Rais Xi Jinping wa China jana alishiriki kwenye majadiliano na wajumbe kutoka mkoa wa Shandong kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge la 13 la Umma la China unaoendelea hapa Beijing. Amesema mkakati wa kuendeleza vijiji ni ajenda kuu ya kazi za serikali katika sekta ya kilimo, maeneo ya vijijini na wakulima, na serikali za mitaa zinatakiwa kutambua vya kutosha umuhimu na ulazima wake na kuutekeleza kwa makini. Wajumbe mbalimbali wametoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kutekeleza mkakati huo wa kuendeleza vijiji.
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China Bibi Yu Liufang ni katibu mkuu wa kamati ya Chama cha Kikomunisti cha China ya kijiji cha Yanbo, mkoani Guizhou. Katika miaka kumi iliyopita tangu ashike wadhifa huo, amefanya pato la kijiji hicho kwa mtu mmoja mmoja kuongezeka kutoka Yuan 800 hadi Yuan 5,600, na thamani ya mali za pamoja kufikia Yuan milioni 8. Safari hii, amewasilisha mapendekezo sita kwenye mkutano wa kwanza wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China. Anasema, "Mali za pamoja za kijiji ni muhimu katika kutekeleza mkakati wa kuendeleza vijiji. Katika mkoa wa Guizhou ninakoishi, vijiji vingi vimekuwa na mali, lakini bado kuna vichache ambavyo havina. Naona serikali inapaswa kutangaza sera, kama vile kutoa mkopo, kukusanya fedha na kutoa miradi na kufanya kila kijiji kianzishe sekta yake, kiwe na umaalumu na nguvu bora.
Mjumbe mwingine Liu Yonghao amesema kuendeleza vijiji sio tu kunahusu kujenga vijiji viwe sehemu nzuri, cha muhimu zaidi ni kukuza kilimo cha kisasa. Hii inahitaji kuandaa vijana wengi bora na kuwawezesha wawe na mashamba ya aina mpya na wakulima wapya.
"Watu wazima na vijana wameondoka vijijini, na kwenda mijini kufanya kazi za vibarua, na wanaobaki ni wazee na watoto. Jambo hilo halisaidii kuhimiza maendeleo ya kilimo cha kisasa. Ndiyo maana tunapaswa kuandaa wakulima wapya, wenye teknolojia ya kilimo, kazi ambayo inahitaji msaada wa serikali, yaani kutunga sera za kuhamasisha, na kama unafanya shughuli za kilimo katika sehemu za vijijini, serikali inaweza kutoa ruzuku na kutoa unafuu wa kodi. Pia ni muhimu kuwafanya watu wanaorudi vijijini waone fahari."
Sifa ya jamii yenye maisha bora na usoshalisti wa kisasa vinaamuliwa na ushindani wa kilimo, mazingira ya vijiji na mapato ya vijiji. Hayo yamesemwa na rais Xi Jinping wa China ambaye pia ni katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha China CPC na mwenyekiti wa kamati Kuu ya Kijeshi. Amezihimiza serikali za mitaa kuzipa nguvu za uhai sekta za vijiji, kuongeza mapato ya wakazi wa vijijini, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wanavijiji.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |