• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 •  Kongamano la kwanza la Kimataifa la Uchumi wa rasilimali za majini lafunguliwa jijini Nairobi

  (GMT+08:00) 2018-11-27 08:52:39

  Kongamano la kwanza la kimataifa la uchumi wa rasilimali za majini (baharini) lilingóa nanga jana jijini Nairobi katika jumba la mikutano la KICC.

  Kongamano hili la Kimataifa limeandaliwa na Kenya kwa ushirikiano na Canada na Japan.

  Kongamano hilo limewaleta pamoja marais 11 na washiriki zaidi ya 4,000 ambao wanajadiliana kuhusu ustawishaji wa uchumi wa majini.

  Mwanahabari wetu Khamis Darwesh alihudhuria kongamano hilo na kutuandalia ripoti ifuatayo.

  Kenya inangángána kutumia jukwaa hili kubwa la kimataifa kuharakisha katika kufufua uchumi wake wa majini.

  Uchumi wa majini unamaanisha utumizi wa bahari,maziwa na rasilimali zake wa ajili ya maendeleo endelevu ya uchumi.

  Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo jana,Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema Kongamano hili lenye kaulimbiu ya "Uchumi wa majini na ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030" linaipa Kenya fursa ya kujadiliana na nchi mbalimbali kuhusu changamoto na jinsi ya kuboresha uchumi wa rasilimali za majini.

  "Niko hapa kushirikiana nanyi ,nina imani kwamba kwa ajili ya vizazi vyetu vya sasa na vijavyo ,na uwezekano wa kuendelea kwa mazingira yetu tunafaa kutazama maisha ya baadae kwa njia tofauti ya mtazamo chanya wa uchumi wa rasilimali za majini"

  Aidha Rais Kenyatta alisema wajumbe wote wamejumuika jijini Nairobi ili kujitolea kutafuta mbinu za kuendeleza bahari,mito na maziwa.Alisema anafahamu fika kwamba hadi utajiri wa mazingira uhifadhiwe ndipo matunda yaonekane,kauli iliyokokotezwa pia na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

  Akizungumza katika kongamano hilo,Rais Museveni alisema rasilimali ya uchumi wa bahari inafaa kutunzwa kwa hali na mali.

  "Mpango wa Uganda katika suala hili,kwanza kabisa tumeanza kupiga vita uvuvi usio mzuri,bado tunatumia mbinu mbaya za uvuvi,lakini hivi sasa tunataka kuweka rada za kufuatilia wavuvi"

  Naye Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo alisema utajiri uliopo baharini iwapo utatumiwa kikamilifu unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa dunia.

  "Uongozi wangu unatambua kuwa rasilimali hii kubwa ambayo bado haijatumiwa ipasavyo inaweza kuleta mabadiliko katika kushughulikia umaskini,uhaba wa chakula,uhaba wa maji,nishati ,na changamoto za ukosefu wa ajira"

  Marais wengine waliokuwa katika kongamano hilo,ikiwa ni pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni,Filipe Nyusi wa Msumbiji,Dkt Ali Mohamed Shein wa Zanzibar,Uhuru Kenyatta wa Kenya,Abdullahi Mohamed Farmajo wa Somalia,na Danny Faure wa Ushelisheli walieleza nia zao kwa ajili ya uhifadhi na ulinzi rasilimali za majini wakisema kuwa iwapo zitaunganishwa zinaweza kuongeza mara mbili uchumi wa sasa dunia.

  Kenya ndio mwenyeji wa kongamano la kwanza la uchumi wa rasilimali za majini.

  Zaidi ya washiriki 4,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani,katika kongamano hili la siku tatu watajifunza kuunganisha uwezo wa bahari,maziwa na mito ili kuboresha maisha ya watu wote,hususan walio katika mataifa yanayoendelea,wanawake,vijana na watu wote wa kiasili.

  Pia wajumbe watajifunza jinsi ya kupanua uvumbuzi wa kisasa,maendeleo ya kisayansi,na mbinu nzuri za kujenga mafanikio na wakati huo huo kuhifadhi maji kwa vizazi vijavyo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako