• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais Xi Jinping wa China ahudhuria Mkutano wa 10 wa kilele wa BRICS na kutoa hotuba muhimu

  (GMT+08:00) 2018-07-27 09:22:28

  Mkutano wa 10 wa Viongozi wa nchi za BRICS unaendelea kufanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Jana marais wa China, Brazil, Russia pamoja na waziri mkuu wa India walihudhuria mkutano huo na kujadiliana kuhusu ushirikiano kati ya nchi za BRICS na masuala muhimu ya kimataifa wanayoyafuatilia kwa pamoja na kufikia makubaliano.

  Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kuhusu "kugeuza ruwaza kuwa hali halisi" ameonesha umaalumu muhimu wa kipindi cha mapinduzi mapya ya kiviwanda, kutoa mapendekezo kuhusu maendeleo ya ushirikiano wa nchi za BRICS katika siku za baadaye, na kusisitiza kuwa nchi za BRICS zinapaswa kushirikiana na kuhimiza kwa pamoja mchakato wa kujenga dunia yenye amani ya kudumu, usalama, ustawi wa pamoja, iliyo wazi na shirikishi, na yenye usafi na uzuri.

  Rais Xi amesisitiza kuwa nchi za BRICS zinatakiwa kufuata mkondo muhimu wa kihistoria, kuhimiza uhusiano wa wenzi wa kimkakati, ili kutimiza ruwaza iliyowekwa kwa ajili ya mwongo ujao. Pia ameeleza kuwa, nchi za BRICS zinapaswa kuonesha mustakabali mkubwa katika ushirikiano wa kiuchumi; kulinda amani na usalama wa kimataifa; kukuza mawasiliano ya kiutamaduni na kuunda mtandao wa uhusiano wa karibu wa kiwenzi.

  Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema hivi sasa hali ya upande mmoja na kujilinda kibiashara inafufuka duniani, hali ambayo imeleta athari hasi kwa masoko mapya na nchi zinazoendelea. Nchi za BRICS zinahitaji kuimarisha ushirikiano, kulinda utaratibu wa pande nyingi, na hadhi ya uongozi ya Umoja wa Mataifa pamoja na kanuni za Shirika la biashara duniani WTO.

  Rais Michel Temer wa Brazil amesema, nchi za BRICS zinabeba majukumu yanayofanana ya kujiendeleza, hivyo zinatakiwa kuimarisha ushirikiano, kukabiliana kwa pamoja matishio na changamoto mbalimbali.

  Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, ili kukabiliana na hali ya kimataifa yenye utatanishi, nchi za BRICS zinatakiwa kushirikiana na kushikilia uhusiano wa pande nyingi na kanuni za kimataifa, kulinda kwa pamoja utaratibu wa uchumi, ili kuhimiza maendeleo yenye kiwango cha juu na yenye usawa, na kutatua masuala muhimu ya kikanda kwa njia ya kisasa.

  Waziri mkuu wa India Bw. Narendra Modi amesema nchi za BRICS zikiwa msukumo muhimu wa maendeleo ya dunia, zinapaswa kujiunga na mchakato wa kukamilisha usimamizi wa dunia, kuhimiza biashara huria na kusukuma mbele mafungamano ya kiuchumi ili kuwanufaisha watu wengi, na kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea.

  Wakati wa mkutano huo Azimio la Johannesburg la viongozi wa nchi za BRICS limetangazwa ambalo limetoa ishara bayana ya kulinda utaratibu wa pande nyingi na kupinga hatua za kukilinda kibiashara, na kuamua kuanzisha uhusiano wa wenzi wa mapinduzi mapya ya kiviwanda, na kukuza ushirikiano katika nyanja za uchumi, biashara na fedha, usalama wa kisiasa na mawasiliano ya kiutamaduni.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako