• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kituo cha kuzalisha umeme cha Karuma kinawawezesha watu wa Uganda waone mwanga wa maendeleo

    (GMT+08:00) 2018-08-26 16:50:13

    Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China alitangaza kuinua kiwango cha uhusiano kati ya China na Afrika kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote, na kutoa mipango 10 mikubwa ya ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, miundombinu, fedha, maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, kurahisisha biashara na uwekezaji, kuondoa umaskini na kuwanufaisha watu, afya, utamaduni, amani na usalama.

    Hiyo ni mipango ya ushirikiano wa kivitendo kati ya China na Afrika, na ilifungua ukurasa mpya wa kihistoria kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili. Kabla ya mkutano mpya wa kilele wa FOCAC utakaofanyika hivi karibuni hapa Beijing, tunakuletea mfululizo wa maelezo juu ya utekelezaji wa mipango hiyo, na kujionea uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote ulio wa kiwango kipya na uhai mpya. Katika maelezo ya leo, utasikia jinsi Kituo cha kuzalisha umeme kwa maji cha Karuma kinavyoboresha maisha ya watu wa Uganda.

    Katika sehemu ya mwisho ya Mto White Nile wa Ziwa Viktoria huko Kiryandongo, kaskazini mwa Uganda, wataalamu wa kitengo cha 8 cha kampuni ya Sinohydro ya China wanashirikiana na wafanyakazi wa Uganda kufanya juhudi za kipindi cha mwisho kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa maji cha Karuma, ambacho ni mradi mkubwa zaidi katika historia ya Uganda. Mradi wa Karuma ulizinduliwa mwezi Disemba mwaka 2013 na asilimia 15 ya fedha za mradi zilitolewa na serikali ya Uganda na asilimia 85 zilizobaki zilitokana na mikopo iliyotolewa na Benki ya Uuzaji na Uagizaji ya China. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, na utakuwa kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme wa maji katika kanda ya Afrika Mashariki.

    Uganda ni nchi iliyo nyuma duniani kwa matumizi ya umeme ya mtu mmoja mmoja. Katika sehemu za mijini, asilimia 40 ya watu wanatumia umeme, na idadi hiyo ni asilimia 6 tu katika sehemu za vijijini. Pia watu wengi wanashindwa kumudu bei kubwa za umeme. Hii imepunguza zaidi mahitaji ya watu ya umeme. Ukweli ni kuwa Uganda ina nguvu bora za kimaumbile katika uzalishaji umeme kwa maji. Meneja mkuu wa mradi wa Karuma Bw. Deng Changyi amesema mto Nile una mwendo tulivu wa mtitiriko wa maji, maji ya kutosha, hauna msimu wa mtiririko mdogo wala mtiririko mkubwa wa maji, na ufanisi wa mitambo ya kuzalisha umeme unaweza kutumiwa ipasavyo na uwezo wa kuzalisha umeme ni wa uhakika na ni tulivu.

    "Mradi wa Karuma umehimizwa na marais wa China na Uganda, na unabeba wajibu wa kutimiza ndoto ya miaka 100 ya kuwatajirisha watu na kuongeza nguvu ya taifa, ni mradi muhimu kwa dira ya taifa ya maendeleo 2040 ya Uganda. Baada ya kukamilika, mradi huo utaweza kutoa umeme wa uhakika na bei nafuu wa kilowati saa bilioni 4 kila mwaka kwa Uganda, kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme mara dufu, kuiletea serikali ya Uganda mapato ya umeme ya dola za kimarekani milioni 200, kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na uzalishaji viwandani na kuifanya Uganda ielekee kuwa nchi yenye kipato cha kati duniani."

    Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Uganda UEGCL ni mmoja wa wamiliki wa mradi wa Karuma, na meneja wake anayeshughulikia mambo ya ushirikiano Bw. Simon Kasyate amesema kampuni ya Sinohydro ni mwenzi mzuri wa ushirikiano katika ujenzi wa mradi na uandaaji wa wataalamu.

    "Katika kujenga kituo hicho cha kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa maji cha Karuma, kampuni ya Sinohydro inakubali kusikiliza maoni yetu na kurekebisha mipango yao, ni mkandarasi anayewajibika. Sisi sote tunaamini kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati, kwa bajeti, na kwa kiwango cha juu. Wakati huohuo, kampuni ya Sinohydro imetusaidia kujenga uwezo na kutoa mafunzo ya kiufundi kwa wafanyakazi wetu. Naona hii ni muhimu sana, kwani baada ya mradi huo kukamilika, wafanyakazi wetu wanaweza kudumisha na kuendesha wao wenyewe kituo hicho cha kuzalisha umeme kwa maji. Naona mradi wa Karuma utakuwa mfano wa kuigwa katika historia ya ukandarasi na ufundi nchini Uganda, pia ushirikiano wa teknolojia ya hali ya juu na ubunifu kati ya nchi zetu mbili hautamalizika kwenye mradi huo, na hakika utaendelea."

    Mbali na kuhimiza uchumi wa taifa na sekta ya uzalishaji umeme nchini Uganda, mradi wa Karuma pia umetengeneza nafasi nyingi za ajira kwa watu wa Uganda. Hivi sasa, mradi umewaajiri wafanyakazi wazawa 6,300, Bw. Khamisi Soniko ni mmojawapo. Kutoka mfanyakazi wa kawaida wa mradi huo miaka mitano iliyopita hadi naibu meneja utumishi wa sasa, uzoefu wote wa kikazi alio nao Bw. Khamisi amepata kwenye mradi wa Karuma.

    Uhusiano wa Bw. Khamisi na mradi wa Karuma ulianzia mwezi Novemba mwaka 2012. Wakati ule, yeye alihitimu katika chuo kikuu na kwenda kutafuta kazi katika mradi huo. Kutokana na kwamba mradi huo ulikuwa haujaanza rasmi, nafasi za ajira zilikuwa chache, na hakukuwa na moja iliyomfaa, na nafasi wazi ya kazi ilikuwa ni ya udereva tu. Japo ni tofauti na aliyojifunza chuoni, lakini kutokana na imani na kampuni ya China na sekta ya uzalishaji umeme wa maji, Bw. Khamisi aliamua kubaki na kuwa mmoja wa wafanyakazi wazawa wa mapema zaidi wa mradi wa Karuma.

    Katika miaka sita iliyopita, mbali na kuendesha gari, Bw. Khamisi alifanya kazi zote alizopewa kwa makini. Baada ya kupandishwa cheo mara mbili, sasa anafanya kazi kwa imani katika ofisi ya idara ya utumishi ya mradi wa Karuma. Akizungumzia uzoefu wake wa kikazi katika mradi wa Karuma katika miaka kadhaa iliyopita, Bw. Khamisi amesema anashukuru uaminifu wa kampuni ya China, pia anashukuru juhudi zake za kuendesha gari lake la Pickup kuingia katika majira ya Spring.

    "Nilipokuwa dereva, nilipewa kazi mbalimbali na wenzangu wachina tena sio za aina moja au mbili tu, na nimezichukulia kazi hizo kama fursa za kujifunza. Kufanya hivyo kunaweza kukufanya uwe na ushindani mpaka uthubutu kukubali changamoto mahali popote pale. Nataka kusema kuwa fursa niliyopewa na Sinohydro, wamewezesha masomo niliyojifunza yatumiwe, kupanua upeo wangu wa ujuzi, kuinua uwezo wangu wa ufundi stadi, na napanga kujifunza shahada ya pili ya kozi ya nguvukazi baadaye."

    Bw. Khamisi anaona kuwa, ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa maji cha Karuma umetoa nguvu kubwa za kuhimiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya sehemu zilizo karibu na mradi huo.

    "Mradi wa Karuma kweli umekuza maendeleo ya uchumi wa sehemu zilizo karibu, na mapato ya wakazi yameongezeka kidhahiri. Mwaka 2013, kama una nyumba ya kupangisha, kila mwezi uliweza kupata Shilingi elfu 7 tu, lakini sasa ni laki 1.2. Vijana waliouza maji katika mabasi hivi sasa wamekuwa na ardhi zao na kufanya biashara."

    Ukweli ni kwamba mradi wa Karuma sio tu umeinua mapato ya wakazi wanaoishi katika sehemu za karibu, pia umetekeleza majukumu mbalimbali ya kijamii. Kampuni ya Sinohydro imejenga daraja katika kijiji kilicho na umbali wa saa nne kwa kuendesha gari kutoka kwenye mradi, kuchimba visima 10 kwa shule za karibu, kutoa huduma bure za matibabu katika uwanja wa michezo wa shule ya msingi ya Karuma, kusambaza dawa bure kwa wakazi wa huko na kujenga soko jipya la mboga…… Tarehe 8, Machi mwaka huu, kampuni ya Sinohydro ilishirikiana na wamiliki wa mradi kufadhili ada za shule na gharama za maisha za miaka minne kwa wanafunzi wawili wa kike wa shule ya sekondari, na kuwasaidia warudi tena shuleni.

    Mwenyekiti wa baraza la mji mdogo wa Karuma Bw. Washington Chaya ameshuhudia shughuli hizo za ustawi wa jamii na pia amenufaika nazo.

    "Kabla ya kuanza kwa mradi huo, mkandarasi wake kampuni ya Sinohydro iliiahidi serikali ya Uganda kusaidia maendeleo ya kijamii katika mji wetu, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya huduma za matibabu, kuchangisha pesa kwa watu wenye shida kiuchumi na kujenga shule. Tumeishi vizuri na kampuni ya SinoHydro, kwani wao kweli wametufanyia mambo mengi mzuri. Mbali na mifano iliyotajwa juu, wao pia wameshiriki kwenye ujenzi wa miundombinu, walichimba visima na kutuwezesha tupate maji, walitupatia rasilimali za kujenga nyumba na walitujengea barabara mpya. Bila shaka, sehemu zisizokuwa na umeme sasa zina umeme. Naona mchango mzuri uliotolewa na mradi huo kwa jamii yetu ni dhahiri."

    Katika sehemu ya katikati ya jengo la ofisi ya mradi wa Karuma, kuna bango linalosema "Sinohyro Together with Ugandans to Built a Better Future" yaani Sinohydro inashirikiana na watu wa Uganda kujenga siku nzuri za baadaye. Kama ilivyosema sentensi hiyo, kutoka kiwanda cha kushughulikia gesi asili cha Tanzania na mradi wa bomba la gesi uliomalizika mwaka 2015, reli ya kutoka Addis Ababa hadi Djibouti iliyozinduliwa mwaka 2016, hadi reli ya kisasa ya SGR ya Mombasa- Nairobi iliyoanza kufanya kazi mwaka 2017 na kiwanda cha kuzalisha umeme kwa maji cha Karuma kinachotarajiwa kumalizika na kuanza kufanya kazi mwaka huu, serikali ya China na wananchi wake siku zote wanapenda kushirikiana na wenzao wa Afrika, kutekeleza mradi mmoja baada ya mwingine wa ujenzi wa miundombinu na kuifanya izae matunda, na kujenga mustakbali mzuri wa uhusiano kati ya China na Afrika katika siku za baadaye.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako