• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaendelea kuchukua hatua za kuhifadhi maji

    (GMT+08:00) 2017-11-29 18:29:37

    Kuanzia mwezi ujao, China itaongeza sehemu za kufanya majaribio ya mageuzi ya kodi ya maji, kwa kulenga kupunguza matumizi ya maji ya kupita kiasi, ili kuhifadhi maliasili ya maji.

    China ilianza kufanya majaribio ya mageuzi ya kodi ya maji mwezi Julai, mwaka jana mkoani Hebei, kwa kutoza kodi ya maji badala ya ada ya maji. Wastani wa umiliki wa maliasili ya maji kwa mtu mkoani humo ni moja ya saba ya wastani wa China, ambapo matumizi ya maji yanayopatikana chini ya ardhi yanachukua moja ya tatu ya matumizi ya maji hayo yote nchini China. Hali hii imesababisha matatizo ya kupungua kwa maji chini ya ardhi kwa kasi, kushuka kwa ardhi na hata kutokea kwa mipasuko, na ni changamoto kubwa inayokabili juhudi za kuhifadhi mazingira na kupata maendeleo endelevu. Naibu mkuu wa idara ya fedha ya serikali ya mkoa wa Hebei Bw. Li Jiegang amesema, mkoa huo umeweka vigezo vya ushuru wa maji kwa kufuata kanuni ya kuhamasisha kutumia maji kwa marudio, kutumia maji ya ardhini kwa njia mwafaka, na kuzuia kutumia maji chini ya ardhi kupita kiasi. Anasema,

    "kodi ya maji ya chini ya ardhi haswa katika mahali ambapo maji yamechukuliwa kupita kiasi, ni kubwa kuliko kodi ya maji juu ya ardhi. Sekta maalumu za viwanda na kibiashara zitatozwa kodi zaidi inayoweza kufikia mara 40 kuliko ya zamani, huku kodi kwa sekta za kilimo ikiwa nafuu."

    Baada ya utekelezaji wa mageuzi hayo kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, matumizi ya maji chini ya ardhi mkoani Hebei yamepungua. Mageuzi hayo pia yamefanikiwa kuzihimiza kampuni zinazotumia maji mengi kubana matumizi ya maji na njia ya kuyatumia. Kuanzia tarehe mosi, Disemba mwaka huu, China itaongeza sehemu za kufanya majaribio ya mageuzi hayo. Sehemu hizo haswa ni kaskazini mwa China ambapo kuna pengo kubwa kati ya mahitaji na maliasili ya maji, pamoja na sehemu nyingine zinazopenda kufanya majaribio hayo. Mkuu wa idara inayoshughulikia mambo ya ushuru ya wizara ya fedha ya China Bw. Wang Jianfan amesema,

    "Kuongeza sehemu za kufanya majaribio ya mageuzi ya kodi ya maji kutaisaidia China kupunguza ufujaji wa maji, na kuhifadhi maliasili hii muhimu kwa njia ya kodi, pia kutatoa uzoefu na kuweka msingi mzuri kwa ajili ya utekelezaji wa kodi hiyo kote nchini China, na kusaidia kukamilisha mfumo wa kodi ya maji."

    Bw. Wang amesema lengo la mageuzi hayo ni kuzuia ufujaji wa maji na matumizi ya maji chini ya ardhi kupita kiasi, ili kurekebisha na kuboresha muundo wa matumizi ya maji, na hayataongeza mzigo kwa raia na kampuni za kawaida.

    Wastani wa maliasili ya maji nchini China kwa mwaka ni mita trilioni 2.8 za ujazo. Lakini wastani kwa mtu ni asilimia 28 ya wastani wa dunia. Mkuu wa taasisi ya sayansi ya mambo ya fedha ya China Bw. Liu Shangxi amesema, kuongeza sehemu za kufanya majaribio ya mageuzi ya ushuru wa maji ni hatua iliyochukuliwa na China kwa ajili ya kukabiliana upungufu wa maji. Anasema,

    "Nchi yetu inakabiliwa na upungufu wa maliasili ya maji. Tuna haja ya kuchukua hatua halisi ya kuwahamasisha watu wawe na mawazo ya kubana matumizi ya maji, na kurekebisha njia ya matumizi hayo. Hii pia ni hatua yetu ya kuhimiza ujenzi wa ustaarabu wa mazingira, na jamii inayobana matumizi ya maliasili."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako