• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • NACADA  na wanawake wa Mombasa waunga mkono pendekezo la kupiga marufuku muguka (majani ya miraa) mjini humo

  (GMT+08:00) 2018-08-14 18:56:35

  Baraza la Kitaifa la kupambana na matumizi ya mihadarati (NACADA),mashirika ya kijamii na wanawake wa kaunti ya Mombasa wamejitokeza kuunga mkono pendekezo la serikali ya kaunti ya Mombasa la kutaka kupiga marufuku matumizi ya muguka,ambayo ni aina ya miraa (khat) katika kaunti hiyo.

  Kilevi hicho kinasemekana kuharibu vijana na kuwafanya kuingia kwenye magenge ya ujambazi na pia kusababisha familia na ndoa nyingi kuvunjika.

  Mwandishi wetu Khamis Darwesh anatuarifu.

  Vita dhidi ya matumizi mabaya ya madawa ya kulevya vinazidi kupamba moto mjini Mombasa.Kwa takriban wiki moja iliyopita serikali ya kaunti ya Mombasa ilivamia vibanda vya kuuza muguka na kuvibomoa.

  Muguka ni majani madogo ya kijani ambayo ni aina ya miraa,na inasemekana ni kilevi kilichosababisha uharibifu mkubwa na mmomoyoko wa maadili katika kaunti ya Mombasa.

  Katika Ripoti yake,Kamati ya Afya ya Bunge la Mombasa ilisema kuwa muguka umeathiri pakubwa ndoa nyingi na kuchangia kuvunjika kwa baadhi ya ndoa hizo.

  Mshirikishi wa Baraza la Kitaifa la kupambana na mihadarati eneo la Mombasa Bi Farida Rashid anasema wanaunga mkono marufuku ya muguka kwa sababu mmea huo unapatikana kwa urahisi na unatumiwa hadi na watoto wadogo ambao hujiingiza katika makundi ya uhalifu.

  "Kila mihadarati ina athari zake,na kila kila mihadarati kuna ambayo ni mbaya zaidi ya nyingine.isi tunazungumzia muguka kwa sababu inatumiwa na vijana wadogo.Muguka ni kitu ambacho kinamuumiza Yule mtoto ndio unaona watoto wengi saa hii wameingilia magenge ya ujambazi.Mtoto wa miaka 12 au 13 anakushikia panga"

  Aidha Bi Rashid amesema hakuna nyumba hata moja mjini Mombasa ambayo haijaathirika na matumizi ya muguka,hivyo ipo haja ya kuunga mkono jitihada hizi zinazofanywa na serikali ya kaunti ya Mombasa..

  "Kila wakati kina mama wanakuja kunililia.Hakuna nyumba ambayo haijaathirika.Mimi kama mama nimejitolea kuungana na serikali ya kaunti ya Mombasa na wamama wa Mombasa kuhakikisha mswada wa kupiga marufuku muguka Mombasa umepita.Tukiangalia kaunti ya Kwale wamepitisha,kwa nini na sisi hapa tusipitishe?"

  Kiongozi wa vijana ambaye ni mkazi wa Mvita Bi Mariam Mohamed anasema wazazi wa Mombasa wanafaa kulaumiwa kwa kuwaacha watoto wao kutafuna muguka.

  "Vijana wengi saa hizi hawaendi skuli haswa skuli za umma,hawaingii darasani mpaka wale muguka.Pia wazazi wenyewe wameregea nyuma kwa kuwaendekeza watoto wao.Kwa sababu wanaona ni nafuu hawajui kama inawaathiri watoto wao.Tunaomba sana muguka ipigwe marufuku"

  Mwenyekiti wa Shirika la wahudumu wa afya wa kujitolea la CHVs Bi Khadija Kassim anasema asilimia 78 ya vijana mjini Mombasa ni mateja na watumizi wakubwa wa muguka.

  "Sisi kama wahudumu wa vijijini na wasaidizi,kulingana na utafiti wetu asilimia 78 ya vijana na akina mama wameathirika na muguka.Kila mwezi tunapata kisa cha mtoto kuathirika na muguka.Tuko na ushahidi thabiti wa kuonesha kwamba muguka umeathiri pakubwa.Lilipokuja hili suala la kupiga marufuku muguka sote tulifurahi na bado tunaunga mkono na tutasukuma hadi ifike mahali iwe hakuna muguka"

  Mombasa ni kaunti ya tatu sasa ambayo imeingia katika kampeni ya kupiga marufuku mmea huo huku serikali ya kaunti ya Kwale ikiwa mwezi Machi mwaka huu ilipitisha mswada wa kuzuia kuuzwa na kutumiwa kwa Muguka.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako