• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uchunguzi umeanzishwa kubaini kifo cha waziri wa usalama wa kitaifa Kenya Jenerali Joseph Nkaissery

    (GMT+08:00) 2017-07-10 10:15:33

    Uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichosababisha kifo cha waziri wa usalama wa kitaifa wa Kenya Joseph Nkaissery siku ya jumamosi alfajiri. Kifo cha Waziri Nkaissery kimewashangaza wengi kwani yeye alikuwa mmoja wa viongozi wa juu wa serikali waliohudhuria maombi ya kitaifa katika uga wa Uhuru Park mnamo Ijumaa, Julai 7.

    Mnamo jumamosi asubuhi wakenya wakenya waliamkia habari za kushtusha.Msimamizi wa wafanyakazi wa ikulu ya Rais,Joseph Kinyua,katika taarifa,alisema Nkaissery amefariki usiku wa kuamkia jumamosi baada ya kuzimia nyumbani kwake na kukimbizwa katika hospitali ya Karen jijini Nairobi.

    Kifo cha Nkaissery kimeiacha familia yake pamoja na viongozi serikalini na maswali mengi wakidai kuwa alikuwa buheri wa afya na hakuonyesha dalili zozote za kuzorota kwa afya,hali ambayo imesababisha minong´ono kwamba huenda aliuawa.

    Wataalam wa upekuzi wanafanya uchunguzi katika mkahawa wa Bomas alikozuru mwendazake na kushiriki kinywaji, nyumbani kwake mtaani Karen na hifadhi ya maiti ya Lee, kukusanya chembe chembe muhimu zitakazoweza kukitegua kitendawili cha kifo chake.

    Mnamo ijumaa Nkaissery alionyesha kuwa mchangamfu na aliendelea na shughuli zake kama kawaida,pia alihudhuria maombi ya kitaifa katika uga wa Uhuru Park akiwa na Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto,pamoja na viongozi wengine.

    Baada ya hapo alirudi ofisini na hatimaye jioni kukutana na rafiki yake wa karibu Francis Charles Mugambi katika mkahawa wa Bomas.

    Nkaissery alifika kwake na kula chakula cha jioni pamoja na familia yake.

    Charles Mugambi anasema alipigiwa simu na familia ya Nkaissery mwendo wa saa sita unusu akiambiwa kuwa Nkaissery amezirai na hali yake sio nzuri.

    Rais Kenyatta ametoa wito kwa wakenya wote kudumisha amani na kuendelea kuwa kitu kimoja wakati uchunguzi wa maiti ya Nkaissery ukitarajiwa kufanywa leo.

    "Wakati tunasubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti yake ili tuweze kubaini kilichosababisha kifo chake,natoa wito kwa wakenya kuwa watulivu na kuendelea kuwa kitu kimoja".

    Wakati huo huo Rais Kenyatta alimteua waziri wa elimu Fred Matiang´i kuwa kaimu wa Wizara ya usalama wa ndani.

    "Hakutakuwa na pengo katika ulinzi wa nchi yetu.Leo asubuhi nimechukua uamuzi wa kumteua Dkt Fred Matiangí kama Kaimu Waziri wa usalama wa ndani kuhakikisha kwamba hakuna pengo katika wizara hiyo muhimu"

    Kifo cha Waziri Nkaissery kimetokea wakati nchi inaelekea kufanya uchaguzi mkuu tarehe 8 mwezi Agosti,ikiwa sasa zimesalia siku 28 kabla ya uchaguzi mkuu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako