• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yatarajia kutimiza malengo ya kupunguza uchafuzi wa hewa

    (GMT+08:00) 2017-12-11 18:11:11

    Mkutano wa mwaka 2017 wa kamati ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya China umefanyika hivi karibuni hapa Beijing, China. Waziri wa uhifadhi wa mazingira wa China Bw. Li Ganjie ameeleza kuwa, huu ni mwaka wa mwisho wa mpango wa kushughulikia uchafuzi wa hewa wa China, na malengo matano ya mpango huo yote yanatarajiwa kutimizwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

    Kwenye kikao cha wajumbe wote wa mkutano wa mwaka 2017 wa kamati ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya China, naibu mkurugenzi mtendaji wa kamati hiyo, ambaye pia ni waziri wa uhifadhi wa mazingira wa China Bw. Li Ganjie amesema, kutokana na juhudi kubwa za China katika kujenga ustaarabu wa viumbe na mazingira katika miaka ya hivi karibuni, hali ya uwiano wa viumbe na mazingira imeboreshwa kidhahiri. Anasema,

    "Mwaka 2016, wastani wa kiwango cha uchafuzi wa vumbi aina ya PM10 katika miji 338 nchini China kilipungua kwa asilimia 15.5 ikilinganishwa na mwaka 2013, huku kiwango cha uchafuzi wa vumbi aina ya PM2.5 katika sehemu tatu zilizoendelea zaidi kikipungua zaidi ya asilimia 30, na kiwango hicho cha Beijing kupungua kwa asilimia 18. Asilimia ya maeneo yaliyokumbwa na mvua ya asidi kwa maeneo yote ya China ilipungua na kuwa 7.2 kutoka 30. Wakati huo huo, uchafuzi wa maji pia umepungua kwa kiasi kikubwa."

    Huu ni mwaka wa mwisho wa mpango wa kushughulikia uchafuzi wa hewa wa China. Bw. Li amesema katika miaka mitano iliyopita, njia maalumu ya China katika kushuhulikia uhifadhi wa viumbe na mazingira imekamilika, China imepata ufanisi mkubwa katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira, na malengo matano ya mpango wa kushughulikia uchafuzi wa hewa wa China yanatarajiwa kutimizwa kikamilifu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Anasema,

    "Kuna malengo matano. La kwanza ni kupunguza kiwango cha uchafuzi wa vumbi aina ya PM10 katika miji 338 mikubwa nchini China kwa asilimia zaidi ya 10, na tumepunguza kiwango hicho kwa asilimia 20.4 hadi kufikia mwishoni mwa Novemba. Lengo la pili ni kupunguza kiwango cha uchafuzi wa vumbi aina ya PM2.5 katika maeneo ya Beijing, Tianjin na Hebei kwa asilimia 25, na hadi sasa tumekipunguza kwa asilimia 38.2. Lengo la tatu na nne ni kupunguza kiwango hicho katika maeneo yaliyoko sehmu ya kati na chini ya bonde la mto Changjiang, na maeneo ya kusini na kati ya mkoa wa Guangdong kwa asilimia 20 na 15, na tumepunguza kwa asilimia 31.7 na 25.6. Lengo la mwisho ni kupunguza wastani wa kiwango cha vumbi aina ya PM2.5 mjini Beijing chini ya mikrogramu 60 kwa mita moja ya ujazo, na inaonekana litatimizwa kwa mafanikio."

    Mafanikio yaliyopatikana nchini China katika kuhifadhi mazingira yamepongezwa na jumuiya ya kimataifa. Naibu mwenyekiti wa kamati ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya China Bw. Erik Solheim, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mipango ya Mazingira la Umoja wa Mataifa amesema, katika miaka ya hivi karibuni, China imerekebisha ufuatiliaji wake kutoka maendeleo ya uchumi peke yake, hadi uwiano wa maendeleo ya uchumi na uhifadhi wa mazingira. Katika siku zijazo, China itatoa mchango muhimu zaidi katika juhudi za kuboresha mazingira ya kimataifa. Anasema,

    "China imeweka ujenzi wa ustaarabu wa viumbe na mazingira kwenye mpango wake wa miaka mitano ijayo. Tunaweza kukadiria kuwa China itatoa uvumbuzi katika utafiti na matumizi ya teknolojia za kuhifadhi mazingira. Hali hii si kama tu itaimarisha ushirikiano husika wa kimataifa, bali pia itanufaisha dunia nzima kwa kusaidia kupunguza gharama za bidhaa na huduma za kuhifadhi mazingira. Mbali na hayo, China pia imechangia sana katika uhifadhi wa anuai ya viumbe duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kuhifadhi anuai ya viumbe nchini humo, China pia inaimarisha usimamizi wake kwa soko, na kupunguza biashara haramu za pembe za ndovu. Mkutano wa 15 wa nchi zilizosaini makubaliano ya anuai ya viumbe utafanyika mjini Beijing mwaka 2020. Natarajia mkutano huo utafanyika kwa mafanikio, na kupata matokeo mazuri."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako