Mkutano wa kwanza wa Baraza la 13 la Mashauriano ya Kisiasa la China umefunguliwa hapa Beijing, masuala ya maisha ya umma kama vile kukabiliana na hali ya jamii yenye idadi kubwa ya wazee, elimu na afya ya kisaikolojia ya watoto wanaoachwa nyumbani na kuboresha hali ya matibabu katika maeneo ya makabila madogomadogo yanafuatiliwa zaidi na wajumbe. Mama Chen ana maelezo zaidi.
Ongezeko la idadi ya wazee katika jamii imekuwa changamoto kubwa inayoikabili China, utunzaji wa wazee ni masuala muhimu na changamoto zinazozikabili familia na jamii. Kujenga mfumo wa huduma za kutunza wazee katika jamii unaoendana na hali halisi ya China ni njia pekee ya kutatua suala hilo. Mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la mkoa wa Guangxi Bw. Qian Xueming amesema, mfumo wa huduma za kutunza wazee unatakiwa kuwa na utandawazi wa hospitali na nyumba za utunzaji wa wazee, na mashirika ya kuwatunza wazee, kuwatunza wazee kwenye maeneo ya makazi na kuwatunza wazee nyumbani. Bw. Qian anasema, "Tunatakiwa kuwa na mashirika makubwa ya kuunganisha matibabu na utunzaji wa wazee, na matawi ya mashirika hayo yataingia katika maeneo ya makazi na kuanzisha huduma za kuwatunza wazee kwenye maeneo ya makazi. Huduma ya matibabu na utunzaji wa wazee inatakiwa kuingia katika familia ili kusaidia kutimiza kuwatunza wazee nyumbani. Pande hizo tatu zitakuwa mfumo mmoja ili kuufanya ufanisi wa huduma za kuwatunza wazee uwe juu zaidi."
Watoto wanaoachwa nyumbani vijijini kwa sababu wazazi wao wanafanya kazi mijini ni hali ya jamii isiyoweza kuepukika na kuwepo kwa muda mrefu katika mchakato wa mabadiliko ya njia ya kuendeleza uchumi na mabadiliko ya mtindo wa maisha ya jamii. Kutatua suala la elimu ya watoto wanaoachwa nyumbani vijijini itakuwa kazi ngumu ya muda mrefu. Mjumbe wa baraza hilo ambaye pia ni naibu meya wa mji wa Weinan mkoani Shaanxi Bibi Gao Jie anaona kuwa nguvu ya serikali za mitaa, idara za elimu na jamii zinahitajika katika utatuzi wa suala hilo. Anasema,
"Tunatakiwa kujenga vituo vya kutoa huduma za afya ya kisaikolojia kwa watoto wanaoachwa nyumbani, ili kuwapa upendo katika mchakato huo. Kwa mfano tunaweza kujenga mfumo wa simu za mezani, ili watoto waweze kuwasiliana na wazazi wao kwa wakati, au kujenga jukwaa la waalimu wastaafu, ambao pia wanaweza kuwasaidia watoto hao. Tunaweza kuwashirikisha watoto hao kwenye shughuli mbalimbali, ili kuwasaidia watoto hao kuimarisha uwezo wa kujiamini, uwezo wa kushirikiana, uwezo wa kukabiliana na matatizo na uwezo wa kuwa karibu na watu wengine."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |