• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano mkuu wa G7 waanza nchini Canada kukiwa na tofauti za kibiashara kati ya Marekani na Washirika wake

    (GMT+08:00) 2018-06-09 19:23:56

    Mkutano mkuu wa mwaka wa Kundi la nchi Saba G7 ambao umeanza jana ijumaa, unatarajiwa kuwa mkutano mgumu kati ya Marekani na washirika wake kutokana na wakati huu ambapo kuna suala la Marekani kutoza ushuru kwa bidhaa za chuma na alminium zinazoingizwa nchini humo.

    Viongozi wa G7 ambazo ni nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda, zikiwemo Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza, Japan na Marekani, hukutana kila mwaka kujadili ushiriki kwenye masuala ya uchumi wa dunia, mabadiliko ya hali ya hewa, usalama na amani.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari, baada ya kuwasili kwa ajili ya mkutano huo, Rais wa Marekani, Donald Trump alifanya mazungumzo mafupi na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu masuala ya kibiashara, na suala la Korea ya Kaskazini.

    Mada kuu za mkutano mkuu wa mwaka huu ni pamoja na uongezaji wa uwekezaji na kuongeza ajira ili kuongeza ukuaji na endelezaji wa masuala ya usawa wa kijinsia.

    Hata hivyo, suala la uamuzi binfasi wa Marekani wa kutangaza kutoza ushuru kwenye bidhaa za Chuma za kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na Canada huenda likachukua sehemu kubwa ya mkutano mkuu huo.

    Na kutokana na uamuzi huo wa Marekani, Canada nayo imetangaza ushuru kwenye chuma na alminium pamoja na bidhaa nyinginezo za viwandani zipatazo 71 za kutoka Marekani.

    Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, waziri wa mambo ya nje wa Canada Chrystia Freeland alisikika akisema "Tumeumizwa na tumetukanwa"

    Nayo jumuiya ya wafanyabiashara ya Canada imekuwa na mashaka juu ya namna Trump anavyoshambulia ambacho ni malengo ya kuwa na biashara huria na ya uwazi.

    Akizungumza na waandishi wa habari, mjumbe wa chama cha wafanyabiashara wa Canada amabaye pia ni waziri wa zamani wa Canada Perrin Beatty, amesema kilichopo ni kwamba Rais mmoja amewadharau viongozi wengine sita wa kundi la G7 na jambo hilo litasababisha ugumu wa upatikanaji wa wazo la pamoja la kuendelea na mambo mengine.

    Na Jana, Trump aliandika maneno makali kwenye ukurasa wake wa Twitter dhidi ya waziri mkuu wa Canada, Rais wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya biashra, akisema anatazamia "kunyoosha masuala ya kibiashara yasiyo na usawa" kati ya nchi yake na nchi za G7.

    Jambo lingine ambalo huenda likachukua sehemu kubwa ya mkutano mkuu wa mwaka wa G7 ni suala la Rais Trump kupinga mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa na kujitoa kwenye suala la nyuklia la Iran.

    Taarifa kutoka ikulu ya marekani imearifu kuwa, Trump hatahudhuria mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba ataondoka mapema zaidi kabla ya wakati aliokuwa amepanga awali.

    Mwishoni mwa mkutano huo, viongozi hao wanatarajiwa kusaini taarifa ya pamoja kuhusu nafasi ya sera na mapendekezo waliyokubaliana.

    Ufaransa na Ujerumani wameonya kuwa hawatasaini makubaliano ya mwisho mpaka hapo Marekani itakapokubali kufuata baadhi ya sera za msingi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako