Katika maadhimisho ya miaka 90 ya kuanzishwa kwa jeshi la ukombozi la umma la China, gwaride la kijeshi limefanyika leo asubuhi katika kituo cha kijeshi cha Zhurihe, mkoani Mongolia ya Ndani, kaskazini mwa China.
Rais Xi Jinping wa China ambaye pia ni katibu mkuu wa chama tawala nchini China, Chama cha kikomunisti, na mwenyekiti wa kamati ya kijeshi ya chama, alikagua gwaride la kijeshi, ambapo akisisitiza kuwa, jeshi la China lina imani na uwezo wa kushinda maadui wanaolivamia taifa, na kulinda mamlaka ya taifa, usalama na maendeleo yake.
Gwaride la kijeshi lilianza leo saa 3 asubuhi. Hilo ni la kwanza kufanyika katika maadhimisho ya kuanzishwa kwa jeshi toka Jamhuri ya watu wa China kuasisiwa mwaka 1949. Katika kituoc cha kijeshi cha Zhurihe, ambacho ni kikubwa zaidi cha kufanyia mazoezi ya kijeshi barani Asia, wanajeshi zaidi ya elfu 12, vifaa 600 na ndege zaidi ya 100 za aina mbalimbali zilikaguliwa na viongozi wa China.
Baada ya kukagua gwaride hilo, rais Xi Jinping aliwahutubia wanajeshi, akisema,
"Ni baraka ya umma kuishi kwa amani, na ni wajibu wa jeshi la umma kulinda amani. Lakini hali haijatulia duniani, na haina budi amani ilindwe. Ninaamini kwamba, jeshi letu la kishujaa lina imani na uwezo kabisa wa kushinda maadui wanaolivamia taifa, kulinda mamlaka ya taifa, usalama na maendeleo yake, na kutoa mchango kwa ajili ya kufanikisha ustawi wa taifa la China na kulinda amani duniani."
Rais Xi Jinping pia alitoa agizo akitaka jeshi la China kuongeza uwezo wa mapambano na kuimarisha ulinzi wa kisasa wa taifa. Alisema, jeshi la ukombozi la umma la China ni lazima lichukulie uwezo wa mapambano kama kiwango pekee cha kimsingi, kujizatiti kwa vita, na kujenga jeshi imara ambalo siku zote liko tayari kwa vita, kuwa na uwezo wa mapambano na kwa hakika linapata ushindi.
Vile vile alitaka maaifsa na askari kujenga jeshi lenye ufahamu wa kisiasa, kuimarisha jeshi kwa kufanya mageuzi, kuendeleza jeshi kwa sayansi na teknolojia, na kusimamia jeshi kwa mujibu wa sheria, ili kuinua kiwango cha ulinzi wa kisasa taifa na jeshi la kisasa.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya ulinzi ya China, gwaride hilo la kijeshi limefanyika kwa mujibu wa mpango wa mazoezi uliopangwa kabla ya mwaka huu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |