• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Ushirikiano wa ulinzi wa mazingira kati ya China na Afrika wachangia mazingira ya Afrika

  (GMT+08:00) 2018-08-28 08:21:13

  Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China alitangaza kuinua kiwango cha uhusiano kati ya China na Afrika kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote. Pia alitoa mipango 10 mikubwa ya ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, miundombinu, fedha, maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, kurahisisha biashara na uwekezaji, kuondoa umaskini na kuwanufaisha watu, afya, utamaduni, amani na usalama.

  Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa China na Afrika umekuwa ukipata maendeleo kwa kasi, ni lengo la pamoja kwa pande hizo mbili kupata maendeleo huku mazingira yakilindwa vizuri. China imepata uzoefu mzuri katika kulinda mazingira ya ikolojia na maendeleo yasiyo na uchafuzi wa mazingira, na inaweka mkazo mkubwa katika kulinda mazingira mazuri ya ikolojia katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati yake na Afrika.

  Benki ya uagizaji na uuzaji wa bidhaa nje ya China ni benki ya kipekee iliyoidhinishwa na serikali ya China kushughulikia utoaji wa mikopo kwa Afrika, ambayo ni chanzo muhimu cha fedha kwa ushirikiano wa uwezo wa uzalishaji na ujenzi wa miundo mbinu barani Afrika. Naibu mkuu wa benki hiyo Bw. Xie Ping ameeleza kuwa, benki hiyo inatoa kipaumbele kwa maendeleo yasiyo na uchafuzi wa mazingira katika ushirikiano kati ya China na Afrika. Anasema:

  "Katika mchakato wa kuunga mkono ushirikiano kati ya China na Afrika, benki hii inafanya juhudi kuzisaidia nchi za Afrika kutafuta maendeleo yasiyo na uchafuzi wa mazingira, na kutekeleza ujenzi wa miradi inayohusika. Kwa mfano mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati ya upepo nchini Ethiopia ambao ulifadhiliwa na benki hii, umeisaidia nchi hiyo kuongeza uwezo wa kiteknolojia katika kuendeleza nishati ya upepo, kupunguza gharama za kujiendeleza, na kutoa mfano mzuri kwa nchi nyingine barani Afrika katika kuendeleza nishati isiyo na uchafuzi wa mazingira. Vilevile benki hii inazielekeza kampuni za China barani Afrika kutekeleza majukumu ya kijamii katika kulinda mazingira, mfumo wa ikolojia na mazingira ya asili."

  Ushirikiano kati ya China na Afrika kamwe hautafanyika kwa kuharibu mazingira ya ikolojia na maslahi ya muda mrefu ujao. Tangu rais Xi Jinping wa China alipotangaza "Mipango mikubwa ya ushirikiano kati ya China na Afrika", China imeimarisha ushirikiano na Afrika katika sekta ya nishati isiyo na uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa wanyamapori na mimea.

  Kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi, katika miaka ya hivi karibuni, nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme, namna ya kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme bila ya kuleta uchafuzi wa mazingira ni changamoto kubwa inayozikabili nchi hizo. Akiba ya maji, upepo na jua barani Afrika inachukua asilimia 10, 32 na 40 ya akiba ya jumla ya dunia nzima, hivyo kuweka mazingira mazuri kwa Afrika kuendeleza nishati isiyo na uchafuzi wa mazingira. China inazisaidia nchi za Afrika kuendeleza nishati ya umeme isiyo na uchafuzi wa mazingira kutokana na sifa zake za fedha na teknolojia, na kusifiwa na pande mbalimbali.

  Mradi wa uzalishaji wa umeme wa Adama uliotolewa mkopo na Benki ya uagizaji na uuzaji wa bidhaa nje ya China uko sehemu ya katikati nchini Ethiopia. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hicho ilianza kufanya kazi mwaka 2012, hivi sasa mitambo ya awamu ya pili ya mradi huo pia imeunganishwa na kuanza kuzalisha umeme. Huu si kama tu ni mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo katika Afrika Mashariki, bali pia ni mradi mkubwa zaidi wa nishati endelevu unaoungwa mkono na China katika nchi za nje. Pia umetoa mchango mkubwa katika kuendeleza nishati isiyo na uchafuzi wa mazingira, kuhimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kuboresha maisha ya watu wa huko. Aidha katika miaka kadhaa iliyopita, China vilevile ilisaidia Kenya kujenga kituo cha nishati ya jua katika kaunti ya Garissa, nishati ya upepo katika eneo la kipeto katika kaunti ya Kajiado, na na umeme kwa kutumia mvuke katika eneo la Ol Karia kwenye kaunti ya Nakuru. Waziri wa nishati wa Kenya Bw. Charles Keter anasema:

  "Ningependa kuishukuru serikali ya China kwa kusaidia juhudi zetu za kuwa na nishati endelevu. Kwa mara ya kwanza tutakuwa na ajira ya kijani, yaani zaidi ya watu 3000 wataajiriwa kwenye mradi huu. Pia sasa tutakuwa na nishati safi isiyochafua mazingira, hivyo naona huu ni mradi wenye athari chanya."

  Mradi mwingine nchini Kenya wa reli ya SGR inayounganisha miji ya Nairobi na Mombasa ambayo ilijengwa na kampuni ya ujenzi ya China, inapita Hifadhi ya wanyamapori ya Tsavo nchini humo. Ili kupunguza kwa kiasi kikubwa zaidi athari hasi zinazoletwa na reli hiyo kwa wanyamapori, ubunifu wa reli hiyo ulizingatia ulinzi wa mazingira usio na uchafuzi wa mazingira, na kujenga mashoroba(passageway) 14 yanayowawezesha wanyamapori kupita. Mbunifu mkuu wa reli hiyo Bw. Zhang Jingqiao anasema:

  "Njia ya reli hiyo ilichaguliwa kwa makini kufuatia kanuni ya kulinda mazingira. Tumechukua hatua mfululizo kupunguza athari mbaya kwa kiasi kikubwa kwa mazingira ya ikolojia ya kienyeji."

  Kadiri uchumi na jamii zinavyopata maendeleo kwa kasi, ndivyo nchi za Afrika zinavyotambua umuhimu wa kulinda mazingira ya asili, na Umoja wa Afrika umetangaza mradi wa "Ukuta Mkuu wa kuhifadhi mazingira" ambao umezishirikisha nchi nyingi barani Afrika. Kutokana na mpango huo, nchi zinazohusika zitapanda ukuta wa miti kwa kufuata eneo la Sahel lililoko mpaka wa Jangwa la Sahara. Ukanda huo wenye upana wa kilomita 5 na umbali wa kilomita 7,000 utakuwa eneo muhimu kwa Afrika katika kukinga na kushughulikia majangwa. Mwezi Septemba mwaka jana, Idara ya utafiti ya ikolojia na jiografia ya Xinjiang katika Taasisi ya sayansi ya China pamoja na upande ulioanzisha Mradi wa "Ukuta mkuu wa kuhifadhi mazingira" zilisaini makubaliano zikiahidi kuwa watafiti wa China watajiunga na ujenzi wa mradi huo. Mratibu wa Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP anayeshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika Bw. Richard Munang anaona kuwa, China ina uzoefu na teknolojia ya juu katika upandaji wa miti. Anasema:

  "Mradi wa 'Saihanba' umelibadilisha jangwa lililoko kaskazini ya China kuwa kituo cha uzalishaji wa kilimo na misitu, teknolojia kama hiyo inatakiwa kuigwa duniani, kwani si kama tu inaweza kukabiliana na changamoto zinazoletwa na kuongezeka kwa jangwa, bali pia itasaidia kulirudisha jangwa kuwa mashamba yanayoweza kulimwa, jambo linalohitajika sana na dunia yenye ongezeko kubwa la idadi ya watu."

  Kutokana na mipango ya ushirikiano, China itaimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika maendeleo yasiyo na uchafuzi wa mazingira, kuzisaidia nchi za Afrika kutekeleza miradi mfululizo kuhusu kushughulikia mazingira, nishati isiyo na uchafuzi wa mazingira, kuandaa mipango kuhusu utoaji wa gesi isiyo na uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa wanyamapori na mimea, ili kuzisaidia nchi za Afrika kutimiza Ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako