• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Aina mpya ya mnazi yazinduliwa Kwale,Kenya

    (GMT+08:00) 2019-02-18 08:37:50

    Wakulima katika ukanda wa Pwani nchini Kenya huenda wakaona faida za kilimo cha minazi kufuatia kuzinduliwa kwa aina mpya ya mnazi katika kaunti ya Kwale.

    Hii ni mara ya kwanza kwa wakulima wa nazi nchini Kenya kupanda aina hii mpya ya minazi iliyoboreshwa.

    Aina hii mpya ya mnazi inachukua muda mfupi kukua na pia inatoa nazi nyingi tofauti na minazi ya kitambo inayochukua muda mrefu na kutoa nazi chache.

    Nazi ndio zao kuu la kuwaingizia kipato wakulima na wafanyabiashara katika ukanda wa Pwani,lakini kwa miaka mingi wakulima wamekuwa wakikuza aina za minazi ya jadi ambazo zinachukua takriban miaka mitano hadi kumi kukomaa.

    Mwishoni mwa wiki iliyopita Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Nchini Kenya ilizindua aina mpya ya mnazi katika kaunti ya Kwale,Kusini mwa Pwani ya Kenya,iliyoagizwa kutoka India.

    Aina hii mpya ya mnazi inachukua takriban miaka mitatu kukomaa na pia inatoa nazi takriban 300 tofauti na minazi ya zamani inayotoa nazi 20 hadi 100.

    Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Nchini Kenya Dk Eliud Kirege anasema aina hii mpya ya mnazi itaboresha kilimo cha nazi na kuongeza kipato cha wakulima katika pwani ya Kenya.

    "Sasa hapa leo tunazindua mradi wa nazi ambazo zimeboreshwa.Hapo awali Pwani ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa nazi,na ni ukulima wa maana hapa pwani,lakini uzalishaji ulienda chini sana.Tukizindua huu mradi tunaona kama utasaidia watu wa pwani sana kwa sababu kwa sasa uzalishaji wa nazi unachangia Sh6bn katika pato la taifa ilhali nazi zina uwezo wa kuchangia Sh15bn-20bn.Tunatarajia ya kwamba tukianza kukuza hii miradi ambayo imeboreshwa itaweza kuinua uchumi wa Pwani"

    Nilimuuliza Dk Eliud Kirege kuhusu tofauti kati ya aina za zamani za minazi na hii mpya ambayo imeboreshwa.

    "Tofauti ni nyingi,kwanza ni fupi kwa hiyo kuvuna inakuwa ni rahisi.Pili inakua kwa haraka,miaka mitatu unaweza kupata nazi,na inatioa nazi nyingi sana.Zile aina za zamani zinatoa nazi 20 hadi 100 lakini hii inatoa nazi 300 ambazo ni kubwa.Mkulima akipanda hizi atapata mapato mengi"

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umma la Micro Enterprise Support Program Trust (MESPT),shirika ambalo lilihusika na uagizaji wa miche hiyo ya mnazi hapa nchini,Rapahel Kuria ,anasema :

    "MESPT ilianza kushughulika na mambo ya mnazi hapa katika ukanda wa Pwani mwaka 2008 na tumekuwa na ndoto ya mnazi ulioboreshwa lakini kutokana na mikakati ya kiserikali hatukuweza kuagiza aina hii ya mnazi.Mwaka 2017 mikakti hiyo ilifanywa rahisi na serikali na ndio imetuwezesha kuagiza aina hii mpya ya mnazi.Tumefanya kazi na wshikadau wengine kama vile KALDRO,APHA na KEPHIS ndio tuweze kufikisha miche hii hapa.Kitu muhimu tuliona badala tu ya kusaidia wakulima wapate soko ni vizuri tuwasaidie na aina ya mnazi ambayo inachukua muda mfupi kupata mavuno "

    Mwakilishi wa Katibu katika Wizara ya Kilimo-Idara ya Utafiti na Kilimo,Bi Jane Otado alisema wakulima watauziwa miche ya aina mpya ya mnazi kwa bei ya Sh500.

    "Tumeletewa minazi ya kisasa iliyoboreshwa,na KALDRO wakishathibitisha kwamba hii inatosha tutawasaidia na kuwafundisha namna ya kuitunza vyema ili wapate mazao ya kutosha.Mbegu/miche itauzwa kwa Sh500"

    Wakulima wa minazi katika ukanda wa Pwani wameukaribisha mradi huu wa aina mpya ya mnazi ulioboreshwa na kusema kwamba itasaidia kuwaongezea kipato.

    Mti wa mnazi unatoa bidhaa mbalimbali kama vile nazi,siki,mafuta ya kupikia,ya kujipaka,maji,makuti ya kuezeka nyumba,mbao na kadhalika.

    Mmea huu unapatikana kwa kiasi kikubwa katika ukanda wa Pwani na ni mojawapo ya vivutio vya utalii,huku watalii wengi wakipenda kunywa maji ya madafu.

    Kulingana na Mamlaka ya Maendeleo ya zao hilo,mnazi unaweza kuipatia Kenya hadi USD 250mn katika mapato kila mwaka.

    Hata hivyo zao hilo linaiingizia nchi mapato ya USD 10 milioni kutokana na mbegu mbaya na kukosekana ongezeko la thamani.

    Mamlaka hiyo aidha inasema kuwa ukanda wa Pwani nchini Kenya una miti milioni 8 ya mnazi,lakini mingi yao imezeeka.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako