Msitu wa Saihanba wenye ukubwa wa hekta elfu 74.7 ulioko kilomita 200 kaskazini mwa mji wa Beijing nchini China, ni msitu mkubwa zaidi duniani uliopandwa na watu. Wafanyakazi wa shamba la msitu huo wametimiza muujiza wa kubadilisha jangwa kuwa msitu katika zaidi ya nusu karne iliyopita.
Kila ifikapo majira ya joto, msitu wa Saihanba unakuwa na mandhari ya kupendeza. Upepo unavuma kwenye misonobari, mimea mingi inakua kando ya mito, wadudu na ndege wanatoa milio, mambo yote hayo yamewavutia watalii wengi.
"Mazingira ya hapa ni mazuri, anga ni ya rangi ya buluu na inapendeza sana."
"Hali ya hewa ya hapa ni safi na mandhari ni nzuri. Mji wa Beijing kuna msongamano mkubwa wa watu na magari. Nimekuja ili kujipumzisha."
Taasisi ya misitu ya China imekadiriwa kuwa, msitu wa Saihanba si kama tu unasaidia kuhifadhi rasilimali ya maji na kusafisha maji, bali pia inaweza kutoa hewa ya Oxygen inayokidhi mahitaji ya watu milioni 2 katika mwaka mmoja.
Wakati watalii wanapohisi upepo wa fufutende unaopita msitu wa misonobari, ni vigumu kwao kujua jinsi msitu huo ulivyopandwa katika miaka mingi iliyopita. Mfanyakazi mstaafu wa shamba la msitu huo Bw. Zhang Baozhu anasema
"Zamani upepo wenye mchanga ulivuma hapa mara kwa mara. Katika majira ya mpukutiko, upepo ukipeperusha mchanga ulikuwa wa manjano, na katika majira ya mchipuko, upepo ukipeperusha theluji ulikuwa mweupe. Wakati upepo ulipopeperusha mchanga mwingi, ilitubidi kuwasha taa nyumbani ili tuweze kuona vizuri."
Mwaka 1962, serikali ya China ilianzisha shamba la msitu wa Saihanba. Wafanyakazi 369 ambao wastani wa umri wao ni chini ya miaka 24 walikwenda kwenye shamba hilo lenye mazingira magumu ambayo theluji inakuwepo kwa miezi 7 kila mwaka, na joto linaweza kufikia nyuzi 43 chini ya sifuri katika majira ya baridi. Jambo linalowasikitisha zaidi ni kwamba katika miaka miwili ya mwanzo, chini ya asilimia 8 ya miti walioyopanda ilistawi. Mkuu taasisi ya shamba la msitu wa Saihanba Bw. Cheng Shun anasema,
"Mwanzoni tuliagiza miti midogo kutoka nje, lakini hatukuweza kutatua suala la kukuza miti midogo. Kupanda miti inahusu mambo mengi, ikiwemo kuchimba miti midogo kutoka sehemu nyingine, kuisafirisha kwa treni, na kuipeleka milimani. Kosa lolote litasababisha miti hiyo kufa."
Kaskazini mwa msitu wa Saihanba wenye urefu wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari, ni jangwa la Hunshandake ambalo ni moja kati ya majangwa kumi makubwa nchini China, na kusini nwa msitu huo ni miji ya Beijing na Tianjin. Zamani upepo wenye mchanga uliingia Beijing kupitia eneo hilo, lakini sasa msitu huo umezuia vizuri mchanga wa jangwani kupeperushwa kusini. Takwimu zinaonesha kuwa siku zenye mchanga na vumbi angani katika majira ya mchipuko mjini Beijing zimepungua kwa asilimia 70 kuliko miaka 50 karne iliyopita. Hali ya hewa na mazingira ya msitu wa Saihanba pia imeboreshwa, sasa aina 1,757 za wanyama na mimea inaishi katika msitu huo.
Wafanyakazi wa shamba la msitu wa Saihanba wanaanza kufikiria matumizi endelevu ya rasilimali za msitu huo. Naibu mkuu wa shamba hili Bw. Chen Zhiqing anasema,
"Kanuni yetu ni kutoa kipaumbele uendelezaji wa msitu na mazingira ya kiviumbe. Rasilimali za msitu zinatakiwa kutumiwa kwa mujibu wa sayansi badala ya kufuatilia faida tu. Tunashikilia maendeleo endelevu ya msitu huo kwenye msingi wa kuhifadhi mazingira ya kiviumbe."
Kuanza mwaka 2012, shamba la msitu wa Saihanba lilianza kupunguza ukataji wa miti kwa kiasi kikubwa. Mapato kutoa mauzo ya mbao yalipungua na kufikia chini ya asilimia 50 kutoka asilimia 90 ya mapato yote. Wafanyakazi wamejitahidi kuendeleza shughuli za kukuza miti midogo, utalii na uzalishaji wa umeme kwa nguvu ya upepo, na pia wamejionea mabadiliko kwenye maisha yao. Wafanyakazi wengi wamepata nyumba mpya katika kaunti ya Weichang iliyoko karibu zaidi na msitu huo, na wengi wamenunua magari. Mfanyakazi Yang Liying anasema,
"Napapenda sana hapa, zamani nilifikiri maisha ya hapa ni magumu, lakini nilitakiwa kuishi hapa kwa sababu wazazi wangu walitaka kuishi hapa. Lakini siku hizi mazingira ya hapa ni mazuri sana, mshahara pia ni mkubwa."
Takwimu zinaonesha kuwa msitu wa Saihanba unaweza kuleta mapato ya yuan milioni 600 kila mwaka kwa maeneo yaliyoko kando ya msitu huo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |