• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hatuwezi kuongeza mishahara kila mara asema rais wa Kenya

    (GMT+08:00) 2019-02-22 09:21:27

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema serikali haiwezi kuwa na fedha za kuongezea watu wote mishahara kila mara na kuwataka watumishi wa umma wafikirie kwanza wananchi wa kawaida badala ya kuitisha migomo kila mwaka.

    Kenyatta ameyasema hayo huku wauguzi nchini humo wakiendelea na mgomo wakitaka kulipwa posho.

    Tatizo la miaka nenda miaka rudi nchini Kenya.

    Migomo.

    Madaktari leo, kesho waalimu na kesho kutwa wafanyakazi wa mabaraza ya miji.

    Sasa kwa mfano wauguzi wa kaunti kadhaa nchini Kenya wamegoma kwa zaidi ya wiki mbili.

    Na wananchi wamelazimika kutafuta huduma kwenye hospitali binafsi na wale wasioweza kumudu gharama wamesalia bila huduma.

    "Mgomo wa wauguzi umeleta shida kubwa, kwa sababu ukuenda kule mashinani, hakuna madawa. Na kwa sababu hakuna wauguzi inakuwa ni vigumu sana kuhudumiwa", anasema mmoja wa wakaazi katika kaunti Trans Nzoia.

    Huduma za afya nchini kenya ni jukumu la serikali za kaunti.

    Awali wauguzi walisaini mkataba na serikali za kaunti na sasa wanazitaka serikali hizo kutimiza ahadi.

    Lakini kama anavyoelezea Halima Adan mmoja wa wawikilishi wa chama cha wauguzi kaunti ya Machakos, mchakato wa utoaji pesa ni mrefu hivyo unahitaji pia ushirikiano na serikali kuu.

    Kupitia chama chao chao, wauguzi wamekuwa wakiteta kwamba serikali ilipuuza makubaliano.

    "Serikali ndio inasukuma wauguzi kugoma, kukiwa na makubaliano hatutagoma, lakini kwa sasa tutatarajia korti na wizara ya leba itushughulikie" anasema Halima Adan

    Wauguzi katika kaunti 18 wamekuwa wakigoma kwa wiki ya tatu sasa, wakitaka serikali iwaongeze marupurupu waliyokubaliana.

    Walikaidi agizo la mahakama kwamba warejee kazini na kushiriki mazungumzo na serikali kutatua mzozo huo.

    Akiongea katika Kaunti ya Kisii Magharibi mwa Kenya, Rais Kenyatta aliwaonya wafanyakazi wa serikali dhidi ya kususia kazi kila wakati kwa ajili ya kushinikiza waongezewe mshahara.

    "Wafanyakazi wetu wanafaa kufahamu kwamba hatuwezi kuwa tukijadili mambo ya mishahara kila wakati. Pesa haitoshi na hakuna wakati ambao itatosha. Wanadhani hizo pesa hutoka wapi?" alisema Rais Kenyatta.

    Mbali na wauguzi, walimu pia wametisha kugoma wakitaka waongezewe mishahara walivyokubaliana na serikali.

    Hata hivyo, Rais Kenyatta aliwaambia kuwa uchumi wa nchi hauwezi kuruhusu mfanyakazi yeyote wa serikali kuongezewa mshahara.

    Kauli ambayo inaungwa mkono na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

    "Tunataka kuwe na amani katika utumishi wa umma nchini Kenya lakini sio migomo ya kila mara kama vile wauguzi leo, kesho madaktari, waalimu na waalimu wa chuo kikuu. Lakini pesa inatoka mahali pamoja tu"

    Wiki jana, Rais Kenyatta aliagiza serikali za kaunti, ambako wauguzi wanagoma, na Wizara ya Afya kuwafuta kazi iwapo watakosa kurudi kazini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako