• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China na Marekani zina maslahi ya pamoja katika ulinzi wa hakimiliki za ubunifu

    (GMT+08:00) 2019-02-24 16:49:52

    Mazungumzo ya ngazi ya juu ya kibiashara kati ya China na Marekani yanayoendelea mjini Washington, Marekani yamepiga hatua chanya katika masuala ya uwiano wa biashara, kilimo, utoaji wa teknolojia, ulinzi wa hakimiliki za ubunifu, huduma za kifedha na mengineyo. Kati ya masuala hayo, nchi hizo mbili zimeafikiana zaidi katika ulinzi wa hakimiliki za ubunifu, kwani zina maslahi mengi ya pamoja katika suala hilo.

    Kwanza, kulinda hakimiliki za ubunifu ni kwa ajili ya kuongeza uwezo wa ushindani wa kiuchumi. Katika miaka 40 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi ya kufungua mlango, China imesahihisha sheria mbalimbali husika za hataza, chapa na uandishi, na kurekebisha idara kuu ya hakimiliki ya ubunifu, na pia ilianzisha mahakama maalumu inayoshughulikia kesi za hakimiliki za ubunifu. Mwaka jana idadi ya hataza nchini China (isipokuwa Hongkong, Macao na Taiwan ) ilizidi milioni 1.6, ambalo ni ongezeko la asilimia 18.1 ikilinganishwa na mwaka 2017.

    Hata hivyo, China bado si nchi yenye nguvu kubwa katika hakimiliki za ubunifu kama Marekani. Ili kuongeza nguvu hiyo, inaibidi China ikuze ushirikiano na nchi nyingine duniani, ikiwemo Marekani. Marekani ni nchi iliyotangulia zaidi katika uvumbuzi, na ina mfumo na utaratibu kamili wa hakimiliki za ubunifu. Mwaka 2017, China iliilipa Marekani dola bilioni 7.13 za Kimarekani kwa ajili ya kununua hakimili za ubunifu. Katika mapinduzi mapya ya sayansi na teknolojia, Marekani inataka kudumisha hadhi yake ya uongozi kupitia kuimarisha ulinzi wa hakimiliki za ubunifu, ili kupata soko kubwa zaidi. Hivyo suala hilo ni moja kati ya masuala yanayofuatiliwa zaidi na Marekani katika mazungumzo yake na China.

    Pili, ulinzi wa hakimiliki za ubunifu ni wa lazima katika utaratibu wa biashara za kimataifa. Zikiwa nchi muhimu zaidi kibiashara, China na Marekani zina maslahi ya pamoja katika kulinda hakimiliki ya ubunifu. China inahimiza sera ya kufungua mlango, inapaswa kufuata zaidi utaratibu wa biashara za kimataifa. Katika mswada wake wa marekebisho ya sheria ya hataza, China imeweka fidia ya adhabu kwa mara ya kwanza. Mbali na hayo, China imeanzisha mahakama maalumu inayoshughulikia kesi za hakimiliki ya ubunifu, na kuhimiza kusahihisha sheria ya chapa kwa mara ya nne. Kutokana na juhudi hizo, mwaka huu, nafasi ya China duniani katika mazingira ya kibiashara imepanda kwa 32.

    Mashirika ya Marekani yana nia imara ya kulinda hakimiliki zao za ubunifu. Ili kuyasaidia mashirika yake kuongeza uwezo wa ushindani duniani, serikali ya nchi hiyo imeweka suala la kulinda hakimiliki za ubunifu katika sera yake ya kibiashara. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwaka 1975 hadi sasa, mashirika ya Marekani yameyashtaki mashirika ya nchi nyingine kwa makosa ya kukiuka hakimiliki za ubunifu karibu mara 300.

    Tatu, China na Marekani zinapaswa kuimarisha ulinzi wa hakimiliki za ubunifu, ili kuendeleza uhusiano wao kiuchumi na kibiashara. Hivi leo, Marekani ni nchi ya kwanza inayonunua bidhaa za China, na pia ni nchi ya sita kuuza bidhaa zake kwa China.

    Marekani inaitaka China kuimarisha ulinzi wa hakimiliki za ubunifu, na matakwa haya pia yanalingana na mwelekeo wa sera ya mageuzi na kufungua mlango ya China. Wakati huohuo, mashirika mengi ya China pia yameanzisha shughuli katika nchi za nje, hivyo China pia inataka jumuiya ya kimataifa ikiwemo Marekani ilinde vizuri hakimiliki za ubunifu za mashirika hayo.

    Hivi leo wajumbe wa China na Marekani wanaharakisha majadiliano, ili kutekeleza maoni ya pamoja ya viongozi wa nchi hizo mbili. Katika mazungumzo yao, suala la ulinzi wa hakimiliki za ubunifu ni mfano mzuri wa kufikia maslahi ya pamoja. Bila kujali ni maswala gani, kama pande hizo mbili zikizingatia maslahi ya pamoja, zitaongeza maafikiano na kupunguza tofauti, ili hatimaye kufikia makubaliano.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako