na kuongeza nafasi za ajira.

    Uwepo wa ajira kwa sasa unashudiwa kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi ambayo inatarajiwa kufunguliwa mwanzoni mwa mwezi Juni.

    Uhuru Kenyatta anaitaja reli hiyo kama mlango wa Afrika Mashariki.

    "Tulikubaliana ya kwamba hii ni reli ambayo itasaidia kuunganisha nchi za Afrika Mashariki, na tukakubaliana ya kwamba reli hii ikijengwa itatusaidia kupanua uchumi, kupanua nafasi za kazi na kupanua nafasi ya kuendeleza uchumi zaidi na kumaliza umaskini na pia kupunguza bei ya wafanya biashara . Na tukifanya hivyo tutapatia watu wetu nafasi ya kujenga viwanda na mambo mengine ambayo sasa hatuna kwa sababu ya ugumu wa usafiri. Kwa hivyo sisi tunashukuru sana serikali ya China kwa vile wametusaidia. Kufika Nairobi hatujamaliza kazi, ile ni robo ya safari na tunataka kuona hiyo reli ikitembea hadi Uganda, Rwanda, DRC na hatimaye kunganisha bahari ya hindi na ile ya Atlantic kwa kupitia uhusiano wetu na watu wa China"

    Ingawaje biashara kati ya Kenya na China imeendelea kuongezeka lakini bado inaegemea upande wa China.

    Taakwimu za mwaka 2015 zinaonyesha kwamba China iliuzia Kenya bidhaa za shilingi bilioni 320.8 lakini Kenya iliuza bidhaa za dhamani ya shilingi bilioni 8.4 hasa yakiwa ni mauzo ya chai, madini ya titanium kahawa na matunda.

    Lakini kwenye ziara yake nchini China rais Kenyatta anasema swala hilo la uwiano wa kibiashara litakuwa ni mojawapo wa yale atakayoangazia.

    "Kuhusu Kenya, mojawapo wa maswala muhimu nitakayowasilisha mezani ni kwamba tungependa kuona ongezeko la kiwango cha bidhaa zinazouzwa na Kenya kwenye soko la China kwa sababu kama vile tunavyosema tunahitaji kuwa na ushindi wa pande mbili. wakati tukifungua soko letu kwa China, pia tunawaomba marafiki wetu wa China kufungua soko lao kwa bidhaa zetu."

    Lakini mbali na na biashara na uwekezaji pia Kenya na China zimepiga hatua kubwa kwenye uhusiano wa watu kwa watu.

    Idadi ya wachina wanaoishi na kufanya kazi au biashara nchini Kenya inaendelea kuongezeka huku nao wakenya pia wakienda china kwa shughuli za masomo na biashara.

    Kwenye ziara yake Rais Uhuru Kenyatta atakuwa mwenyekiti wa hafla ya kujadili mabadilishano ya watu kwa watu.

    Kenyatta anasema uhusiano huo unahitaji kukuzwa zaidi.

    "Hata wakati bado hatukuwa na uhusiano wa kiuchumi kama ilivyo sasa, uhusiano wetu wa kwanza ulikuwa ni wa watu kwa watu. Tulikuwa na mabadilishano kwenye sekta za michezo, utamaduni. Sasa tuna wakenya wengi ambao wanajiunga na taasisi za kujifunza lugha ya kichina na huo ni ubadilishaji mzuri wa kilugha ambayo ni muhimu. Hivyo wakati tukiangazia uchumi hatufai kusahau maeneo mengine ya ubadilishanaji."

    Viongozi 28 wa nchi na serikali watahudhuria mkutano wa Beijing wa Ukada moja na njia moja , barani Afrika ikiwa ni Rais wa Uhuru Kenyatta Kenya , na waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Hailemariam Dessalegn.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako