• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Matukio makubwa yaliyotokea wiki hii (Novemba 3-Novemba 9)

  (GMT+08:00) 2018-11-09 16:06:55
  Abiria watatizika kufuatia msako wa matatu Nairobi

  Abiria wengi wanaendelea kutatizika jijini Nairobi baada ya shughuli za usafiri jijini humo kuathirika tangu siku ya jumatatu kufuatia msako wa magari ya umma unaotekelezwa na maafisa wa trafiki.

  Matatu (daladala) nyingi zimenaswa na polisi wa trafiki katika msako huo kwa makosa ya kupiga muziki kwa sauti ya juu, mapambo ya rangi nyingi, kukosa mikanda ya usalama, na yale yasiyofaa kuwa barabarani.

  Kufuatia msako wa magari ya umma katika jiji la Nairobi, wakazi wengi wamelazimika kutembea masafa marefu kutokana na kukosekana kwa magari ya umma maarufu matatu kwani mingi yamenaswa kwa makosa mbalimbali ya trafiki.

  Magari machache ambayo yako barabarani yameongeza nauli maradufu, na kuzidi kuwaumiza kiuchumi abiria wanaotumia usafiri huo.

  Oparesheni hii inalenga kuhakikisha kuwa madereva na wenye magari ya umma wanazingatia sheria za trafiki maarufu "sheria za Michuki" kama vile kufunga vidhibiti mwendo, kuwa na mikanda ya usalama, kutocheza muziki kwa sauti ya juu, magurudumu yaliyoidhinishwa, kutii sheria za barabarani, miongoni mwa mambo mengine.

  Hata hivyo baadhi ya wahudumu wa matatu wamelalama wakisema kuwa msako huo unawalenga visivyo kwani wanakamatwa bila kuambiwa makosa yao.

  "Huu si ungwana. Kama gari iko na makosa onyesha lakini sio kuingiza gari kwa kituo cha polisi. Gari iko na stakabadi zote zinazohitajika kubeba abiria,kwa nini mnashukisha abiria"

  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Francis Meja amewaonya waendeshaji wa huduma za usafiri wa umma kuwa wote wanaokiuka sheria za barabarani watachukuliwa hatua.

  "Madereva wengi hawana stakabadhi sahihi. Kama saccho mna jukumu la kuhakikisha wafanyakaz wako wana leseni zinazohitajika.Ukishindwa kufanya hivyo sisi tutasema lete leseni zetu,usibebe abiria"

  Msako huu unatekelezwa kufuatia ilani iliyotolewa na Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi na mwenzake wa uchukuzi James Macharia kuwa magari ya uchukuzi wa umma yatii sheria zote barabarani almaarufu "sheria za Michuki".


  1  2  3  4  5  6  7  
  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako