• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kongamano la maonesho ya biashara na viwanda Afrika Mashariki laanza mjini Kigali,Rwanda

    (GMT+08:00) 2017-05-23 09:53:56

    Kongamano la pili la maonesho ya Biashara ya Viwanda Afrika Mashariki (East Africa Manufacturing Business Summit-EAMBS) limeanza rasmi hii leo tarehe 23 katika hoteli ya Serena jijini Kigali,Rwanda. Kongamano hili linawaleta pamoja wamiliki wa viwanda,wafanyabiashara na wawekezaji kwa lengo la kukuza biashara kati ya mataifa ya Afrika Mashariki.

    Kongamano hili la pili la maonesho ya viwanda na biashara limeandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,Baraza la Biashara la Afrika Mashariki,serikali ya Rwanda na Mataifa mengine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Kongamano hili litafunguliwa rasmi baadae leo na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

    Zaidi ya maafisa 300 katika sekta ya viwanda na kilimo biashara,maafisa wa ngazi za juu wa utungaji sera,taasisi mbalimbali za fedha kutoka Afrika na ughaibuni wameshiriki katika kongamano hili.

    Sekta binafsi inatarajiwa kutumia kongamano hili kusukuma kasi ya mageuzi ya viwanda yanayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta za kimkakati za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Naibu Katibu Mkuu wa EAC Mh.Christophe Bazivamo amesema EAMBS inatoa jukwaa zuri serikali katika kanda kuhusisha sekta binafsi katika hatua muhimu zinazohitajika kuinua viwango vya uwekezaji katika viwanda.

    Bazivamo amesema kwamba EAC tayari imetambua maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika kanda.

    Aidha EAMBS itatilia maanani jukumu la wawekezaji waishio ughaibuni na kongamano hili litajadili na kutoa masharti spesheli kuhusu ni vipi wawekezaji hao wanaweza kushawishiwa wawekeze katika ukanda wa Afrika Mashariki.

    Wafanyabiashara wataonyesha bidhaa mbalimbali walizokuja nazo kama vile magari,fanicha,viatu,chuma,nguo,vitambaa na ushonaji,bidhaa na vifaa vya kilimo,madawa na vipodozi,saruji,kemikali,rangi n.k.

    Baadhi ya vigogo ambao wamehudhuria kongamano hili na wanatarajiwa kuzungumza ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame,Katibu Mkuu wa kongamano la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) Dkt Mukhisa Kituyi,Balozi Liberat Mufumukeko,Katibu Mkuu wa EAC,pamoja na mawaziri kutoka mataifa wanachama wa EAC,ambao watajadiliana na sekta binafsi kuhusu jinsi ya kuinua viwango vya uwekezaji katika viwanda.

    Kongamano hili la pili la EAMBS litakuwa na vikao vitakavyojadili mtizamo wa sekta ya umma na binafsi kuhusu viwanda katika kanda ya Afrika Mashariki,mkataba wa Afrika Mashariki na itifaki zake,ubunifu na ufadhili wa muda mrefu wa sekta ya viwanda na ushiriki wa wanaoishi ugenini,jukumu la serikali za EAC katika kukuza bidha za ndani hasa chuma,madini vifaa vya ujenzi,ushindani ulioboreshwa kupitia taaluma na uvumbuzi,miongoni mwa mambo mengine.

    Kongamano hili la siku tatu linaanza leo hadi tarehe 25 Mei,2017.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako