• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Kikosi cha kulinda amani cha China nchini Sudan Kusini chachangia ushirikiano wa amani na usalama kati ya China na Afrika

  (GMT+08:00) 2018-09-02 18:18:40

   

  Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China alitangaza kuinua kiwango cha uhusiano kati ya China na Afrika kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote, na kutoa mipango 10 mikubwa ya ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, miundombinu, fedha, maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, kurahisisha biashara na uwekezaji, kuondoa umaskini na kuwanufaisha watu, afya, utamaduni, amani na usalama.

  Hiyo ni mipango ya ushirikiano halisi kati ya China na Afrika, ambayo ilifungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya pande hizo mbili. Wakati mkutano mpya wa kilele wa FOCAC utafanyika hapa Beijing, tunakuletea maelezo juu ya utekelezaji wa mipango hiyo, na hali ya ustawi ya uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote. Maelezo ya leo yanahusu ushirikiano wa amani na usalama.

  Jua ni kali katika majira ya joto nchini Sudan Kusini, lakini halikuwatisha askari wa kulinda amani kutoka China waliokuwa wakifanya mazoezi nje ya nyumba. Kikosi hiki cha watu 700 kiliingia mjini Juba, Sudan Kusini mwezi Novemba mwaka 2017, na majukumu yake ni kulinda msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa, kufanya doria katika kambi za wakimbizi, kutoa ulinzi kwa operesheni za uokoaji wa jamii, na kukamata silaha haramu kwa kushirikiana na polisi wa kulinda amani.

  "Mimi ni askari wa kikosi cha nne cha kulinda amani cha China nchini Sudan Kusini, naitwa Li Dong, hii ni mara yangu ya pili kuja na batalioni ya askari wa miguu ya kulinda amani. Kila ninaposhika zamu ya doria, nitatumia dakika tatu au tano kuwafundisha askari wenzangu, namna ya kushika zamu ya ulinzi na doria. Kwa mfano namna ya kushughulikia hali ya dharura, na ni hatua gani zinafaa kuchukuliwa kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa mataifa, hatuwezi kuwa na mahangaiko, tunatakiwa kushughulikia kila kinachotokea kwa kufuata utaratibu wetu."

  "Mimi naitwa Lin Xiao, hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki kwenye operesheni za kulinda amani katika nchi ya nje. Siku moja hivi karibuni, wakati t tunapumzika kwenye UN House, milio ya risasi ilisikika ghafla kwenye kambi ya wakimbizi. Platuni ya mwitikio wa haraka ilifikia katika eneo la tukio mara moja, hali ya wakati ule ilikuwa ya hatari sana. Lakini nikiwa ni ofisa wa mawasiliano, na mtu wa pekee anayeongea Kiingereza, ilinibidi kujitokeza kutekeleza majukumu yangu."

  "mimi ni sajini wa Kikosi cha kwanza cha Batalioni ya askari wa miguu ya kulinda amani, naitwa Yang Tao. Huu ni mwaka wa kumi ambao sikuweza kujumuika na wazazi wangu kusherehekea Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi, kweli najisikia vibaya kila ninapowakumbuka. Wakati wa sikukuu ya mwaka mpya, tulikuwa kwenye doria na tuliwafundisha lugha ya kichina watoto tuliokutana nao njiani, kuwafundisha namna ya kusema Heri ya mwaka mpya kwa kichina, na tukapiga video na kuituma nyumbani watazame, wote waliguswa sana."

  Ili kuwalinda wanawake na watoto, kikosi hicho kina kikundi cha askari 11 wa kike. Mazoezi wanayofanya ni sawa na ya wanaume, na wao pia ni shupavu wanapotekeleza majukumu yao.

  "Naitwa Hao Ruiting, nina umri wa miaka 21, hivi sasa nafanya doria kwenye njia ya Kusini mashariki. Majukumu yetu ya kila siku ni kufanya doria na ulinzi, wakati wa doria, tutajizatiti na kubeba vifaa vyote na silaha, na kuvaa nguo na kofia za kuzuia risasi, na tunashika zamu kwa wastani wa saa saba kila siku."

  Kila siku kikosi hicho kinapeleka askari zaidi ya 560 nje kutekeleza majukumu. Wanabeba mizigo zaidi ya kilo 20 na kufanya kazi kwa saa zaidi ya 8 kila siku. Hii ni kazi ngumu, haswa kwa wanawake.

  "Mimi ni sajini wa kikosi cha askari wanawake cha Batalioni ya askari wa miguu wa kulinda amani, naitwa Yu Peijie. Tangu nilipojiunga jeshini, wote wanapenda kuniita 'Kaka Qiang Ge'. Nakumbuka mara ya kwanza niliposhika zamu ya doria, tulitekeleza majukumu yetu sawa na wanavyofanya askari wanaume, na kushika ulinzi tukiwa ndani ya maderaya. Siku hiyo ilikuwa ni joto sana, Sote tulitokwa na jasho, na tulikuywa na vumbi usoni, kichwani na nguoni, hatimaye tukaonekana kama sanamu za udongo. Wakati ule nilimsikia mtu mmoja akisema 'labda hao wote ni askari wanaume', kweli niliposikia hiyo nilikuwa nafurahi sana moyoni kwa kuwa naona hii ni sifa kubwa kwetu."

  Mwezi Septemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za kulinda amani, rais Xi Jinping wa China aliahidi kujenga kikosi cha watu 8,000 cha kulinda amani, kuwafundisha askari 2,000 wa kulinda amani kutoka nchi nyingine, na kutoa msaada wa kijeshi wa dola milioni 100 za kimarekani kwa Umoja wa Afrika.

  Kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini Sudan Kusini ni mfano mzuri wa China wa kujiunga na operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa barani Afrika. Kijiji cha Nakitun chenye familia 500 ni moja ya sehemu kikosi hicho kinapofanya doria. Mwenyekiti wa kijiji hicho Charles Lado alipozungumzia mabadiliko ya hali ya usalama kijijini humo baada ya kuja kwa wanajeshi wa China, anasema,

  "Kabla ya kuja kwa walinda amani wa China hali ni mbaya kutokana na wahalifu lakini tangu waanze kulinda eneo hili, hali sasa imekuwa zuri na watu wako salama na tunawashukuru kwa kazi yao. Tunaomba wengine waendelee kuja ili tuwe na amani. Uhusiano wa wakaazi wa hapa n walinda amani wa China ni mzuri sana na nawashukuru sana. Tutaendelea kujenga urafiki na uhusiano wetu pamoja na kupata amani."

  Licha ya kufanya doria kwa saa 12 kila siku, askari wa China pia wanatoa msaada wa matibabu kwa wakimbizi waliojeruhiwa, na hata baadhi ya wakati wanawapeleka watu waliolewa pombe nyumbani kwao. Mwanakijiji wa Nakitun Mary Bosco anasema,

  Mary Bosco: Kila siku tunawapenda wachina kwa sababu wanashika doria usiku na mchana. Sasa tuko salama ikilinganishwa na awali ambapo wezi walikuwa wanatuvamia usiku na mchana.

  Mwanahabari: Kwa hiyo wanakuletea hema, ili kila mtu aweze kuingia?

  Mary Bosco: Wachina walitupatia huduma za matibabu ya malaria na homa ya matumbo hapa kwenye kijiji chetu cha Nakitun na sasa kila mtu ana afya zuri. Waliwapa dawa watu wote. Hivyo kazi yao sio tu kulinda amani lakini pia n kutoa misaada ya kibinadam kusaidia watu wa Nakitun.

  Tarehe 8 mwezi Julai mwaka 2016, makundi ya jeshi la serikali ya Sudan Kusini yalipambana vikali mjini Juba. Kwa bahati mbaya gari la kikosi cha China lilipigwa na roketi, wanajeshi wawili walifariki, na wengine watano kujeruhiwa. Katika miaka 26 iliyopita tangu China ianze kujiunga na operesheni za kulinda amani, wanajeshi 19 wa China wamefariki. Kamanda wa kikosi hicho Chen Ximing anasema,

  "Mapambano yanatokea hapa na pale. Kikosi chetu huenda sehemu yenye hatari zaidi. Katika miezi mitatu iliyopita, tumeshughulikia matukio 224 ya hatari. Wanajeshi wetu wanakabiliwa na hatari za aina mbalimbali."

  Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Sudan Kusini, ambaye pia ni kiongozi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja huo nchini humo David Shearer alisema, raia zaidi ya milioni mbili wa Sudan Kusini walikimbia makazi yao kutokana na vita, kikosi cha askari wa China nchini Sudan Kusini si kama tu wamelinda usalama wa watu, bali pia kimetoa mchango kwa ajili ya ukarabati wa uchumi na jamii nchini humo. Anasema,

  "Hatutaki watu kwenye kambi, tunawataka nyumbani kwao. Lakini tusisahau kazi muhimu inyofanywa na kundi la wahadisi wa China wanaojenga barabara katika eneo la Magharibi mwa nchi hii. Bila kuwepo na wahadisi hao wachina magari ya misaada na biashara haingeweza kufanyika. Tumependezwa sana na jinsi walinda amani wa China wamefanya kazi hapa Sudan Kusini. Wanafanya kazi kwa utaalam wa hali ya juu na kuonyesha ushirikiano mzuri na wenyeji ambalo ni jambo muhimu."

  Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Johannesburg wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, rais Xi Jinping wa China alisema,

  "China na nchi za Afrika zote ni nguvu muhimu za kulinda amani na kuhimiza maendeleo duniani. Tuna wajibu na uwezo wa kufanya kazi zaidi katika masuala ya kimataifa, na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa ajili ya ujenzi wa mahusiano mapya ya kimataifa yanayozingatia ushirikiano na mafanikio ya pamoja."

  Mkurugenzi wa kituo cha ushirikiano wa usalama cha ofisi ya ushirikiano wa kimataifa wa kijeshi ya wizara ya ulinzi ya China Jenerali Zhou Bo alisema, kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za kulinda amani rais Xi Jinping alitoa ahadi nyingi ambazo ni nadra kwa nchi nyingine. Anasema,

  "Kwanza, tuna nia thabiti ya kisiasa, yaani kuongeza ushiriki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa mataifa. Pili, wanajeshi wa China wana sifa nzuri. Tatu ni kwamba jeshi la China lina vifaa vizuri vya kisasa. Unachohitaji sasa Umoja wa Mataifa, ni vikosi vya kisasa vyenye teknolojia ya hali ya juu. China ndiyo ni nchi yenye sifa hizo tatu, tuseme ni sifa za kipekee. Ni hakika kwamba katika siku zijazo, China itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye shughuli za kulinda amani duniani."

  Kikosi cha China nchini Sudan Kusini ni kikosi kamili pekee cha China cha kulinda amani katika nchi za nje. Kwa kukabiliwa na mazingira magumu ya kiasili, hali mbaya ya usalama na hali duni ya ugavi, kikosi hicho hakikati tamaa hata kidogo. Kamanda wa kikosi hicho Chen Xi Ming anasema,

  "Ingawa wanajeshi wetu wanakabiliwa na mazingira magumu, majukumu mazito na shinikizo kubwa, lakini wamedumisha mshikamano na kufanya kazi kwa taratibu. Watatoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa uhusiano mpya wa kimataifa na jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, na mambo ya diplomasia yenye umaalumu wa China."

  "Madhumuni yangu ni kuthibitisha thamani yangu, na kuitika wito wa rais Xi Jinping."

  "Napenda vitu vya kuvutia kama vile maua na kuwa na nywele ndefu. Lakini nikiwa mwanajeshi, nina wajibu."

  "Tumekuja hapa kwa agizo la taifa, matumaini ya familia zetu na majukumu ya kijeshi."

  "Fahari yetu kubwa zaidi ni kulihudumia taifa letu. Nikiwa mwanajeshi wa miaka mingi, nataka kutoa mchango wangu."

  "Nikiwa mwanajeshi, kulinda amani katika nchi ya nje ni fahari kubwa kwangu.

  "Rangi ya anga ni ya kibuluu, na bendera ya kitaifa ni nyekundu. Tunafunga safari tukiwa na majukumu mapya. Tunaaga familia zetu kwa ajili ya taifa, na kuanza safari ndefu. Sisi tunalinda amani, hatuogopi changamoto yoyote. Wanajeshi wa China wote ni ndugu…."

  Huu ni Wimbo wa Wanajeshi wa Kulinda Amani, pia ni ahadi ya wanajeshi wa China. Tunaamini kuwa ushirikiano wa amani na usalama kati ya China na Afrika utaendelea siku hadi siku.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako