• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • SGR, Reli yangu
    Hadithi ya Mugo na Sharon, wahudumu wa SGR waliopata mfunzo China

    (GMT+08:00) 2018-10-24 10:46:03

    Kwenye makala yetu ya hadithi za SGR leo mwandishi wetu amekutana na Kennedy Mugo na Chelangat Sharon, wahudumu wa abiria kwenye treni mpya ya SGR kati ya Nairobi na Mombasa.

    Wawili hao ni miongoni mwa wale waliopata mafunzo nchini China.

    Ni sauti za Kennedy Mugo na Chelangat Sharon ambao ni wahudumu wa ndani ya treni mpya ya kisasa nchini Kenya na wamekuwa wakifanya kazi hapa kwa zaidi ya mwaka mmoja unusu.

    Kennedy aliwahi kufanya kazi kwenye shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways hivyo anaweza kulinganisha majukumu ya kuhudumia wasafiri.

    "Ninapofika asubuhi shughuli za kupanga abiria huwa zinaanza kama saa kumi na mbili asubuhi, mnaingia kwenye treni mnahakikisha kila kitu kiko sawa, halafu mnakaribisha abiria saa moja hivi na dakika arobaini halafu saa mbili na dakika ishirini treni inaondoka."

    Katika safari moja, treni hiyo inabeba abiria 1,200 ikianzia kituo kikuu cha Nairobi, na kwenda Athi River, Emali, Kibwezi, Mtito Andei, Voi, Miaseny, Mariakani, na hatimaye Miritini.

    Kwenye safari hii Sharon ana jukumu muhimu la kuhakikisha wasafiri wanafika salama.

    "Kazi yangu ni kuangalia abiria, niwachunge, ili kuhakikisha kwamba wanafika kwenye kituo chao vizuri na kwa muda unaotakikana, kuhakikisha usafi wa hali juu, kuchunga watoto, na kila mtu ajisikie amechungwa vizuri na wafurahie."

    Kabla ya kuanza kufanya kazi hapa Sharon na Mugo walipokea mafunzo yaliyotolewa na wataalamu wa China hapa nchini Kenya na baadaye wakasafiri nchini China kwa mafunzo zaidi na pia kujionea jinsi treni za China zinavyofanya kazi.

    Mugo anasema kutokana na mafunzo waliyopata sasa utendaji kazi wao umeimarika na wameweza kuendesha opresheni zao kwa mafanikio makubwa.

    "Sisi mafunzo tuliyopokea ni ya kichina na baadaye tukapata nafasi ya kwenda China kujionea moja kwa moja jinsi wanavyoendesha shughuli kwenye treni zao. Tuliwasili mjini Beijing na kuabiri treni moja hadi mji wa Wuhan ambayo ilichukua saa tano hivi kwenye umbali wa kilomita karibu 1000. Tulipomaliza mafunzo hapo tukaelekea mjini Chengdu. Wafanya kazi wa huko wamejitolea sana kwa kazi yao ndio tukaweza kuelewa vile walivyotaka nasi tuwe tukifanya kazi na sasa tumerudi na kuweza kuleta hayo mafunzo kwa wengine."

    Baada ya muda uliowekwa, Kenya itakuwa na jukumu la kuendesha yenyewe oparesheni za treni hii.

    Ingawa sasa wakenya wanaendelea kuwa na uwezo wa kufanya hivyo na kupata mafunzo siku hadi siku, Sharon anasema mafunzo aliyopata hadi sasa yanamwezesha kufanya kazi bila ya msaada mwingi.

    "Ndio naweza bila ya wachina lakini hao ndio walionipa muongozo na kunifunza lakini kukiwa na upungufu tunaweza kuwaomba msaada na tunasaidiana mkono kwa mkono."

    Kwa miaka mitano Mugo alifanya kazi kwenye shirika la ndege la Kenya na kwa wengi wenye umri mdogo kama yeye wanaiona kama sekta yenye ufanisi na fursa kubwa.

    Lakini anasema alizingatia maswala kadhaa na kuamua kujiunga na SGR ambayo ndio reli ya kwanza ya kisasa kwenye kanda ya Afrika Mashariki iliyojengwa na wachina.

    "Niliona kwamba siku za baadaye za SGR ni nzuri na kuna fursa kubwa sana na pia haitakuwa na shughuli nyingi za kwenda nje mara kwa mara. Nikaona pia naweza kutumia fursa hii kama jukwaa la kuendeleza shauku yangu ya kuhudumia wateja. Naweza nikasema SGR ni kitu muhimu sana kwangu, hata ukiniamsha usiku jina la kwanza kusema itakuwa SGR kwa sababu muda, mawazo na maisha yetu yote tumeelekeza hapo na ni kama huwa tunaishi hapa, hakuna nafasi ya kurudi nyuma ni mbele, mbele na kuendelea."

    Sharon anajivunia kuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kuwa mtoa huduma kwenye treni mpya.

    Yuko tayari kukabili changamoto yoyote kwenye kazi za kila siku na pia anawaalika wakenya wasafiri kwenye treni hiyo na kujionea huduma zake za kisasa.

    "Wapande kwanza treni, waone jinsi tunavyofanya kazi na waone kwamba tuna viwango vizuri na kila kitu kinafanyika kwa njia ya hali ya juu kwa kufuata saa, mavazi. Tumefunzwa na wachina kufanya haya yote lakini pia kuna ile furaha ya wakenya hata tuna madereva wanawake kwa hivyo waje wajionee."

    Kennedy Mugo na Chelangat Sharon ni mfano wa ushirikiano wa kuhamisha utaalamu wa sekta ya huduma kutoka China hadi Kenya kupitia mafunzo.

    Pia ni ishara kwamba lengo la jumla la ushirikiano huo ni kuwezesha nchi nyingi za Afrika kuendesha zenyewe miradi yao iliyoanza kwa msaada wa China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako