• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wafanyabiashara nchini Kenya wapata hasara wakati uchaguzi mkuu ukikaribia

    (GMT+08:00) 2017-08-04 10:35:30

    Wafanyabiashara wadogo katika jiji la Nairobi nchini Kenya wanapata hasara wakati biashara zao zikishuka kidhahiri kutokana na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini humo.

    Wafanyabiashara hao, hususan wanaouza bidhaa kama nguo, viatu, na simu za mkononi wanasema mauzo yamepungua kwa sababu mawazo ya wateja yamehamia kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika jumanne wiki ijayo. Hivi sasa wafanyabiashara wanachofanya ni kufungua maduka yao, na kukaa kusubiri siku imalizike kabla ya kurejea makwao, huku wakiomba uchaguzi huo ufanyike na kumalizika mapema.

    Patrick Kimani, anayemiliki duka la kuuza viatu jijini Nairobi anasema, biashara kwa sasa ni mbaya, na kwamba mambo hayajawahi kuwa mabaya kama ilivyo sasa. Kwa mtazamo wake, anasema hata uchaguzi wa mara ya mwisho ulikuwa mzuri kuliko sasa. Kimani anasema, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, biashara ilishuka siku tatu kabla ya uchaguzi, lakini safari hii, wafanyabiashara wameanza kushuhudia kushuka kwa biashara takriban wiki mbili kabla ya uchaguzi. Anaendelea kusema, kabla ya fikra za uchaguzi kuanza, alikuwa akiuza bidhaa zenye thamani ya dola 100 za kimarekani kwa siku, lakini sasa, hata kupata dola 20 ni kazi kubwa. Idadi kubwa ya wafanyabiashara pia hawajaleta biashara mpya kwenye maduka yao, wakichukua mtazamo wa kusubiri na kuona.

    Rais Uhuru Kenyatta anatafuta kuchaguliwa tena dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga, ambaye ni mgombea kupitia muungano wa upinzani wa NASA.

    Muuzaji wa computer jijini Nairobi Gilbert Wandera anasema, sala yake ni kwamba uchaguzi huu utamalizika katika raundi ya kwanza ili watu waweze kuendelea na maisha yao. Anasema kama hakuna mgombea atakayeshinda katika raundi ya kwanza na ikalazimu kuingia raundi ya pili, jambo hilo litaongeza muda wa kufanyika uchaguzi na hilo litaathiri vibaya biashara.

    Katika eneo la Gikomba, ambalo ni maarufu kwa bidhaa za mitumba, wafanyabiashara wanalalamikia mauzo madogo huku wakigundua kuwa wasambazaji wameacha kuagiza bidhaa kwa wingi. Vincet Moses, muuzaji wa viatu, anasema idadi ya watu wanaotembelea soko hilo imepungua kwa kiasi kikubwa, hakuna watu wa kununua bidhaa zao, hivyo na wao hawawezi kununua kutoka maduka ya jumla. Maelfu ya watu wanaondoka jijini Nairobi kuelekea miji mingine, moja ya sababu ikiwa ni hali mbaya ya kibiashara.

    Hata hivyo, kupungua kwa mauzo kunashuhudiwa sio jijini Nairobi pekee, wateja katika miji mingine pia wanakabiliwa na tatizo hilo, huku wateja wakionekana kukaa na pesa zao.

    Beryl Auma, anayeshona na kuuza nguo za jumla huko Kakamega, magharibi mwa Kenya anasema, hakuna biashara katika soko kwa sasa. Amepeleka nguo zake katika masoko tofauti katika siku chache zilizopita, lakini ameuza chache sana kwa sababu wamiliki wa maduka hawazinunui.

    Wachunguzi wanaona kuwa uchaguzi, hususan nchini Kenya, una kawaida ya kuleta hali ya wasiwasi ambayo inaathiri wateja, na hivyo kufanya maendeleo yoyote kuwa katika hatihati. Mhadhiri wa masuala ya uchumi jijini Nairobi Henry Wandera anasema, watu hawapendi kutumia pesa zao wakati hawana uhakika wa kesho yao. Amesema uchaguzi wa mwaka 2007 ulishuhudia vurugu na ilikuwa ni jambo jipya kwa Wakenya, ambao wengi wao mpaka sasa hawajasahau.

    Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Takwimu nchini Kenya zinaonyesha kuwa, pato halisi la ndani (GDP) limeongezeka kwa asilimia 4.7 katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikiwa ni ukuaji wa chini zaidi tangu mwaka 2013.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako