• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mkuu wa jumba la makumbusho la taifa la Kenya: Jumba la Makumbusho ni chombo cha kuhifadhi, kurithisha na kuunganisha kumbukumbu

  (GMT+08:00) 2018-05-18 15:52:11

  Jumba la makumbusho la taifa la Kenya lililoko kaskazini magharibi mwa Nairobi, ni jumba lenye idadi kubwa zaidi ya vitu vya kale, na lenye historia ndefu zaidi katika eneo la Afrika Mashariki. Leo ni maadhimisho ya 42 ya siku ya kimataifa ya majumba ya makumbusho, mwandishi wetu Masika Yang amefanya mahojiano na mkuu wa jumba hilo Bw. Mzalendo Kibunja.

  Hivi sasa jumba la makumbusho la taifa la Kenya linahifadhi vitu zaidi ya elfu moja vya kale, likiwa na maeneo 12 ya maonesho yanayohusiana na binadamu, ndege, chimbuko la viumbe wa baharini, mabadiliko ya kijiolojia na historia, utamaduni na sanaa ya Kenya. Mkuu wa jumba la makumbusho la taifa la Kenya Bw. Mzalendo Kibunja amesema, jumba la makumbusho linahifadhi kumbukumbu na kuwa na umuhimu katika kuimarisha utambuzi wa nchi na taifa. Anasema,

  "Kazi ya jumba la makumbusho ni muhimu sana na nitakwambia kwa nini. Kwa mfano kama leo nakwenda China na tuchukulie kwamba sina mtu ninayemfahamu kabisa nchini China na wala siijui China, sehemu gani nzuri ya kwenda na kuona, kisha kujua kuhusu watu wa China, naweza kufanya hivyo kwenye jumba la makumbusho tu kwa sababu jumba la makumbusho ni kama ninavyowaambia kila siku, ni mkusanyiko wa kumbukumbu za taifa. Hiyo ni sawa na jumba la makumbusho ya taifa la Kenya ni mkusanyiko wa kumbukumbu za Kenya. Hakuna nchi inayoweza kuwepo bila ya kuwa na jumba la makumbusho, kwa sababu linahifadhi kumbukumbu za taifa."

  Kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya majumba ya makumbusho ya mwaka huu ni "Jumba la Makumbusho lenye uwezo mkubwa wa kuunganisha: Njia Mpya, Umma Mpya", ambayo inaonesha mageuzi mapya yanayoletwa na teknolojia kwenye majumba ya makumbusho. Bw. Kibunja amesema, maendeleo ya teknolojia yanabadilisha mtazamo wa jadi kuhusu kutembelea jumba la makumbusho, hivyo jumba la makumbusho pia linatakiwa kuendana na wakati kwa kutumia njia mpya kukidhi mahitaji mbalimbali ya umma. Anasema,

  "Unajua sasa naweza kukaa, kwa mfano, ofisini kwangu au nyumbani kwangu ama sebuleni kwangu na kuweza kuona kilichomo kwenye jumba la makumbusho, ndio maana tunasema ni umma mpya, kuna watu ambao hawana muda wa kwenda kwenye majumba ya makumbusho lakini bado wanaweza kuona kilichomo kwenye majumba hayo. Ndio maana tunaongelea kuhusu majumba ya makumbusho yaliyoungana kwa kiasi kikubwa na umma mpya. Nadhani kwa ulimwengu tulionao sasa, tunalazimika kufika mahali hapo, ndio maana kwenye jumba la makumbusho ya taifa la Kenya tunaingiza vitu vyote tulivyokusanya kwenye kompyuta."

  Teknolojia kweli imeleta uwezekano mwingi kwa maendeleo ya majumba ya makumbusho, na inatoa njia nyingi zaidi kwa umma kugusa historia. Lakini Bw. Kibunja anaona kuwa utegemezi wa teknolojia hautoshi, ushirikiano kati ya mashirika ya kijamii, sehemu mbalimbali na mataifa unaweza kuzidisha uwezo mkubwa wa kuunganisha wa majumba ya makumbusho. Anasema,

  "Tuna ushirikiano mkubwa na China na bila shaka ni moja ya ushirikiano wa kihistoria kwa maana ya kwamba unajaribu kuchunguza uhusiano tuliokuwa nao katika miaka 600 iliyopita. Unajua tumekuwa tukifanya uchunguzi wa chini ya bahari na Wachina huko Lamu na Malindi na kupata meli ambazo ni mabaki ya meli tu kwa sasa kwenye pwani ya Afrika Mashariki, na hayo mabaki yanatupa historia. Na pia tunajaribu kutaka kubadilishana vitu vya maonesho kati ya majumba ya makumbusho ya Kenya na China hasa makumbusho ya jumba la kifalme tunataka kushirikiana kwa hilo, lakini muhimu zaidi pia ni kubadilishana ujuzi, wachina wamekuwa wakitusaidia kuwapa mafunzo Wafanyakazi wa Kenya katika kusimamia majumba ya makumbusho na vitu vya kale kwa sababu wana historia ndefu ya kusimamia vitu vya kale na majumba ya makumbusho. Tuna wafanyakazi kadhaa wa majumba ya makumbusho waliokwenda kwenye mafunzo nchini China, na kusema kweli naweza kusema wiki ijayo nitakwenda China kushuhudia mahafali ya kuhitimu kwa wafanyakazi wa majumba ya makumbusho ya taifa ya Kenya ambao wanatunukiwa shahada zao za uzamili na uzamivu kwenye masomo ya makumbusho. Kwa hiyo ushirikiano wetu umeanza kitambo sana. Na pia tuna ushirikiano wa kupata vifaa vingi vinavyokuja kutoka China."

  Hivi sasa jumba la makumbusho la taifa la Kenya linafanya maonesho kuhusu makabila 42 ya Kenya na historia ya pamoja, Bw. Kibunja amesema anataka kufanya maonesho hayo nchini China ili kuunganisha umma mpya wa China. Anasema,

  "Moja ya miradi mikubwa tunayoushughulikia ni kujaribu kukuza tunachokiita "maonesho ya kusafiri" kwa takriban makabila 42 ya Kenya, na pia historia ya pamoja kwa ujumla na tunatarajia maonesho haya yataweza kutembelea makumbusho mbalimbali ya China. Ili waweze kuona, tuna vitu vingi vinavyofanana kihistoria tukiwa kama binadamu. Kutakuwa na Wachina wanaoshindwa kutembelea Kenya, lakini nataka kuwapatia fursa ya kuona vitu hivi ambavyo vinasimulia historia yetu ya pamoja nchini China, hivyo lengo la maonesho ya kusafiri ni muhimu sana kwetu, na tunajaribu kushughulikia hilo."

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako