• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Kenya inalenga kuweka historia yake mtandaoni

  (GMT+08:00) 2018-05-18 19:37:44

  Dunia leo inaadhimisha siku ya jumba la makumbusho. Kaulimbiu ya mwaka huu ni kutumia teknolojia ili kuwezesha watu wengi zaidi kutembelea jumba la makumbusho mtandaoni.

  Ni siku ya majumba ya makumbusho duniani, na Kenya inajiunga na nchi nyingine kuadhimisha siku hii.

  Siku hii ilitengwa miaka 42 iliopita kutambua wajibu wa majumba ya makumbusho kama chombo cha kubadilishana tamaduni na kuhimiza umuhimu wa kuhifadhi historia.

  Maudhui ya mwaka huu ni "Nyumba za makumbusho zilizounganiswha kwa mtandao njia mpya, umma mpya".

  Katika makao makuu ya majumba ya makumbusho nchini Kenya tumezungumza na mkurungezi wake bwana Mzalendo Kibunjia kwanza akituelezea kwa nini anaona maudhui ya mwaka huu ni muhimu.

  "Maudhui ya siku ya majumba ya makumbusho mwaka huu ni muhimu kwa sababu sasa tunaondoka kutoka kwa mawazo ya kawaida ambapo watu wanafikiria kwamba jumba la makumbusho ni mahali pa kwenda, kutembea na kuona vitu vya kale ambavyo havitumiki tena. Lakini sasa tunabadilisha na kuwezesha watu kukaa kwa nyumba zao ama ofisini na kutembelea jumba la makumbusho. Ndio maana tunalenga kuunganisha watu wote na kujumuisha watu wapya kwenye mvumo wa dijitali. Hapa katika makavazi ya kitaifa ya Kenya tunaweka vitu vyetu vyote kwenye mfumo wa dijitali", anasema Mzalendo.

  Mzalendo Kibunjia anasema hakuna nchi inayoweza kuwa bila majumba ya makumbusho kwani ndio njia ya pekee ya kuelezea historia, tamaduni na safari ya watu wa ncho hiyo.

  Katika jumba la makumbusho mjini Nairobi kumehifadhiwa aina nyingi ya ndege, wanyama wa porini na baharini mashine za kale michoro na hata magazeti ya zamani.

  Kila siku wageni wa ndani na nje ya nchi wanatembelea hapa kujionea histioria ya Kenya.

  Pia kimekuwa kituo muhimu kwa wanafunzi kama vile Caroline Mungai wa kidato cha kwanza.

  ""Tumekuja hapa kwenye jumba la makumbusho kujifunza mambo mapya, kuhusu maisha ya kale, kuhusu walikotoka nyanya zetu kwa sababu tumesikia hadithi nyingi kuwahusu ila hatujui walitoka wapi. Hapa pia tumeona wanyama wengi ambao sijawahi kuwaona pia nimeona pesa za kale kama vile senti tano. Sasa hatutasahahu tena kwa sababu tumeziona na zimeingia akilini mwetu. Na kuhusu China ningependa kujionea tambi, nadhani ni tamu sana na pia kujifunza kutumia miti ya kula yaani Chopstick. Aidha ningependa kujifunza tamaduni kwa sababu nazipenda na ni mojawepo wa vitu ningeenda kuona kwenye jumba la makumbusho la China."

  Na mwalimu wake bwana Nywaraba anaona kuwatembeza wanafunzi wake hapa kuna manufaa ya moja kwa moja katika masomo yao ya kila siku .

  Alisema "Nafunza biolojia na kemia. Tunaona ni vyema kuwaleta wanafunzi wetu kwenye jumba la makumbusho ambako kuna vitu vingi na wanaweza kujionea jinsi wanyama mbalimbali walivyo na maumbile tofauti ya kujikinga na wakati huo huo tunaweza kuunganisha baiolojia na historia. Tunaweza kujionea binadamu wa kale na vile alivyobadilika mapaka sasa. Kila mwaka lzima nilete familia yangu hapa kila mwezi wa Desemba."

  Lakini uhifadhi wa historia na tamaduni haujafanikiwa bila juhudi za pande tofauti.

  Kenya imekuwa na ushirikiano mpana na China hasa katika ubadilishanaji wa utaalam na kushiriki kwa pamoja oparesheni za utafiti wa chini ya bahari.

  Bwana Mzalendo Kibunjia anasema, "Tuna ushirikiano mkubwa na China na mojawepo ni kwenye upande wa kihistoria ambapo tunajaribu kufuatilia uhusiano wetu wa zaidi ya miaka 600 iliopita. Tumekuwa tukifanya uchunguzi wa kiaikolojia kwenye maeneo ya Lamu na Malindi kujaribu kutafuta meli za China zilizozama humo. Aidha China imekuwa ikitusaidia katika utoaji wa mafunzo kwa maofisa wetu kuhusu jinsi ya kusimamia majumba ya makumbusho kwa sababu wao wana uzoefu wa muda mrefu. Pia kuna maafisa wetu ambap sasa wamepokea mafunzo nchini China na nitasafiri kwenda kushudia maafala yao wakipata vyeti vya PHD katika masomo ya majumba ya makumbusho."

  Lakini wakati huu dunia ikiadhimisha siku la jumba la makumbusho nchi zinazokumbwa na vita kama vile Syria na Mali tayari zimeshuhudia uharibifu mkubwa wa majumba yake ya kale ambayo ni sehemu ya historia yao.

  Hivyo maudhui ya mwaka huu ya kuweka makumbusho kwenye mtandao huenda ni njia moja inayoweza kuhakikisha watu wanajionea historia yao hata baada ya kuharibiwa na machafuko au majanga.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako