• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • SGR, Reli yangu
  Hadithi ya Jeff, afisa wa ngazi ya kati ya SGR

  (GMT+08:00) 2018-10-26 10:28:08

  Kwenye makala yetu ya hadithi za SGR leo mwandishi wetu anazungumza na Jeff Muiruri ambaye ni afisa wa ngazi ya kati kwenye mradi wa ujenzi wa reli kati ya Nairobi na Narok.

  Jeff Muiruri anafanya kazi katika kampuni ya China Communications (CCCC) inayojenga reli ya kisasa nchini Kenya.

  Yeye ni afisa wa mawasiliano na jukumu lake ni kuwa daraja kati ya kampuni na wakaazi walio karibu na reli hiyo na pia maafisa husika wa serikali.

  "Nahusika sana sana na mambo ya vile jamii inahusika na SGR na hasa katika mambo ya mashamba kuangalia ni watu wangapi wameathiriwa na reli yenyewe ili kujua ni wapi kunahitajika kufanywa malipo."

  Jeff ni afisa wa ngazi ya kati kwenye kampuni hii.

  Alisomea nchini China na anaweza kuzungumza kwa ufasaha kichina.

  "Kuwa na uwezo wa kuelewa lugha zote pia inasaidia kwa sababu nilipokuwa nchini China pia nilijifunza lugha ya kichina na inasaidia sana kwa vile kuna wahadisi wengine ambao tunafanya nao kazi pale wa kutoka China na wakati mwingine lugha inaweza kuwa ni tatizo kidogo lakini nikiwa pale naingilia kati na kusaidia kama kuna jambo lolote wanataka kueleza wafanyakazi ama watu wa nje wanaoathiriwa na SGR kwa njia yoyote ile."

  Hadi kufikia sasa mradi huo wa reli ya kisasa umetoa ajira kwa zaidi ya watu 30,000 na kuufanya kuwa mradi unaoajiri watu wengi zaidi kwa pamoja nchini Kenya.

  Licha ya kuwa kuna wakenya wanaofanya kazi za mikono, lakini pia kampuni hiyo ya China inatoa fursa za ngazi ya juu kwa kufuata viwango vya elimu na mahitaji husika.

  Jeff anasema mbali na manufaa ya jumla ya kurahisisha uchukuzi, pia mradi huu umepunguza shinikizo la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana.

  "Kwangu mimi SGR imekuwa ni njia ya kuwapa wakenya nafasi ya ajira na pia kusaidia mipango yetu ya kuelekea ruwaza ya 2030. Nafikiri pia katika kila kazi, iwe ni kampuni ya Kichina ama ya Kenya, ukimpatia mtu nafasi ya kazi lazima awe na uwezo wa kufanya ile kazi na vyeti vinavyolingana na kazi yenyewe. Sikubaliani na watu ambao wanasema kwamba mkenya hatapatiwa nafasi ya kazi za ofisi, bora uwe na vyeti kila mkenya ana nafasi sawa na mtu wa nje pia."

  Sasa Jeff yuko kwenye awamu ya pili ya ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Nairobi ya Narok yenye urefu wa kilomita 120.

  Licha ya kuwa reli ya SGR imeleta mwamko mpya wa kiuchumi kwenye maeneo inakopitia, lakini pia baadhi ya jamii zinahitaji elimu kuhusu manufaa ya mradi huo.

  Jeff anakumbuka eneo moja walilokuwa wanajenga handaki lakini pia kulikuwa na changamoto ya lugha.

  "Nakumbuka tulikuwa tunataka kuanza kujenga lile handaki katika kaunti ya Kajiado na lilikuwa na urefu wa kilomita 1 hivi. Wenyeji wa hapo ni wamasai na hawaelewi kiingereza wala Kiswahili nao wahandisi wetu wachina wanaongea kiingereza kidogo na kichina na ili kukubaliana maswala ya eneo tutakapofanyia kazi ilinibidi niende hapo na kukaa huko karibu muda wa wiki mbili. Hapo niliweza kutuliza hali na tukamaliza kazi hiyo."

  Mara kwa mara jamii inakopitia reli wakaazi wanafanya maandamano wakitaka kwanza kulipwa kabla ya mradi wenyewe kuendelea.

  Ijapokuwa serikali inawafidia watu wote wanaoathirika, lakini ukosefu wa ufahamu kuhusu mchakato husika ndio chanzo kikubwa cha maandamano. Jeff anaelezea.

  "Nafikiri kwamba toka mwanzoni watu wengi hawajaweza kuelewa uhusiano wa kampuni ya ujenzi na tume ya kitaifa ya ardhi. Kwa kawaida kampuni ya CCCC hainunui mashamba lakini tunachofanya ni kuandikiana tu na kukubaliana na wenye mashamba kwamba kuanzia muda fulani tutaendelea na kazi halafu baadaye tume ya ardhi itakuja kufidia shamba hilo kwa sababu mahali ambapo reli inapitia baadaye panamilikiwa na serikali na hiyo ni kumaanisha kwamba serikali itanunua shamba lako kulingana na makubaliano ya mwenye shamba na serikali yenyewe."

  Kama maelfu ya watu walioajiriwa kufanya kazi hapa kwenye mradi wa SGR, Jeff anajivunia kuwa na fursa ya kihistoria ya kushiriki ujenzi wa reli ya kisasa lakini pia kuendeleza daraja la urafiki na mawasiliano kati ya China na Kenya.

  "Naendelea kukua na huu mradi kadiri unavyosonga mbele kwa sababu kila mara maisha yangu yanaendelea kubadilika. Naona hizi ni nafasi tunazoweza kupata kuendeleza nchi yetu. Kwa hivyo nafikiri kila siku ninapokuwa kwenye kampuni hii na kufanya kazi kwenye mradi huu mawazo yangu ni kwamba Kenya inaendelea kubadilika. Nafikiri ilikuwa ndoto mwanzoni lakini sasa tunaona ni kitu kinachoweza kufanyika."

  Mpango wa baadaye wa serikali ya Kenya ni kufikisha reli hii kwenye mpaka wake na Uganda ili kuanza kuunganisha kanda ya Afrika mashariki katika mfumo mmoja wa uchukuzi wa reli.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako