• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mradi wa kawi Garissa unaofadhiliwa na China kuwanufaisha wakazi wa Kenya

    (GMT+08:00) 2018-02-19 16:38:21

    Huku kukiwa na makampuni zaidi ya 50 kutoka China yanayoshughulika na miradi mbalimbali ya miundombinu nchini Kenya, wadadisi wanasema China imekuwa mwenzi wa kuaminika katika masuala ya miundombinu na maendeleo wa Kenya.

    Uwekezaji wa China nchini Kenya umeongezeka mwaka hadi mwaka hadi katika nyanda za biashara,barabara,uzalishaji nishati,uchukuzi wa majini,reli pamoja na ujenzi wa nyumba.

    Miongoni mwa miradi mikubwa inayofadhiliwa na kutekelezwa na China ni mradi wa nishati ya jua mjini Garissa,kaskazini mashariki mwa Kenya.Hiki ni kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme wa jua katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

    Mradi huu umegharimu Sh13 bilioni ($116milioni).

    Mjenzi wa mradi huu ni kampuni ya China Jiangxi Corporation for International Economic and Technical Company Limited (CJIC).

    Mwanahabari wetu Ahmed Bahajj anaripoti

    Niko mjini Garissa.Niko katika kiwanda kikubwa cha uzalishaji nishati ya jua,mradi unaotekelezwa na kampuni ya China ya China Jiangxi Corporation for International Economic and Technical Company Limited (CJIC).

    Ujenzi wa mradi huu unaendelea vizuri na umepiga hatua si haba.

    Mradi huu ulio katika ardhi ya ekari 200 unatarajiwa kuimarisha maendeleo katika eneo ambalo limeathirika pakubwa na mashambulizi ya kigaidi.Mradi huu utazalisha megawati 50 za umeme utapunguza uzalishaji wa kaboni kwa tani 64,190 kwa mwaka.

    Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya usambazaji umeme vijijini nchini Kenya (REA) Bw Peter Mbugua anasema mradi huu usioharibu mazingira utaleta manufaa mengi nchini Kenya.

    "Huu ni mradi wa nishati mbadala ambao utategemea rasilimali zetu za kitaifa na una manufaa mengi ya kifedha na kiuchumi kwa nchi ya Kenya wakati tutakapoanza kuweka umeme huo katika gridi ya taifa"

    Kwa upande wake mwenyekiti wa Mamlaka ya usambazaji umeme vijijini (REA) Simon Gicharu anasema mradi huu mbali na kuzalisha umeme utasaidia pakubwa katika kuhifadhi mazingira

    "Nafahamishwa kuwa mradi huu utatumia paneli 200 za megawati 250 na zitazalisha megawati 76,473 za umeme kwa mwaka na pia kupunguza uzalishaji wa kaboni kwa tani 43,000"

    Gicharu anasema umeme utakaozalishwa na kiwanda hicho utaweza kukidhi mahitaji ya watu wa Garissa.

    "Umeme utakaozalishwa katika kiwanda hiki utatosha kusambazwa kwa nyumba 625,000.pia umeme utakaozalishwa katika kiwanda hicho utatosha kusambazwa kwa shuke zote msingi Garissa.Huu ni mradi ambao serikali ya Jubilee unafanya kuhakikisha kwamba shule zote zina umeme"

    Waziri wa Nishati na Petroli nchini Kenya Charles Keter anasema mradi huu utabadilisha kwa kiasi kikubwa uchumi na maendeleo katika kaunti ya Garissa.

    "Mradi wa nishati ya jua wa megawati 50 mjini Garissa ni mradi wa kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu.Ningependa kuishukuru serikali ya China kwa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 13.Ajira katika nishati zisizoharibu mazingira kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya zitafikia 2000 hadi 3000.Kutakuwa na fursa za ajira.Mradi huu utapunguza uzalishaji wa kaboni.Mradi huu kwa ujumla utaleta mambo mazuri"

    Balozi wa China nchini Kenya Liu Xianfa anasema mradi huu unafadhiliwa na Benki ya China Import Export Bank na utakuwa mradi mkubwa sana barani Afrika.

    "Benki ya China Import Export Bank inafadhili mradi huu kwa kutoa mkopo usio na masharti,na mradi huu utakuwa mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya umeme wa jua barani Afrika"

    Mradi huu unalenga kuimarisha maendeleo katika kaunti ya Garissa na kutoa nafasi za kazi zitakazosaidia kupunguza umaskini na kuzuia vijana kujihusisha na ugaidi.

    Baada ya kaunti ya Garissa kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyopelekea vifo vya watu 148, China iliwahi kutuma msaada wa fedha wa dola 67,000 kwa ajili ya familia za waathirika.

    Umeme kutokana na mradi huo utakaotoa ajira zaidi ya Elfu Moja unatarajiwa kuunganishwa kwenye gridi ya taifa ndani ya mwaka mmoja.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako