• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mkutano wa Kilimo Barani Afrika wafunguliwa rasmi jijini Kigali, Rwanda

  (GMT+08:00) 2018-09-06 08:13:58

  Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (Africa Green Revolution Forum) umeanza rasmi jana jijini Kigali,Rwanda.

  Mkutano huu unawakutanisha viongozi wa mataifa ya Afrika,mawaziri,wawakilishi wa sekta binafsi,wakulima,wanasayansi,na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kujadiliana kuleta mabadiliko na mapinduzi ya kijani barani Afrika.

  Mkutano huu wa Mapinduzi ya Kijani Barani ulifunguliwa rasmi jana hapa jijini Kigali,katika jumba la mikutano la Kigali Convention Centre.

  Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Ongoza,Pima,Kua:Kuwezesha njia mpya za kubadilisha wakulima wadogo kufanya kilimo biashara endelevu".

  Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo,Waziri Mkuu wa Rwanda Mheshimiwa Edouard Ngirente alisema licha ya bara la Afrika kuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji katika kilimo,bado bara hili liko nyuma katika masuala ya kilimo.

  "Changamoto zilizoko ni utumizi mdogo wa pembejeo za kisasa za kilimo,upatikanaji mdogo wa fedha,miundombinu mibovu ya kufikia soko,na utumiaji mdogo wa mbinu za unyunyizaji"

  Hata hivyo alisema kuna mipango mingi inayotekelezwa na taasisi na nchi mbalimbali,ambayo inaweza kutumika kama chombo cha kuongeza uwezo wa kilimo wa bara la Afrika.

  Alisema ni lazima mikakati kabambe iwekwe ili bara la Afrika liweze kupiga hatua kubwa katika kilimo.

  "Kupeleka kilimo cha bara la Afrika hadi hatua nyengine kutahitaji mipango thabiti ya kuibadilisha mikakati iliyopo na kuifanya kwa vitendo.Sote tunaelewa kwamba mageuzi ya kilimo barani Afrika yatahitaji juhudi za ziada.Tunahitaji kujitolea zaidi ili kutekeleza mikakati katika nchi zetu,lakini sote tunajua kuunda sera sio sawa na utekelezaji wa sera yenyewe"

  Rais wa shirika la Kilimo Barani Afrika,AGRA,Dk Agnes Kalibata, alisema ipo haja ya bara la Afrika kujitathmini ni kwa nini ndio bara pekee ambalo halijitoshelezi kwa chakula.

  "Mbali na kukumbatia teknolojia,kwa nini bara la Afrika ndilo bara pekee duniani ambalo halijitoshelezi kwa chakula?Haya ni mambo ambayo tunafaa kujiuliza,ni mambo tunayofaa kuzungumza.Na sio tu kuzungumza tunafaa kuchukua uongozi na kuanza kujipima maendeleo yetu"

  Mkurugenzi wa shughuli ya Kilimo cha Kimataifa katika Benki ya Dunia,Dk Simeon Ehui alisema kuwa kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikijaribu kujitosheleza kwa chakula kwa kufanya umwagiliaji wa mashamba makubwa,na tunajua matokeo yanakuwa vipi.

  Alisema hivi sasa duniani kote umwagiliaji unaofanywa na wakulima unatumiwa kama chombo cha kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mkulima,haswa hii inafanyika sana barani Asia.

  "Umwagiliaji wa mashamba ni muhimu sana,na kama Benki ya Dunia,IFC,na washirika wake tunaongeza uwekezaji katika sekta hii"

  Dk Ehui pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwaboresha wakulima wa mashamba madogo kwa kuwawezesha kwenda mbele kupelekea mazingira ya kilimo biashara na hatimaye kuinua uchumi.

  Jukwaa hili la kila mwaka la Kilimo huandaliwa na Shirika la Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA) na linatarajiwa kukamilika jumamosi tarehe 9 Septemba.

  Shirika la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika linalenga kuimarisha uongozaji na maongozi ya ufadhili kwa kusukuma uzalishaji wa kilimo na mapato ya wakulima katika mazingira ya njia ya uendelevu.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako