• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bei ya mafuta yapanda Tanzania

    (GMT+08:00) 2018-06-08 20:18:34

    Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati nchini Tanzania (Ewura) imetangaza kupanda kwa bei ya rejareja ya mafuta kwa Sh55 kwa lita moja ya petroli mwezi huu.

    Tangazo la Ewura lililotolewa jana linaonyesha kupanda kwa viwango tofauti kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ikilinganishwa na mwezi uliopita.

    Tangazo hilo linabainisha kuwa ongezeko la bei hizo limetokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia hivyo kuziathiri nchi zinazoagiza kutoka nje.

    Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Ewura, Nzinyangwa Mchany alisema mabadiliko hayo ya bei yalianza jumatano wiki hii.

    Wakati petroli ikipanda kwa Sh55 mwezi huu ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4, dizeli imepanda kwa Sh19 sawa na asilimia 0.88 na mafuta ya taa Sh36 au asilimia 1.68.

    Bei ya jumla nayo imepanda pia. Wauzaji wa nishati hiyo watanunua lita moja ya petroli kwa Sh54.85 zaidi kwa kila lita wakati dizeli ikipanda kwa Sh18.83 na mafuta ya taa Sh36.08.

    Mabadiliko hayo ya bei yamechangiwa na kupanda kwa bei katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na bandari pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani inayotumika kwenye ununuzi wa nishati hiyo.

    Taarifa ya Ewura inafafanua kuwa bei ya mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga imepanda pia mwezi huu ikilinganishwa na iliyokuwapo Mei.

    Kwa miaka kadhaa sasa, Ewura inatumia mfumo wa pamoja wa uagizaji mafuta kutoka nje (BPS) unaolenga kupunguza gharama ili kuwapa nafuu wananchi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako