• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ya Walinda Amani Duniani-Juhudi za Jeshi la Kenya kulinda amani nchini Somalia

    (GMT+08:00) 2018-05-29 08:45:21

    Hii leo Kenya inaungana na nchi nyengine duniani kuadhimisha siku ya Walinda Amani Duniani.

    Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Walinda Amani Duniani ni "Walinda Amani wa Umoja Mataifa:Miaka 70 ya Huduma na Kujitolea"

    Kenya inaadhimisha siku hii wakati ikiwa inafikisha miaka 7 sasa tangu wanajeshi wa Kenya kwenda kulinda amani nchini Somalia mwaka 2011.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Tarehe 29 Mei ni siku ambayo ilitengwa na Umoja wa Mataifa kusherehekea michango ya wanajeshi na raia katika shirika hilo na kuwapatia heshima walinda amani zaidi ya 3,700 ambao wamepoteza maisha yao wakihudumu chini ya mwamvuli wa Umoja Mataifa tangu mwaka 1948,ikiwa ni pamoja na 129 waliokufa mwaka uliopita.

    Jeshi la ulinzi la Kenya chini ya mwamvuli wa majeshi ya Umoja wa Afrika,AMISOM,limekuwa mstari wa mbele katika kuleta amani na kupambana na kundi la ugaidi la Al shabaab nchini Somalia.

    Wanajeshi wa KDF wanalinda amani katika eneo la Sector 2 nchini Somalia.Eneo hili linajumuisha mpaka wa Kenya na Somalia,mji wa Dhobley,Tabda,na Afmadow.

    Eneo hili linatajwa kuwa eneo hatari zaidi kati ya maeneo sita yaliyogawanywa na Amisom nchini Somalia.

    Kamanda wa kikosi cha mahandaki katika Sector 2 Aden Hassan Ali anasema kazi yake kubwa ni kuwatia wenzake motisha wa kupambana na adui na kuhakikisha kuwa ustawi wao unazingatiwa.

    "Kazi yangu hapa ni kuwatia motisha askari wangu ili waweze kupigana hii vita"

    Kamanda wa Jeshi la Amisom Meja Jenerali Tai Gituai anasema vita dhidi ya magaidi wa Al shabaab vinaendelea ijapokuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali.

    "Tunapambana na adui ambae sio wa kawaida.Sio wa kawaida kwa sababu huwezi kuona safu ya adui,yuko kila mahali"

    Aidha Meja Jenerali Tai Gituai anasema eneo la Sector 6 lililo katika eneo la baharini la Kismayu ndio eneo jipya nchini humo,na kuwa eneo hilo linajumuisha vikosi vya usalama kutoka nchi tofauti.

    "Eneo hili lilikuwa jaribio la vikosi tofauti ambapo tuna vikosi kutoka Kenya,Burundi,na pia Ethiopia.Hii ni mara ya kwanza tumekuwa na majaribio ya vikosi tofauti mahali pamoja.Wote wanafanya kazi kulingana na mamlaka ambayo yanahitajika,na pia kulingana na mahitaji ya Umoja wa Afrika".

    Umoja Mataifa mwaka jana ulipitisha pendekezo nambari 2372 la 2017 la kutaka idadi ya wanajeshi wa Amisom ipunguzwe kwa awamu ili kupisha Jeshi la Serikali ya Somalia,SNA,kuendelea kupambana na Al-Shabaab.

    Pendekezo linataka wanajeshi kuondolewa wote ifikapo mwaka 2020.Tayari wanajeshi 1,000 waliondolewa mwaka jana huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kadri inavyokaribia mwaka 2020.

    Lakini Kamanda wa kambi ya Sector 2 Brigedia Joakim Mwamburi anasema kuwa Umoja wa Mataifa huenda unaanza kusherehekea mapema kwa kutaka wanajeshi wa Amisom kuondolewa Somalia bila kuzingatia changamoto zilizopo.

    "Wanafaa kuchelewesha kuondoa wanajeshi wakulinda amani hadi pale jeshi la SNA,ambalo wamesema wataajiri wanajeshi 1,000 kwa kila eneo wataweza kuja kushikilia nafasi za wanajeshi wa Amisom"

    Meja Jenerali Mstaafu Lucas Tumbo,anayehusika na masuala ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili jirani anasema kuwa Kenya inafanya mengi zaidi ya kusaidia tu kuleta amani nchini Somalia.

    Anasema kwamba wakenya takriban 35,000 wanaishi nchini Somalia,huku wengi wao wakipatikana eneo la Hargeisa,wakijishughulisha na biashara mbalimbali.

    "Wanajishughulisha katika sekta za ukarimu,hoteli,elimu,afya,na katika mashirika yasiyo ya serikali"

    Mwaka huu,Umoja Mataifa unasherehekea maadhimisho ya miaka 70 ya Walinda Amani wa UM.

    Ujumbe wa kwanza wa amani wa Umoja wa Mataifa ulianzishwa tarehe 29 Mei,1948 wakati Baraza la Usalama liliidhinisha kupelekwa kwa idadi ndogo ya waangalizi wa kijeshi wa UM katika Mashariki ya Kati kuunda Shirika la Usimamizi wa Suluhu la Umoja wa Mataifa (UNTSO) kufuatilia makubaliano ya silaha kati ya Israel na majirani zake wa nchi kiarabu.

    Zaidi ya miongo 7 sasa,watu zaidi ya milioni 7,wanawake kwa wanaume wamehudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa katika operesheni 71 za ulindaji amani,na kuathiri moja kwa moja maisha ya mamilioni ya watu,kulinda walio katika mazingira magumu na kuokoa maisha ya watu wasiohesabika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako