• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Viongozi mbalimbali wa Afrika waisifu China kwa ushirikiano na mchango wake katika bara la Afrika

    (GMT+08:00) 2019-02-13 09:41:50

    Viongozi wa Afrika wamekamilisha mkutano wa kilele wa 32 wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa siku mbili mjini Addis Ababa Ethiopia, huku wakipongeza ushirikiano wa kimkakati na China chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika. Viongozi mbalimbali waliopongeza ushirikiano huu ni pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Smail Chergui pamoja na makamishna na wakuu mbalimbali wa umoja huo.

    Akiongea kwenye ufunguzi wa mkutano huo Bw. Faki amesema Umoja wa Afrika ambao umezindua rasmi ofisi yake ya uwakilishi hapa Beijing Septemba 2018 wakati wa mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC, umekuwa na ushirikiano wa kihistoria kwa miaka mingi, na pande hizi mbili zimepata maendeleo makubwa kwenye uhusiano wao.

    Naye Katibu mtendaji wa Mfuko wa Kujenga Uwezo wa Afrika ACBF Emannuel Nnadozie, ameeleza jukumu la China katika pendekezo la Ukanda Mmoja Njia moja na mkutano wa FOCAC kwamba vimeimarisha zaidi ushirikiano kati ya Afrika na China. Amesema wamekamilisha utafiti juu ya Afrika itakavyoweza kunufaika zaidi na pendekezo la Ukanda Mmoja Njia Moja, kwa sababu linatarajiwa sana na Afrika pamoja na China.

    Akizungumzia suala la ujenzi wa uwezo Bw. Nnadozie amesema vijana wa Afrika wamechangia sana maendeleo ya Afrika baada ya kupatiwa udhamini wa masomo na serikali ya China. Amesema wameangalia na kuridhishwa na uungaji mkono katika nyanja mbalimbali unaotolewa na serikali ya China katika kujenga uwezo kwenye maeneo yanayohitajika.

    Akiongea na Shirika la habari la China Xinhua Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Smail Chergui amesema kuwa China ni mshirika mzuri wa AU aliyetoa mchango mkubwa na kuisaidia kamisheni hiyo kukabiliana na changamoto nyingi za amani na usalama zinazolikabili bara hilo, kutoka juhudi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini hadi tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa kwenye mgogoro wa Mali, walinda amani wa China wameshiriki kwenye majukumu mbalimbali ya Umoja wa Mataifa katika Afrika, ikiwemno Sudan Kusini, Jimbo la Darfur la Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Mali.

    Aidha waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Sierra LeoneAlie Kabba, amesema wanakaribisha ushiriki wa China, kwasababu unawapa matumaini kwamba wana msingi imara katika kuimarisha pande nyingi nje ya mipaka, akisema katika miaka ya karibuni kumekuwa na upinzani dhidi ya mfumo wa pande nyingi. Amesisitiza kuwa wanaamini kuwepo pamoja kutahakikisha wanakuwa na mustakabali mzuri kwa kila mtu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako