Katika miaka ya hivi karibuni, China imefanya juhudi kubwa katika kuhifadhi mazingira, na hali ya uchafuzi wa mazingira katika sehemu mbalimbali nchini China imepungua. Wataalamu wanasema, mawazo ya kuendeleza uchumi bila ya kuchafua mazingira yamekubaliwa na watu wote, na hatua ijayo ya China ni kujenga utaratibu wa muda mrefu katika uhifadhi wa mazingira.
Bw. Rao Min mwenye umri wa miaka 31 anaishi katika makazi yaliyoko karibu na Mto Changjiang mjini Luzhou mkoani Sichuan. Amesema katika miaka miwili iliyopita, mazingira ya makazi yake yameboreshwa sana. Anasema,
"Zamani kulikuwa na takataka nyingi kwenye makazi yetu, palikuwa pachafu sana. Lakini sasa hali imebadilika, makazi yetu yanaonekana kama bustani. Hata sisi wakazi wote tumekuwa na mawazo ya kuhifadhi mazingira."
Maboresho ya mazingira katika maeneo ya makazi mjini Luzhou yanatokana na harakati ya kusafisha maji na mazingira ya Mto Changjiang iliyoanzishwa na serikali ya mji huo miaka miwili iliyopita, kwa kutenga zaidi ya (dola za kimarekani) fedha za reminbi yuan zaidi ya milioni 17.
Wakati huo huo, mji wa Yichang mkoani Hubei ambao pia uko karibu na Mto Changjiang umefanya marekebisho katika sekta za viwanda ili kuboresha mazingira ya mto huo. Mwaka jana, mji huo ulifunga viwanda 25 vya kemikali vilivyokuwa kando ya Mto Changjiang, na utashughulikia viwanda vingine 134 vya kemikali katika miaka mitatu ijayo. Hadi kufikia mwaka 2020, viwanda vyote vya kemikali vitaondolewa kutoka kando ya mto huo.
Naibu meya wa mji wa Yichang Bw. Yuan Weidong amesema, mji huo umepanga kujenga eneo la viwanda vya kikemikali vya hali ya juu, ambavyo havitaleta uchafuzi wa mazingira. Anasema,
"Tutaendeleza viwanda vya kemikali vya hali ya juu, kama vile malighafi mpya za teknolojia za juu, dawa, vifaa vya kuhifadhi mazingira."
Uchafuzi wa hewa unachukuliwa kama uchafuzi sugu zaidi. China pia imepiga hatua kubwa katika kushughulikia uchafuzi wa aina hiyo. Takwimu zilizotolewa na wizara ya uhifadhi wa mazingira ya China zinaonesha kuwa, mwaka jana kiwango cha uchafuzi wa vumbi aina ya PM2.5 katika sehemu za Beijing, Tianjin na Hebei kilipungua kwa asilimia 9.9. Mtaalamu mkuu wa uchumi wa Kituo cha Mawasiliano ya Uchumi wa Kimataifa cha China Bw. Xu Hongcai anasema,
"Tunapaswa kufuata vigezo vya ngazi ya juu kwa hiari, na kuhimiza maendeleo ya teknolojia, ili kurekebisha sekta za jadi za uchumi."
Wataalamu wanaona kuwa baada ya mawazo ya uhifadhi wa mazingira kukubaliwa na watu wote, China inapaswa kujenga utaratibu wa muda mrefu katika uhifadhi wa mazingira.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |