• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maofisa wa Afrika wajadili ripoti iliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa 19 wa CPC

    (GMT+08:00) 2017-10-20 18:24:49

    Mkutano mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC unafanyika hapa Beijing. Ripoti iliyotolewa na katibu mkuu wa Kamati kuu ya chama hicho Bw. Xi Jinping ambaye pia ni rais wa China kwenye mkutano huo inafuatiliwa sana na dunia nzima zikiwemo nchi za Afrika.

    Ripoti hiyo imesema China itavumbua njia mpya za uwekezaji katika nchi za nje, ili kuhimiza ushirikiano wa uzalishaji duniani. Ofisa wa wizara ya viwanda ya Jamhuri ya Watu wa Congo Bw. Jules Nkiambi Kiese anaona kuwa, China itazisaidia nchi za Afrika kuondoa matatizo sugu ya kimaendeleo kwa kuongeza ushirikiano wa uzalishaji kati ya pande hizo mbili.

    "China imetupatia msaada wa teknolojia, na kuzisaidia nchi za Afrika kuondoa matatizo sugu ya kimaendeleo. China ina uwezo mkubwa wa fedha na teknolojia, huku tukiwa na maliasili nyingi. Kuongeza ushirikiano katika sekta ya uzalishaji kati ya China na Afrika kutazisaidia nchi za Afrika kutimiza maendeleo zaidi."

    Naibu mkurugenzi wa idara ya kuhimiza haki miliki za viwanda ya Mali Bw. Boubacar Traore pia anafurahia China na Afrika kuongeza ushirikiano wa uzalishaji, na kusema uwekezaji wa China barani Afrika utasaidia nchi za Afrika kupunguza pengo la maendeleo na nchi nyingine duniani.

    Ofisa wa wizara ya fedha ya Benin Mehdi Mama Yari anatarajia nchi yake itafanya ushirikiano katika nyanja ya uzalishaji na China katika sekta mbalimbali. Amesema China ni mwezi mzuri zaidi wa ushirikiano wa nchi za Afrika. Imeanzisha ushirikiano halisi na Benin katika sekta nyingi, na Benin inatarajia pande hizo mbili zitaongeza ushirikiano katika sekta za kilimo, teknolojia na miundombinu. Amesema pia China imepata mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini, na uzoefu wake katika shughuli hizo unastahili kuigwa na Benin.

    Ripoti hiyo pia imesema China itahimiza ushirikiano wa kimataifa wa Ukanda Mmoja na Njia Moja, na kuunganisha sera, miundombinu, biashara, fedha na maelewano ya watu kati ya pande mbalimbali, ili kujenga jukwaa jipya la ushirikiano wa kimataifa, na kuongeza injini mpya ya kuhimiza maendeleo ya pamoja.

    Ofisa wa wizara ya viwanda ya Madagascar Bw. Juducael Flavien amesema, pendekezo la China la Ukanda Mmoja na Njia Moja litaleta fursa mpya ya kujiendeleza kwa nchi za Afrika.

    "Pendekezo la China la Ukanda Mmoja na Njia Moja limeleta fursa kubwa kwa Madagascar. China ina maendeleo ya kasi. Tunatarajia kuongeza ushirikiano na China, kwani China imeleta fursa ya maendeleo kwa uchumi wetu."

    Ofisa wa wizara ya fedha ya Benin Mehdi Mama Yari amesema pendekezo hilo ni muhimu, Benin ina bandari kubwa, inatarajia kujiunga na pendekezo hilo kwa njia ya bahari.

    Naibu mkurugenzi wa idara ya kuhimiza haki miliki za viwanda ya Mali Bw. Boubacar Traore anaona kuwa pendekezo hilo linaweza kuzinufaisha nchi zote za Afrika. Anasema,

    "Pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja limefika Afrika ya Mashariki, lakini haimaanishi kuwa China italimalizia hukohuko tu, pendekezo hilo litazinufaisha nchi zote za Afrika. Tunakaribisha miradi ya maendeleo kwenye pendekezo hilo. Tuna malighafi na rasilimali, lakini hatuna uwezo wa kutosha katika sekta ya viwanda. China ina uwezo huo, pia ni hodari katika ujenzi wa miundombinu."

    Ripoti hiyo pia imetaja kuongeza misaada kwa nchi zinazoendelea hasa zile zilizopo nyuma zaidi kimaendeleo, ili kupunguza pengo kati ya nchi za kusini na za kaskazini. Maofisa wa nchi za Afrika wamesema, ni tofauti na nchi za magharibi, China haiweki sharti lolote kwenye misaada yake kwa nchi za Afrika. Misaada ya China inaweza kuzinufaisha zaidi nchi za Afrika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako