• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Wadau wa Sekta ya Utalii Afrika Mashariki waipongeza China kwa kuanzisha Wizara ya Utalii na Utamadumi

  (GMT+08:00) 2018-04-19 15:38:13

  Wadau wa Sekta ya Utalii kutoka nchi za Afrika Mashariki wameipongeza Serikali ya China kwa kuanzisha Wizara mpya ya Utalii na Utamaduni, ambayo wamesema itakuwa kiungo muhimu katika kuimarisha shughuli za kuzitumia rasilimali za utalii zilizopo na kujiongezea kipato kwa pande zote mbili washirika.

  Samweli Abikunda ni Mwambata wa Biashara na Utalii katika ubalozi wa Rwanda nchini China, yeye alitoa pongezi zake mjini Beijing wakati wa maonyesho ya kimataifa ya Utalii ambapo amesema, kwa kuwa Wizara ndiyo serikali hivyo wigo wa mawasiliano yanayolenga zaidi utalii yataimarika.

  Samweli Abikunda – Afisa Utalii na Biashara Rwanda

  "Ndiyo nafikiri kuwa na Wizara ya Utalii na Utamaduni ni muhimu sana kwa sababu hata kama kwa mfano makampuni binafsi ya utalii ya China na Rwanda yangefanya kazi vizuri, bado umuhimu wa ushirikiano baina ya serikali na serikali ni muhimu, hivyo kwa sasa Bodi ya Utalii ya Rwanda ama hata sisi ubalozi tuna Wizara ambayo tutafanya nayo kazi za Utalii."

  Mwingine aliyetoa maoni yake kuhusu kuanzishwa kwa wizara hiyo ni Wakala wa watalii kutoka Tanzania, Peter Larocque ambapo yeye amesema Wizara hiyo sasa itasaidia kuunganisha wizara na sekta ya utalii ndani ya taifa la China na nchi zingine na zaidi itakuza pato na kuimarisha uchumi.

  Peter Larocque – Wakala wa Utalii Tanzania

  "Nina matumaini kuwa Wizara ya utalii ya Tanzania sasa, tashrikiana na wizara ya utalii ya China, nikiamini kuwa hii itasaidia makampuni mengi hapa China na Tanzania ili kufanya ushirikiano kwa kuleta watu wa China nchini Tanzania lakini vile vile watanzania kuja China ili kufanya biashara, tena si katika utalii tu, bali pia katika Nyanja zingine za kiuchumi."

  Katika maonyesho hayo ya sekta ya utalii yanayolenga kuwatangazia na kuwaalika watalii wa China na makampuni ya utalii ya China kwenye rasilimali za utalii zilizopo kwenye pande mbalimbali duniani, zaidi ya nchi mia moja zimeshiriki.

  Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ilizungumza na baadhi ya washiriki ili kujua maoni yao baada ya kukutana na wadau wao ambao ni makampuni ya utalii ya China pamoja na watu wa China wanaotaka kwenda kutalii katika nchi zao, wakiwemo Hassan Vuai ambaye ni Afisa Mipango wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Yves Nzengi ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii ya Rwanda pamoja na Peter Makuta ambaye ni Afisa Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Tanzania.

  Hamisi Vuai – Afisa Mipango wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar

  "Na pia wanapendelea zaidi kuzungumza lugha yao kuliko lugha nyingine, hivyo wanapenda zaidi wawe na muongoza watalii anayejua lugha ya kichina, kwa hiyo hii ni fursa kwa nchi kuwekeza katika masuala ya lugha kuwafundisha vijana ili waweze kuwaongoza watalii hawa wa aina ya kichina, ili kulipata soko hili."

  Yves Nzengi – Mkurugenzi wa Masoko Bodi ya Maendeleo ya Utalii Rwanda

  "Hivyo kwetu hii ni fursa, tumejadili biashara na tumeona wengi ambao wanahitaji kutembelea Rwanda, jambo ambalo tunaamini kuwa litaongeza idadi ya watu wanaotoka China kuja Rwanda, japo hatuwezi kuyaona matokeo yake ndani ya mwezi mmoja, lakini itakuwa baada ya muda fulani na kutokana na kujitangaza zaidi."

  Peter Makuta – Afisa Utalii Hifadhi ya taifa ya Ngorongoro Tanzania

  "Nilichojifunza ni kwamba soko hili la China lina manufaa, na niwaambie vijana wengi wa kitanzania ambao wanasoma hapa China kwamba tunawahitaji kwa kuwa watakapokuja watalii wengi kutahitajika wahudumu wengi wanaojua lugha, kwa hiyo nitoe wito kwa watanzania wenzangu kwamba tuboreshe miundo mbinu na elimu ili wageni wanaokuja tuwahudumie."

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako