• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Idadi ya wahamaji yapungua nchini China kwa miaka miwili mfululizo

    (GMT+08:00) 2017-11-13 17:41:24

    Kamati ya afya na uzazi kwa mpango ya China hivi karibuni ilitoa ripoti ya mwaka 2017 kuhusu hali ya wahamaji nchini China, ikionesha kuwa mwaka 2016, idadi ya wahamaji nchini China ilikuwa milioni 245, na kupungua kwa watu milioni 1.71 ikilinganishwa na mwaka 2015. Idadi hiyo imepungua kwa miaka miwili mfululizo, wakati huohuo idadi ya wahamaji waliozaliwa baada ya miaka ya 80 ya karne iliyopita imeongezeka na kuchukua nafasi ya kwanza ikilinganishwa na wahamaji wa umri mwingine.

    Mkurugenzi wa ofisi ya kutoa huduma za uzazi kwa mpango kwa wahamaji ya kamati ya afya na uzazi kwa mpango ya taifa la China Bw. Wang Qian amesema, mwelekeo wa jumla wa hali ya uhamaji nchini China kwa mwaka 2016 unafanana na wa miaka iliyopita, na watu wanaendelea kuhamia miji mikubwa, haswa ile iliyo karibu na pwani, mito mikubwa na reli. Lakini idadi ya wahamaji inapungua. Anasema,

    "Baada ya kufanya uchambuzi, tumetambua kuwa kupungua kwa idadi ya wahamaji kunatokana na athari ya sera na hatua zilizotekelezwa katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mfano China inahimiza mageuzi ya sera ya uandikishaji wa makazi, na kupanga kuhamasisha wakulima milioni 100 kuwa wakazi rasmi wa miji. Pia imetoa sera ya kuunga mkono wakulima wanaofanya vibarua mijini kurudi kwao kuanzisha shughuli. Aidha, baadhi ya miji imeweka lengo la kudhibiti ongezeko la wakazi."

    Wakati huo huo, idadi ya wahamaji waliozaliwa baada ya miaka ya 80 inaongezeka, na kuchukua asilimia 56.5 ya wahamaji wote hadi kufikia mwaka 2016. Profesa Duan Chengrong wa Chuo Kikuu cha Umma cha China anayetafiti elimu za jamii na idadi ya watu anasema,

    "Tunawaita vijana waliozaliwa baada ya miaka ya 80 kuwa kizazi kipya. Asilimia ya kizazi kipya katika wahamaji wote inaongezeka kwa mfululizo. Hii ni hali ya kawaida, kwani vijana wanahamia mijini. Hali hiyo italeta athari gani? Kwa jumla ongezeko la wahamaji hao vijana wenye elimu zaidi litasahihisha maoni kwamba wakulima wanaofanya kazi vibarua mijini hawana elimu, na pia litahimiza maendeleo ya uchumi na taifa."

    Aidha ripoti hiyo pia inaonesha kuwa katika miaka ya hivi karibuni wahamaji wengi wanahamia mijini pamoja na familia zao, na hali ambayo imesababisha mahitaji mengi zaidi ya huduma za jamii, ikiwemo uzazi, matibabu, elimu na matunzo ya wazee. Bw. Duan Chengrong anasema,

    "Wahamaji hao wana matarajio makubwa zaidi kwa maisha yao mijini. Wana uwezo wa kuchagua kazi inayowapatia kipato zaidi, na kutaka watoto wao wapate elimu na nafasi kubwa zaidi ya kujiendeleza. Hali hii inaitaka jamii haswa miji, iwapatie wahamaji hao wa kizazi kipya mazingira na nafasi nzuri zaidi."

    Bw. Wang Qian amesema, China itasukuma mbele usawa wa huduma za kimsingi za kijamii kwa watu wote, na kuwapa wahamaji huduma za afya na uzazi kama wakazi rasmi wa miji.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako