• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Kujenga taswira ya maisha bora kwa kutumia chuma na saruji

  (GMT+08:00) 2018-08-24 07:55:22

  Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China alitangaza kuinua kiwango cha uhusiano kati ya China na Afrika, kuwa uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote. Pia alitoa mipango 10 mikubwa ya ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, miundombinu, fedha, maendeleo yasiyochafua mazingira, kurahisisha biashara na uwekezaji, kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya watu, afya, utamaduni, amani na usalama. Katika kipindi cha leo, unasikiliza sehemu ya kwanza ya mfululizo wa ripoti zetu, kuhusu "Kujenga taswira ya maisha bora kwa kutumia chuma na saruji".

  Hiyo ni mipango ya ushirikiano halisi kati ya China na Afrika, ambayo ilifungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya pande hizo mbili. Wakati mkutano mpya wa kilele wa FOCAC utafanyika hapa Beijing, tunakuletea maelezo juu ya utekelezaji wa mipango hiyo, na hali ya ustawi ya uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote. Maelezo ya leo yanahusu ushirikiano wa viwanda.

  "tunatumai kuwa kutokana na kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa nafasi za ajira na mapato, tutaweza kujenga nyumba za bei nafuu nchini kote. Ni ndoto yangu kwamba katika muda mfupi ujao, watu wenye mapato ya kati nchini Kenya wataweza kumudu kununua nyumba nzuri."

  Hayo yalisemwa na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipotoa hotuba mwezi Mei mwaka huu, akisisitiza mara nyingine tena kuhusu lengo la kupatikana kwa nyumba za bei nafuu, ikiwa ni sehemu ya ajenda yake ya Big Four. Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya mwaka jana, rais Kenyatta alitoa ajenda hiyo ya Big Four inayozingatia kutatua masuala yanayokabili maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Kenya. Kuhusu suala la nyumba, rais Kenyatta ameweka mpango wa kujenga nyumba laki tano za bei nafuu kabla ya mwaka 2022.

  Ripoti iliyotolewa mwaka 2017 na Benki ya Dunia inaonesha kuwa, mashirika ya ujenzi nchini Kenya yanajenga nyumba zisizozidi elfu 50 kila mwaka, na kuacha pengo la nyumba zaidi ya milioni mbili, ambapo asilimia 61 ya familia za mijini zinaishi katika makazi duni. Hivi sasa Kiwango cha ukuaji wa miji nchini Kenya ni asilimia 4.4, ikiwa ni sawa na ongezeko la wakazi laki tano wa mijini kila mwaka, hali ambayo itapanua zaidi pengo la ukosefu wa nyumba.

  Je, ni kwa vipi Kenya itaweza kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba? Mapema mwaka 2016, kampuni ya ujenzi ya Wuyi ya China tawi la Kenya iliwekeza dola milioni 100 za kimarekani kujenga kituo cha utafiti na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, na supamaketi ya vifaa vya ujenzi mjini Nairobi, ikiwa ni juhudi zake za kutafuta ufumbuzi wa suala hilo. Kituo hicho chenye eneo la ekari 29.6, kina mistari sita ya uzalishaji. Naibu meneja mkuu wa Kampuni ya Wuyi Tawi la Kenya Bw. Lin Yihua, anaona muundo wa jadi wa majengo yanayojengwa kwa matofali na zege una ukomo wake kwenye maendeleo ya majengo ya mijini nchini Kenya.

  "Tumefanya utafiti katika miji mitatu ya Nairobi, Mombasa na Eldoret, barabara kwenye maeneo ya kati ya miji hiyo ni nyembamba, na hakuna nafasi za kutosha za kuweka vifaa vingi vya ujenzi, matatizo hayo mawili hayawezi kuepukwa kwenye ujenzi wa majengo ya zege. Mbali na hayo, ujenzi wa majengo ya aina hiyo unahitaji malori mengi ya kubeba zege na saruji, na usafiri wa malori hayo utatoa kelele kubwa, na kuleta vumbi nyingi na maji chafu mijini."

  Ili kutatua changamoto hiyo, Kampuni ya Wuyi ya China Tawi la Kenya imeamua kuingiza muundo wa kisasa wa "majengo ya kuunga" nchini Kenya. Mwaka 2017, mistari sita ya uzalishaji ya kampuni hiyo yote ilianza kufanya kazi, ambayo sehemu mbalimbali za majengo, zikiwemo nguzo na ukuta, zitatengenezwa kwanza viwandani kabla ya kuunganishwa na kuwa majengo kamili. Bw. Lin Yifu amesema, njia hiyo mpya ya ujenzi inapunguza kidhahiri matumizi ya nishati ikilinganishwa na muundo wa jadi.

  "Tunatengeneza sehemu mbalimbali za majengo viwandani, halafu sehemu hizo zitasafirishwa kwenye eneo la ujenzi na kuungwa kuwa majengo. Njia hii ya kuunganisha majengo inachukua asilimia 1 hadi asilimia 5 tu ya eneo la kuweka vifaa vya ujenzi ikilinganishwa na ile ya kawaida. Kwa kutumia teknolojia hii ya kisasa, matumizi ya chuma pia yamepungua, kwa kuwa tunatumia makalibu ya chuma ambayo yanaweza kutumika zaidi ya mara elfu mbili, ikilinganishwa na mara 3.5 tu ya makalibu ya mbao. Viunzi vyote vya zege vinatengenezwa viwandani, ambako pia kuna vifaa vya kushughukulia maji taka."

  Bw. Lin Yihua amesema matumizi ya makalibu ya chuma si kama tu yameongeza ufanisi wa matumizi ya malighafi, na bali pia yameinua kidhahiri ubora wa majengo.

  "Makalibu ya mbao yaliyotumika zamani yana dosari katika usahihi wa kutengeneza viunzi sanifu vya ujenzi, lakini makalibu ya chuma tunayotumia sasa yametatua kabisa dosari hizi, na hivyo kuinua kidhahiri ubora wa majengo."

  Hivi sasa mahitaji ya nyumba na majengo mengi ya kiraia nchini Kenya yamezidi ugavi kwa kiasi kikubwa, na majengo ya kuunganisha yenye sifa za muda mfupi wa ujenzi na gharama ya chini, yanalingana na mahitaji ya Kenya. Bw. Lin Yihua ametolea mfano wa mradi wa jengo la ofisi za Benki kuu ya Kenya unaojengwa na kampuni yake. Anasema,

  "Miradi kama huu, kwa njia ya kawaida, inamalizika kwa muda wa miaka nne na nusu hadi mitano, kama ukijengwa kwa njia ya kuunganisha viunzi, inachukua miaka mitatu hadi minne, kwa jumla inaweza kupunguza theluthi moja ya muda wa ujenzi. Kwa ufupi tunaweza kusema kwa kutumia njia hii mpya tanaweza kujenga nyumba nyingi zaidi ndani ya muda sawa, ili kufikia lengo la serikali ya Kenya. Makadirio yetu ya gharama pia yanalingana na gharama zinazotakiwa na serikali ya Kenya, kama ikijumuishwa na gharama za ukusanyaji fedha, gharama zetu za mradi zitakuwa hata chini zaidi, na muda tunaohitaji kukamilisha ujenzi utakuwa mfupi zaidi, ndiyo maana itaweza kuleta faida haraka zaidi."

  Bila shaka maendeleo ya teknolojia yanaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, mashirika ya China yanatumai kuwa yataweza kuhamisha teknolojia za kisasa za China nchini Kenya, ili wakenya waweze kunufaika kutokana na teknolojia hizo na kujiendeleza.

  "Madhumuni yetu ya kufanya jambo hili nchini Kenya ni kusaidia kuinua kiwango cha ujenzi barani Afrika, kuandaa mafundi ujenzi wazawa, na kuvileta barani Afrika vitu bora vya China, wala sivyo vitu vilivyopitwa na wakati kwa kupitia "Ukanda mmoja, Njia moja". Hivi sasa tumeweza kutoa nafasi zaidi ya mia sita za ajira, na kati ya hizo mafundi ujenzi waliopewa mafunzo maalumu wanachukua nafasi zipatazo 200, kama kuna miradi ya nyumba za bei nafuu, kwa wastani tunaweza kutoa nafasi 2,500 hivi za ajira kwa kila mradi."

  Miaka minne iliyopita, Pepela Edwin alikuwa ni mtunza bustani huko Naivasha, mwaka 2014 alijiunga na kampuni ya Wuyi ya China tawi la Kenya na kujifunza ufundi seremala, hivi sasa amepandishwa cheo na kuwa kiongozi wa timu katika kituo cha utafiti na uzalishaji cha kampuni hiyo. Bw. Edwin anaona kampuni ya Wuyi imeshuhudia kila hatua ya maendeleo yake.

  "kufanya kazi hapa kumenisaidia sana, kumeweza kunisaidia kuinua uwezo wangu, mwanzoni nilikuwa nafanya kazi rahisi za mikono, baadaye nikajifunza ufundi seremala, hivi sasa nimekuwa kiongozi wa timu yetu. Mabadiliko makubwa pia yametokea katika maisha yangu, kabla ya kuja hapa, sikuwa na shamba, sikuwa na familia, lakini sasa nimenunua shamba na nimefunga ndoa, na pia nimejenga nyumba mpya. Baada ya kujifunza ufundi seremala, nimeweza kutengeneza vitu vingi, kama vile meza na viti, hata nyumba yangu mpya ninajenga mwenyewe. Natumai kuwa katika siku zijazo nitaendelea kufanya kazi hapa, kujifunza ufundi mwingi zaidi, na kuboresha maisha yangu, pia nataka kununua gari."

  Pamoja na maendeleo ya biashara zao nchini Kenya, makampuni ya China yameleta manufaa mengi zaidi kwa wananchi wa Kenya, na wakati huohuo pia yamepatana zaidi na wenyeji wa huko.

  "Tulipofika katika maeneo ya magharibi, ambako kuna upungufu wa maji, tulijenga mabwawa ya kuhifadhia maji, kwenye maeneo yaliyoko nyuma kiuchumi, tulijenga shule, na wakati walipokumbwa na majanga, tuliwapatia chakula na vitu vya msingi katika maisha, haya ni majukumu yetu ya kijamii. Kwa kweli tumeungana na wenyeji, na pia hatukujichukulia kama ni kampuni ya kigeni, kwani zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wetu ni wenyewe wa Kenya."

  Mtaalamu wa sekta ya nyumba ya Kenya anaona, katika mazingira ambayo rais Uhuru Kenyatta anajitahidi kuhimiza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, sekta ya nyumba ya Kenya inatarajiwa kufufuka mwaka huu, katibu wa chama cha CPC katika kampuni ya Wuyi ya China tawi la Kenya Bw. Wang Shuwen amesema China na Kenya zinatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano kwenye sekta ya ujenzi ya kisasa.

  "Tumehamisha nguvu bore zetu za uzalishaji nchini Kenya, ambazo zinaungana vizuri na zile za Kenya. Naamini kuwa China inaweza kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na Kenya kwenye sekta ya ujenzi ya kisasa, ili kunufaishana zaidi. Pia tunatumai kuwa tunaweza kufanikisha miradi ya ujenzi wa nyumba nchini Kenya, ili kuwanufaisha kihalisi watu wa Kenya."

  Viwandani mashine zinaendelea kufanya kazi, na viunzi mbalimbali vya ujenzi vinatengenezwa kwa utaratibu, vile vilivyokamilika vimesafirishwa nje, na kuunda taswira ya maisha bora ya wananchi wa Kenya.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako