• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China yafadhili miradi mingi ya maendeleo Zanzibar

  (GMT+08:00) 2018-02-12 10:39:12

  Miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na China visiwani Zanzibar inatarajiwa kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi itakapokamilika.

  Baadhi ya miradi ambayo inafadhiliwa na China visiwani Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume,uwanja wa Michezo wa Mao,miundombinu ya barabara,nyumba miongoni mwa miradi mengine.

  Mwanahabari wetu Khamis Darwesh ametembea visiwani Zanzibar na kutuandalia ripoti ifuatayo.

  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga hatua kubwa za kimaendeleo.Hapa katika visiwa vya Zanzibar kuna miradi mbalimbali mikubwa inayoendelea,ambayo inafadhiliwa na China.

  Ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume mjini Zanzibar chini ya ufadhili wa serikali ya watu wa China ni mojawapo ya miradi mikubwa inayoendelezwa hapa.

  Ujenzi huu utakaogharimu dola $128.7 unafadhiliwa na Benki ya Exim ya China.

  Jengo hilo jipya litakapokamilika litawezesha uwanja huo kushughulikia ndege kubwa na kufanikisha uchukuaji na ushushaji wa shehena na pia kuongeza idadi ya abiria ,haswa watalii wanaozuru visiwa vya Zanzibar.

  Mbali na mradi huu kuna miradi kama ya ujenzi wa uwanja wa michezo,taa za barabarani,mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mpigadori,nyumba,mashule na miradi mengine mengi.

  Mkurugenzi wa Manispaa ya mjini Zanzibar Aboud Hassan Serenge wiki iliyopita alitia saini na balozi mdogo wa China visiwani Zanzibar juu ya mradi wa taa za barabarani.

  "Huu mradi ni awamu ya pili ya taa za barabarani.Mradi wa mwanzo ni ule ambao tuna taa za barabarani tunaita Four Ways kutoka Darajani kuelekea Kariakoo,na kutoka Mlandege kuelekea Maisara.Wachina walitusaidia hizi taa za barabarani,wachina walitufanzia mabadiliko ya zile taa na sasa zinafanya vizuri"

  Aidha Serenge ametoa wito kwa wananchi na madereva kushirikiana na serikali katika kutoa taarifa za uharibifu wa taa hizo.

  "Baadhi ya taa zinagongwa sana,zile taa zina gharama kubwa.Kwanza wito kwa wananchi na wale waendesha magari kwamba watahadhari sana juu ya hizi taa na pili wananchi tushirikiane na serikali wale ambao tumewabaini taa hizi wameziharibu basi walete ripoti tuwajue ni kina nani na hatua za kisheria zichukuliwe ili kudhibiti hiyo hali"

  Mkurugenzi huyo anasema kuwa mradi huo utakapoanza utaimarsiha na kuweka vizuri haiba ya mji wa Zanzibar,na pia kutoa ajira kwa watu wa tabaka mbalimbali.

  Naibu Mkurugenzi Idara ya Habari maelezo,Zanzibar,Dr Juma Muhammad Salum anaeleza kuhusu baadhi ya miradi inayofadhiliwa na China visiwani Zanzibar pamoja na Tanzania bara.

  Sauti Dkt Juma Salum

  Aidha Dkt Juma anasema ziara ya Rais wa China nchini Tanzania mwaka 2014 imeleta mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi mingi inayoendelea.

  "Ziara ya Mheshimiwa Rais wa China Xi Jinping mwaka 2014 imeleta mafaniko makubwa sana ya utekelezaji wa miradi hii ambayo sasa ujenzi wake unaendelea hasa katika miundombinu ya barabara kwa upande wa Tanzania bara kwa sehemu kubwa sana imekuwa ikifadhiliwa na serikali ya China"

  Balozi mpya wa China nchini Tanzania Wang Ke alipomtembelea Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein alisema ataendeleza ushirikiano mwema baina ya Zanzibar na China.

  Balozi Wang Ke alisema China itaendelea kuisaidia na kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake.

  "Tuna jukumu moja la kuendeleza nchi zetu,tunaweza kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa ila mmoja,tukasaidiana,na pia kuna fursa nyingi sana ambazo tunaweza kufanya kwa pamoja na kuzinufaisha nchi na watu kutoka pande zote.Mimi kama balozi nahisi nina jukumu kubwa,nitajaribu kadri niwezavyo kuimarisha mahusiano yetu baina ya nchi zetu mbili"

  Wakati huo huo,Balozi Wang Ke aliihakikishia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa mara baada ya kumalizika kwa miradi ambayo inaendelea,serikali ya China itakuwa tayari kuunga mkono katika kuanzisha miradi mipya mikubwa Zanzibar kwa siku za usoni ,na pia kuleta wawekezaji kwa ajili kujenga viwanda vinayotokana na rasilimali za bahari kwa lengo la kukuza sekta ya uvuvi na sekta ya viwanda.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako