Rais wa China awasili Kigali kwa ziara rasmi Rwanda
(GMT+08:00) 2018-07-23 06:29:01
Rais Xi Jinping wa China amewasili Kigali na kuanza ziara ya kiserikali nchini Rwanda ikiwa ni ziara ya kwanza ya rais wa China nchini humo.
Akizungumza na mwenzake wa Rwanda Bw. Paul Kagame, rais Xi amesema ingawa China na Rwanda ziko mbali, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa wa kirafiki. Katika miaka 47 tangu nchi hizo mbili zianzishe uhusiano wa kibalozi, pande zote mbili zimetendeana kwa usawa na urafiki, na uhusiano kati ya China na Rwanda umeendelea vizuri kwa utulivu siku zote.
Rais Xi pia amesema wakati rais Paul Kagame alipofanya ziara nchini China mwezi Machi mwaka jana, viongozi wa nchi hizo mbili walifanya mazungumzo ya kina kuhusu uhusiano kati ya nchi mbili na ushirikiano wa kunufaishana, ambayo yanaonyesha kwamba pande zote zinatilia maanani kuendeleza uhusiano kati yao. Amesema katika ziara hiyo atabadilishana maoni na rais Kagame kuhusu maendeleo ya uhusiano wa nchi mbili katika zama mpya, ushirikiano kati ya China na Afrika pamoja na masuala muhimu ya kimataifa na kikanda.
Kwa upande wake rais Kagame amesema anaamini kwamba ziara hiyo ya rais Xi Jinping itahimiza ushirikiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.
Rais Xi Jinping amekwenda Kigali nchini Rwanda baada ya kumaliza ziara nchini Senegal, ambayo ni kituo chake cha tatu katika safari yake. Baada ya kumaliza ziara nchini Rwanda, rais Xi atakwenda Afrika Kusini ambako pia atahudhuria Mkutano wa kilele wa BRICS mjini Johannesburg. Rais Xi pia anatarajiwa kutembelea Mauritius akiwa njiani kurudi nyumbani.