• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • SGR, Reli yangu
    Hadithi ya Diana, meneja wa holeti mjini Mombasa

    (GMT+08:00) 2018-10-22 10:22:43

    Kwenye makala yetu ya hadithi za SGR leo mwandishi wetu anaangazia sekta ya hoteli mjini Mombasa.

    Mji wa Mombasa.

    Ni wenye kuvutia watalii kwa wingi kutoka ndani na nje ya nchi.

    Upepo wake ni mwanana na yenye bahari na fukwe za kupendeza.

    Lakini katika siku za nyuma ilikuwa ni vigumu kwa watu wengi kufika hapa kwani hakukuwa na njia rahisi ya usafiri.

    Na sasa usafiri wa kuelekea pwani umekuwa rahisi kutokana na kuwepo kwa reli mpya ya SGR ambayo inatumia muda wa saa nne unusu tu, ikilinganishwa na usafiri wa barabarani ambao unachukua zaidi ya saa nane.

    Na matokeo yake ni wazi na ni furaha kwa wenye hoteli kama anavyoeleza Bibi Diana Amayi meneja wa mauzo kwenye Hoteli ya Swahili Beach

    "Mombasa na Diani naweza nikasema imesaidia sana kwa sababu tunapata watu wengi ambao wanakuja kwa sababu ya SGR. Kabla ya hapo ilikuwa lazima mtu atafute basi, asafiri kwa usiku nzima na ilikuwa inafanya watu wengi wasitake kuja Mombasa. Biashara kubwa ya hoteli huwa ni ya kufanya mikutano, na watu awali walikuwa wanakwenda Nakuru lakini sasa wameanza kuja Mombasa kwa sababu safari imepungua. SGR imeileta Nairobi karibu na Mombasa na Diani kwa jumla."

    Bei ya nauli ya treni mpya hii kati ya Nairobi na Mombasa ni kati ya dola 10 na dola 30.

    Watu wengi wanasafiri kwenye daraja la kwanza ambalo bei yake ni dola 10 tu na hivyo wanaona ni nafuu sana ikilinganishwa na dola 15 kwenye basi au dola 50 kwa ndege.

    "Kama unataka kusafiri na labda kuja kuona ufukwe hutataka kutumia pesa nyingi sana. Kwa hivyo hii imesaidia sana kwa sababu watu awali walikuwa wakikataa kwenda Mombasa, kwenye hoteli nzuri lazima wapande ndege ambayo ni ghali sana ama basi ambayo itachukua muda. Lakini SGR imesaidia sana hasa kwa sababu ya bei yake nafuu na sasa watu wanaweza kuleta familia zao."

    Kulingana na takwimu za chama cha utalii mjini Mombasa idadi ya watalii wa ndani wanaofika eneo hilo imepanda kutokana na huduma za SGR.

    Mwaka jana utalii wa ndani kulingana na chama hicho ulikua kwa asilimia 14.6 na vitanda milioni 3.6 vikiwa vimelipiwa na watalii wa ndani ikilinganishwa na vitanda milioni3.1 mwaka 2015.

    Hali hii pia imeendelea kuimarika wakati SGR ikiwa kwenye mwaka wa pili tangu ianze huduma. Anasema Diana.

    "Mwezi wa Aprili na Julai mara nyingi huwa hakuna watalii wengi na hata baadhi ya hoteli huku Diani huwa zinafungwa lakini mwaka huu tumeona hali imeimarika kumekuwa na shughuli nyingi na hoteli nyingi zilikuwa na kazi nyingi na hiyo inaonyesha SGR imesaidia."

    Ili kuvutia watalii zaidi wa ndani, wenye hoteli hutuma mabasi kwenda kuwapokea wasafiri katika kituo cha treni cha miritini.

    Lakini sasa wanaliomba shirika la reli nchini humo kuanzisha mpango wenye uhakika zaidi ili kuwezesha wasafiri wanaotembelea Mombasa kwa ajili ya utalii tu kutengewa viti na kifurushi maalum.

    "Tungependa watupatie njia ya kuwezesha wateja wetu kupata nafasi kwenye treni pindi tu wanapolipia hoteli, lakini huwa tuna mabasi yetu ambayo yanachukua wale ambao tayari wamelipia hoteli, hapo Miritini."

    Hadithi ya SGR kama anavyosema Diana imeleta msisimko sio tu Kenya lakinihata kwa nchi nyingi za Afrika.

    Mawaziri, na watu wa ngazi za juu kutoka nchi nyingine za Afrika wamekuwa wakitembelea Kenya ili kujionea mafanikio ya SGR wakiwa na matumaini kwamba uwekezaji sawa na huu wa China utafika kwenye nchi zao hivi karibuni.

    Naye Diana anaelezea alipotembelea Rwanda siku moja.

    "Nilienda Kigali siku moja, na watu wengi hapo hata hawajui Diani walikuwa wanasema sasa kuna treni inakuja Mombasa na ile iliweza kuvutia watalii wa kule kuja hapa kwa sababu wanaona imekuwa rahisi. Na pia barani Afrika sio nchi nyingi zilizo na treni hivyo wanakuja Kenya kutumia treni."

    Hadi sasa zaidi ya watu milioni moja wamesafiria treni ya SGR tangu ianze oparesheni zake Juni 2017.

    Serikali ya Kenya inatarajia usafiri huu utawezesha sekta ya utalii kukua, kufungua nafasi zaidi za ajira na hatimaye kuunganisha kanda ya Afrika Mashariki na hadi reli itakapofika Malaba kwenye mpaka wa Kenya na Uganda.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako