Ripoti kuhusu kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira iliyoandaliwa na Baraza la Serikali la China imewasilishwa kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge la umma la China. Kwenye ripoti hiyo, waziri wa mazingira ya ikolojia Bw. Li Ganjie amefahamisha maendeleo muhimu yaliyopatikana kwenye hatua ya kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira nchini China mwaka 2018, akisisitiza kuwa inapaswa kuhimiza utatuzi wa matatizo makubwa ya ikolojia kwa kufuata sheria na kanuni zinazohusika, ili kukidhi mahitaji ya wananchi katika kuboresha mazingira ya ikolojia ambayo yanaongezeka siku hadi siku.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, mwaka 2018 kazi ya China katika kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira imepata maendeleo makubwa, mazingira ya ikolojia yamezidi kuboreshwa, na lengo lililowekwa limekamilika. Hata hivyo waziri wa uhifadhi wa mazingira wa China Bw. Li Ganjie anasisitiza kuwa hivi sasa mazingira ya ndani na ya kimataifa yana mabadiliko ya kina tena yenye utatanishi mkubwa, kazi ya kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira inakabiliwa na changamoto nyingi. Anasema:
"Hivi sasa hali ya uchumi nchini China ina mabadiliko na changamoto wakati inapata maendeleo kwa utulivu, hali ambayo inazifanya baadhi ya sehemu kulegeza usimamizi wa mazingira. Baadhi ya sehemu zinakabiliwa na matatizo makubwa ya uchafuzi wa kimuundo. Ujenzi wa miundo mbinu ya mazingira kwenye eneo la vijijini bado uko nyuma."
Hivi sasa mikoa 31 nchini China imetangaza kanuni za kulinda mazingira ya asili, ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu katika kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Katika mwaka uliopita, Wizara ya uhifadhi wa mazingira imechukua hatua mbalimbali ili kutatua matatizo makubwa katika mazingira ya asili. Ripoti hiyo pia imesisitiza kuwa ni lazima kutoa kipaumbele katika kuhimiza kwa pande zote kazi ya kulinda mazingira, haswa kwa njia ya kuboresha miundo ya viwanda, nishati, uchukuzi na matumizi ya ardhi. Bw. Li ganjie anasema:
"Tunapaswa kuwa na nia thabiti na kuchukua hatua zenye ufanisi, kusukuma mbele kazi ya kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa hatua madhubuti, kuhimiza utatuzi wa matatizo makubwa katika kulinda mazingira ya asili kwa mujibu wa sheria na kanuni, na kuzidi kuboresha mazingira ya ikolojia, ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa mazingira mazuri ya asili yanayozidi kuongezeka siku hadi siku."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |